• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bibi Anna Chennault, "balozi wa kiraia" anayehimiza mawasiliano ya kirafiki kati ya China na Marekani

    (GMT+08:00) 2010-01-07 14:55:38

    Bibi Anna Chennault ni Mchina mwenye uraia wa Marekani. Katika miongo kadhaa iliyopita, amekuwa anafanya juhudi ili kuhimiza maendeleo ya uhusiano wa kirafiki kati ya China na Marekani, kwa hiyo anasifiwa kuwa ni "balozi wa kiraia kati ya China na Marekani".

    Bibi Anna Chennault alizaliwa mwaka 1925 katika familia maarufu mjini Beijing, baba yake aliwahi kusoma nchini Uingereza na Marekani, na alikuwa profesa na mwanadiplomasia. Wakati Japan ilipoivamia China, bibi Anna Chennault alikuwa kijana, alikuwa akiishi na jamaa zake kati ya Hongkong na sehemu za ndani za China, na maisha yao ya wakati ule yalikuwa magumu. Wakati huo baba yake, ambaye alikuwa anafanya kazi nchini Marekani, aliwataka yeye na dada zake waende kusoma nchini Marekani, lakini bibi Anna Chennault alikataa na kubaki nchini China. Alisema,

    "Wakati ule nilikuwa kijana, niliona watu wote wanalipenda taifa letu, na katika miaka ya vita ambayo maisha yalikuwa magumu, ilitubidi tukae pamoja na taifa letu. Ingawa maisha yangu yalikuwa magumu, lakini hali kadhalika maisha ya wengine, kwa hiyo niliona hayo si kitu. Sasa naona wakati ule ulinifanya niwe mwenye nguvu, hivyo uzoefu wa wakati ule una umuhimu mkubwa kwangu."

    Mwaka 1944, bibi Anna Chennault alikuwa mwandishi wa habari wa kwanza wa kike wa shirika la habari la serikali kuu, na alitumwa kumhoji amirijeshi wa kundi la watu wanaojitolea wa jeshi la anga la Marekani AVG lililolisaidia jeshi la anga la China Bw. Claire Lee Chennault. Bibi Anna Chennualt alipokumbusha alipokutana mara ya kwanza na Bw. Claire Lee Chennault alisema,

    "Wakati ule ulikuwa ni mwaka wa mwisho wa mapambano dhidi ya Japan, na nilikuwa mwandishi wa habari, yeye alikuwa amirijeshi wa kundi la AVG, alikuja nchini China kutoka sehemu ya mbali na kuisaidia China kupambana na Japan, hivyo watu wote walimheshimu sana, na mimi pia nilimheshimu sana."

    Baada ya kumalizika kwa vita dhidi ya Japan, bibi Anna Chennualt na Bw. Claire Lee Chennualt walikutana tena mjini Shanghai, wakapendana na kuoana. Wakati huo bibi Anna Chennualt alikuwa na umri wa miaka 23, na Bw. Claire Lee Chennualt alikuwa na umri wa miaka 54. Ingawa umri na utamaduni wao ni tofauti, lakini bibi Anna Chennault alisema, "kama watu wawili wakipendana, basi matatizo mengi yanaweza kuondolewa." Ndoa yao ilisifiwa na watu.

    Mwaka 1949 bibi Anna Chennault alihamia Taiwan pamoja na mumewe, ambapo alishughulikia uandikaji wa vitabu. Mwaka 1960, ambao ulikuwa miaka miwili baada ya mume wake kufariki, bibi Anna Chennault alihamia Washington nchini Marekani pamoja na watoto wake wawili. Kitabu chake cha kiingereza "siku elfu moja za mchipuko" kilinunuliwa na watu wengi baada ya kuchapishwa huko New York. Alitoa hotuba kote nchini Marekani kuhusu hali ya China, kuchambua uhusiano kati ya China na Marekani, pia alieleza utamaduni wa China, ambazo ziliwavutia sana watu nchini Marekani. Lakini akiwa mwanamke mwenye asili ya China, alikabiliwa na changamoto kubwa katika taifa la mume wake. Bibi Anna Chennault alisema,

    "Kikwazo kikubwa zaidi ni kwamba, nchini Marekani, wewe ni mtu mwenye asili ya Asia, wakaona kuwa kwa nini unataka kupata heshima kubwa namna hii?! Hii ndiyo tatizo kubwa zaidi."

    Kutokana na nia yake imara na haiba zake, bibi Anna Chennault alipata ushindi: mwaka 1963 aliteuliwa na rais wa zamani wa Marekani Bw. Kennedy akafanya kazi katika ikulu ya Marekani, ambaye alikuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya China kufanya kazi katika ikulu ya Marekani; mwaka 1970 alikuwa naibu meneja mkuu wa kampuni ya shirika la ndege la AVG, na kuwa naibu meneja mkuu wa kwanza mwanamke katika shirika la ndege nchini Marekani; pia alijiunga na benki kubwa ya Marekani, na kuwa mkurugenzi wa kwanza mwenye asili ya Asia katika bodi ya wakurugenzi; vilevile alichaguliwa kuwa mmoja kati ya watu 70 wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Marekani.

    Baada ya China mpya kuanzishwa, uhusiano kati ya Marekani na China ulikuwa umesimamishwa kwa karibu miaka 30. Bibi Anna Chennault siku zote alifuatilia mabadiliko na maendeleo ya China, na kufanya juhudi ili kuhimiza maendeleo ya uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili. Alitoa mchango mkubwa katika mambo mbalimbali makubwa yakiwemo ziara ya rais wa zamani wa Marekani Bw. Nixon nchini China ya mwaka 1972 na kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Marekani mwaka 1979.

    Mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 1980, baada ya kuondoka kwa miaka 31, bibi Anna Chennault alirudi tena mjini Beijing. Alikuwa mjumbe maalum wa rais wa zamani wa Marekani Bw. Reagan, alimkabidhi kiongozi wa China Bw. Deng Xiaoping barua ya rais Reagen kuhusu kukuza uhusiano kati ya Marekani na China.

    Baadaye bibi Anna Chennault alisafiri mara kwa mara kati ya China na Marekani, ili kuhimiza mawasiliano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali. Bibi Anna Chennault alisema, katika miaka 30 iliyopita, Marekani haikuifahamu China, na China haikuifahamu Marekani, hivyo alieleza na kujulisha hali kati ya nchi hizo mbili.

    Rais Barack Obama wa Marekani alifanya ziara nchini China kuanzia tarehe 15 hadi 18 Novemba. Bibi Anna Chennault alipokumbusha miaka 30 iliyopita, aliona kuwa mabadiliko makubwa zaidi ni kwamba, China na Marekani zimezidisha maelewano, na zinaweza kushirikiana, mambo haya ni muhimu sana. Pia anaona kuwa, pande hizo mbili bado zinahitaji juhudi za muda mrefu ili kutatua matatizo mengi. Alisema,

    "Katika miaka 30 iliyopita, uhusiano kati ya China na Marekani hakika uliendelezwa, lakini haukuendelezwa kama ilivyo sasa. Sasa nchi hizo mbili zinaelewana, na uhusiano kati yao umeimarishwa sana, kwa hiyo kulikuwa na umuhimu mkubwa kwa rais Obama kufanya ziara nchini China."

    Hivi sasa, ingawa bibi Anna Chennault ana umri wa miaka zaidi ya 80, lakini bado anafanya kazi kila siku, na kuitembelea China mara mbili kila mwaka, ili kuhimiza mawasiliano ya kiraia kati ya China na Marekani.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako