• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Msanii anayechora Picha kwa Sindano badala ya Brashi Bw. Gu Yuchun

    (GMT+08:00) 2009-12-28 17:03:34

    Siku chache zilizopita kwenye maonesho ya bidhaa za utamaduni yaliyofanyika mjini Shenzhen, picha moja ilivutia sana wafanyabiashara kutoka nchini China na nchi za nje. Hii ni picha iliyotariziwa kwa nyuzi za hariri kwenye karatasi ya aina ya Xuan,picha ambayo inaonekana kama ilichorwa kwa burashi ya wino. Urefu wa picha hiyo ni mita 12, kuna watu 1,200 kwenye picha hiyo, inayoonesha mila na desturi za watu wa mji wa Nanchang katika siku za kale.

      Bw. Guyuchun mwenye umri wa miaka 55 alikulia huko Nanchang, mji mkuu wa mkoa wa Jiangxi. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, alikwenda mji wa Yangzhou mkoani Jiangsu kumfanyia tambiko babu yake, siku alipokuwa huko aliambiwa kwamba babu zake wote walikuwa mafundi wa kazi ya utarizi, hivyo akavutiwa sana na ufundi huo. Tokea hapo akaanza kufanya utafiti kuhusu picha za aina mbalimbali zilizotariziwa, baada ya kufanya utafiti kwa miaka 20 hivi bwana huyo aliibuka na wazo la kutarizi picha kwa nyuzi za hariri kwenye karatasi na kuionesha picha ionekane kama ni picha ya mtindo wa kichina iliyochorwa kwa burashi ya wino. Mwanzoni alitaka kutarizi picha kwenye kitambaa kwa mujibu wa picha zilizochorwa kwa burashi ya wino, lakini baadaye aligundua dosari ya kufanya hivyo alisema,

      "Kwa sababu kitambaa kilichotariziwa picha lazima kiwambwe kabla ya kutariziwa picha juu yake, baadaye kitambaa hicho kinakuwa na mikunjo kutokana na nguvu ya kuvuta, ukitarizi picha kwa nyuzi za hariri kwenye kitambaa kwa mujibu wa picha iliyochorwa kwa burashi ya wino kwenye karatasi, hali halisi ya mandhari ya mito na milima ya picha iliyochorwa kwenye karatasi haiwezekani kuonekana vizuri "

      Bw. Gu Yuchun alichemsha sana bongo kwa muda mrefu ili kutatua tatizo hilo lakini hakupata jibu, baadaye alipata mwanga kutoka kwenye mtandao wa internet. Alisema,

      "Kwenye mtandao kuna data moja inayosemekana kwamba picha za Kichina zilizochorwa kwenye karatasi ya Xuan zinadumu sana, na hakuna sanaa yoyote inayoweza kudumu kama sanaa inavyokuwa kwenye karatasi ya Xuan. Hivyo nikafikiri kama nikitarizi picha kwenye karatasi ya aina hiyo si itadumu vilevile?"

      Lakini wazo lake hilo lilipingwa na jamaa na marafiki zake. Alisema,

      "Jamaa na marafiki zangu wote walikuwa wananipinga wakisema, haiwezekani kwa sababu karatasi ni rahisi kuchanika, sindano ikitoboa yatatokea matundu."

      Basi ni karatasi ya aina gani ya Xuan inayofaa kwa kazi hiyo? hili lilikuwa tatizo gumu kwa bwana huyo. Alichemsha bongo kwa muda mrefu ili kutatua tatizo hilo. Mara nyingi Bw. Gu Yuchun alikwenda mjini Xuanzhou zinakotengenezwa karatasi ya Xuan kwa wingi, alitembea kiwanda kimoja hadi kingine akizungumza na mafundi wengi kuomba ushauri wao, mafundi walifanya majaribio tena na tena na mwishowe walifanikiwa kutengeneza karatasi inayotakiwa. Alisema,

      "Karatasi ya aina hiyo ni tofauti na karatasi zinaouzwa sokoni, karatasi hiyo imetiwa nyuzi za pamba ndani yake."

      Kupata karatasi inayofaa ilikuwa ni hatua kuelekea kufanikiwa kutarizi picha kwenye karatasi, lakini kwa sababu picha za Kichina zilizochorwa kwa burashi ya "wino", na kutarizi picha kwa "nyuzi za hariri" kwa mujibu wa picha za kichina zilizochorwa kwa burashi ya wino, kweli ni taabu sana kuonesha tofauti ya rangi ya wino. Bw. Gu Yuchun alitumia siku zaidi ya kumi akapata ufundi wa kuzifanya nyuzi za hariri ziwe na rangi tofauti kwenye picha zilizotariziwa. Alisema,

      "Kwanza ni lazima nihakikishe kuwa nyuzi za hariri hazing'ari kama kawaida, kwani picha zilizotariziwa kwenye karatasi ni za rangi ya wino, toka mweusi mzito hadi kijivu, na toka kijivu nyepesi hadi weupe. Kwa mfano, kuna aina tatu za rangi ya kijivu, yaani kijivu nzito, ya wastani na nyepesi, yaani kila aina ni lazima iwe na namna tatu tofauti, kwa hiyo kwa jumla nyuzi za hariri zapaswa kuwa na rangi tofauti ya wino hata kwa aina zipatazo 39."

      Mwezi Juni mwaka 2006, Bw. Gu Yuchun alifanikiwa kutarizi picha yake ya kwanza kwenye karatasi kwa mujibu wa picha iliyochorwa kwa burashi ya wino na mchoraji maarufu wa Enzi ya Ming. Alisema,

      "Picha ya kwanza niliyotarizi kwa nyuzi za hariri kwenye karataksi ni kwa mujibu wa picha ya 'tai wawili' iliyochorwa na mchoraji maarufu wa zama za kale sana."

    Bw. Gu Yuchun alitumia muda wa miezi mitatu kutarizi picha hiyo ya "tai wawili" ambayo urefu wake ni mita moja na upana wa nusu mita, hii inamaanisha kwamba sanaa ya picha iliyotariziwa kwa nyuzi za hariri kwenye karatasi ya Xuan kwa mujibu wa picha ya kichina iliyochorwa kwa burashi ya wino imevumbuliwa. Katika picha hiyo Bw. Gu Yuchun aliunganisha kikamilifu ufundi wa kutarizi na uzuri wa picha za wino za Kichina, hivyo ametoa mchango wake kwenye sanaa ya uchoraji wa Kichina.

    Bw. Wu Yinshui ambaye ni mtu mashuhuri anayejihusisha na kutunza picha za kichina zilizochorwa kwa burashi ya wino, alisifu sana picha alizotarizi Bw. Gu Yuchun, akisema,

      "Huu ni uvumbuzi mpya kabisa ambao unaunganisha vizuri ufundi wa kutarizi na uchoraji wa picha za wino za Kichina, sanaa hiyo itakuwa na mustakabali mzuri sana."

      Mwaka 2008 picha alizotarizi kwenye karatasi zilipata tuzo kubwa ya sanaa ya Kichina.

      Hivi sasa, uvumbuzi wa sanaa ya kutarizi picha kwenye karatasi ya Xuan na uvumbuzi wa karatasi inayotumika katika usanii huo, vimepata hataza za taifa. Picha alizotarizi zinatunzwa na wahifadhi wengi wa nchi zaidi ya kumi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako