• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Urithi wa Utamaduni Usioonekana wa China"-Usanii wa Kutengeneza Vichwa vya Simba kwa Karatasi mjini Guanhu

    (GMT+08:00) 2010-01-18 17:02:25

    Mji mdogo Guanhu mkoani Jiangsu China unajulikana kwa maendeleo ya kasi kiuchumi na usanii wa kutengeneza vichwa vya Simba kwa karatasi. Kutokana na usanii huo kuwa na historia ndefu, serikali imeuweka katika orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana wa China, na Bw. Shi Rongsheng ambaye ana ujuzi mkubwa wa usanii huo amechaguliwa kuwa mrithi wa usanii huo.

    Vichwa vya Simba vinatengenezwa kwa karatasi na gundi, kazi za kutengeneza vichwa hivyo ni pamoja na kufinyanga kichwa cha Simba kwa udongo, kubandika karatasi kwa gundi kwenye kichwa kilichofinyangwa na kutia rangi kwenye gamba la kichwa hicho. Sura ya Simba inatisha kutokana na macho kuonekana makali na kinywa kutanuka, lakini ukiangalia zaidi sura hiyo pia inapendeza na kuchekesha. Wenyeji walio karibu na mji mdogo Guanhu wote wanamfahamu Bw. Shi Rongsheng na kumsifu kwamba yeye ni gwiji wa kutengeneza vichwa vya Simba na ukoo wake umekuwa na ufundi huo kwa zaidi ya miaka 500.

     Mchezo wa kuchezesha Simba wa bandia umekuwa na historia ndefu sana nchini China. Wachezaji wanachezesha Simba wa bandia kwa vitendo mbalimbali huku wakicheza ngoma. Kwa mujibu wa kumbukumbu za historia, mchezo huo ulianza kutokea miaka 1,700 iliyopita katika enzi ya Madola Matatu ya Kifalme nchini China. Na katika enzi za Ming na Qing mchezo huo ulienea zaidi. Bw. Shi Rongsheng alisema,

    "Katika vijiji hakuna burudani nyingi, kwa hiyo katika siku za mwaka mpya wa jadi wa China, watu wanafurika kuangalia maonesho ya mchezo wa kuchezesha Simba wa bandia na kuwasha fataki, hali ya shamrashamra hujaa kote vijijini."

    Ingawa ufundi wa kutengeneza kichwa cha Simba ni kazi inayoweza kupata faida nono, lakini muda wa utengenezaji huwa ni mrefu, tena kazi hiyo inataka watu wawe na ustadi, si rahisi hata kidogo kwa mtu kupata ufundi huo. Msanii anatumia udongo wa ufinyanzi na kuchanganya nyuzi za katani ili udongo usipasuke baada ya kukauka, na baadaye anatengeneza kichwa cha Simba, kisha anabandika tena na tena karatasi nene iliyolowa gundi ili kupata gamba la kichwa hicho. Baada ya kukamilisha kazi hizo zote, anachora sura ya Simba kwa rangi nyekundu, kijani, nyeusi, manjano na nyeupe, na mwishowe anachora kinywa na ndevu. Bw. Shi Rongsheng alisema,

    "kuna kazi zaidi ya kumi za kutengeneza kichwa kimoja, baada ya kufinyanga kichwa, kazi nyingine ni kubandika karatasi tena kwa gundi na baadaye kuchora sura kwa rangi."

    Kwa sababu mchezo wa kuchezesha Simba wa bandia ni burudani isiyoweza kukosekana katika siku za mwaka mpya wa jadi wa China, shughuli za kutengeneza vichwa vya Simba zimewahi kuvutia watu wengi, kama mtu fulani akiwa hodari wa ufundi huo, anaheshimiwa kutokana na mapato yake makubwa. Zamani katika kijiji cha Guanhu kulikuwa na familia kumi hivi zinazoshughulika na kazi hiyo, na familia maarufu kwa shughuli hizo ni familia ya Bw. Shi Rongsheng, hivyo hali ya maisha ya familia yake ilikuwa ni nzuri kuliko familia nyingine. Mke wa Bw Shi Rongsheng, Bibi Liu Yinling alisema,

    "Zamani kichwa kimoja cha Simba kiliweza kuuzwa kwa Yuan kumi wakati yai moja liliuzwa senti tano tu."

    Baada ya kujifunza na kufanya shughuli kwa miongo kadhaa, hivi sasa Bw. Shi Rongsheng licha ya kuwa fundi kama wazazi wake pia ameendeleza usanii huo kwa sura na rangi. Mwaka 1992 UNESCO ilimpa Bw. Shi Rongsheng sifa ya "Msanii Mkubwa wa China wa Sanaa ya Mikono", na kichwa cha Simba alichotengeneza kilisifiwa kuwa ni "Ufundi wa Kipekee wa China". Lakini kadiri miaka inavyopita ndivyo Bw. Shi Rongsheng anavyokabiliwa na hali ngumu, hapo awali aliweza kuuza vichwa kumi kadhaa vya Simba kwa mwaka, lakini hivi sasa anauza vichwa kadhaa tu.

    Ili kupanua biashara yake Bw. Shi Rongsheng anatengeneza vichwa vya Simba kwa ukubwa tofauti, kichwa chenye sentimita 80 anauza Yuan 400 kwa jozi, na kichwa kidogo chenye ukubwa kama ngumi anauza Yuan 200, hata hivyo hawezi kuuza vingi. Mwaka jana aliuza jozi moja tu ya vichwa vikubwa. Kutokana na hali hiyo familia nyingine zinazotengeneza vichwa vya Simba zimeacha na kufanya kazi nyingine, na Bw. Shi Rongsheng pia amelazimika kufanya kazi nyingine, isipokuwa tu anapokuwa nyumbani anaendelea na ufundi wake baada ya kazi. Vichwa vya Simba vimejaa kwenye rafu, Bw. Shi Rongsheng anaviangalia tu asijue la kufanya. Kinachomfariji Bw. Shi Rongsheng ni kuwa mtoto na mkamwana wake wanapenda ufundi huo, kutokana na yeye kuwafundisha wamepata msingi wa ufundi huo. Mtoto wake alisema,

    "Hivi sasa vijana wanaona ufundi huo umepitwa na wakati, lakini mimi naona ufundi huo una thamani, sitaki upotee, kwa hiyo baada ya kutoka kazini najifurahisha kwa ufundi huo."

    Hivi karibuni mtoto wake amefungua duka la kuuza vichwa vya Simba kwenye tovuti ya Taobao ambayo ni tovuti kubwa ya kuuzia bidhaa nchini China. Baada ya kuanzisha duka hilo, Bw. Shi Rongsheng amekuwa na kazi mpya, nayo ni kumhimiza mtoto wake aangalie hali ya mauzo ikoje katika mtandao.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako