• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Shule ya msingi ya kabila la Wajinuo iliyoko chini ya mlima Jinuo

    (GMT+08:00) 2010-01-21 15:37:36

    Kabila la Wajinuo ni kabila dogo lenye historia ndefu, na ni kabila la mwisho kuwekwa katika orodha ya makabila madogo madogo nchini China. Watu wengi wa kabila hilo wanaishi katika sehemu ya Mlima Jinuo iliyoko katika wilaya ya Xishuangbanna mkoani Yunnan. Kila asubuhi, watoto wa vijiji mbalimbali vya kabila la Wajinuo wanakwenda kusoma kwenye shule yao ya msingi iliyoko chini ya Mlima Jinuo. Katika shule hiyo maalumu iliyoanzishwa kwa ajili ya wanafunzi wa kabila la Wajinuo, wanafunzi wanasoma kwa furaha.

    "Kila asubuhi ninafika shuleni saa 12 na nusu, ambapo walimu wetu wanafika saa moja na kutupa kifungua kinywa. Tunaanza masomo saa 2, na baada ya vipindi vinne vya masomo tunakwenda nyumbani kula chakula cha mchana. Saa 8 mchana tunarudi shuleni, na kuingia darasani saa 8 na nusu. Baadhi ya wakati tuna kipindi cha kompyuta."

    Jina la msichana huyo anayekumbuka vizuri ratiba ya shule ni Zhang Kexin, yeye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi ya kabila la Wajinuo, na amekuwa kiranja wa darasa lake kuanzia darasa la pili. Wazazi wa Zhang Kexin wote wanafanya kazi za vibarua katika sehemu ya nje, na anatunzwa na babu na bibi yake. Ingawa familia yake ni maskini, lakini Zhang Kexin anasoma shuleni bila wasiwasi. Kwani shule hiyo imewasamehe ada ya masomo kwa wanafunzi wote. Mkuu wa shule ya kabila la Wajinuo Bw. Yang Shize alisema,

    "Serikali inatoa elimu bure katika shule yetu, hata vitabu vinatolewa kwa wanafunzi bila malipo. Katika shule yetu, wanafunzi wa bweni wanapewa ruzuku ya yuan 50 kila mwezi, ambapo wanafunzi wa makabila madogo madogo wanapewa ruzuku nyingine ya yuan 250 kwa mwaka. Hii ni sera maalumu inayotekelezwa na serikali kuu kwa kabila la Wajinuo. Hivi sasa watoto hawana wasiwasi tena kuhusu tatizo la kiuchumi wanapokuwa shuleni. Kwani hivi sasa wanafunzi wetu hawalipa ada yoyote shuleni, mbali na hayo wanapewa ruzuku."

    Kabila la Wajinuo ni moja kati ya makabila madogo madogo yenye watu wachache zaidi nchini China, na lina watu karibu elfu 22. Kabila hilo lina lugha, lakini lugha hiyo haina maandishi. Ili kuhifadhi na kurithisha utamaduni wa lugha ya kabila la Wajinuo, shule hiyo inawafundisha wanafunzi kwa lugha mbili za kichina sanifu ambayo ni lugha ya taifa ya China na kijinuo. Mwalimu wa shule hiyo anayefundisha lugha ya kijinuo Sha Wenyuan alisema hatua hiyo ina manufaa mawili, alisema,

    "Naona kuwafundisha wanafunzi kwa lugha mbili ni muhimu. Kwa sababu watoto wengi wa kabila la Wajinuo wanapokua, hawajui lugha ya kijinuo, hili litakuwa tatizo kubwa. Wakati watoto wa kabila la Wajinuo wanapoanza kwenda shule, wanafahamu vizuri lugha yao ya kikabila, tukiwafundisha kwa lugha mbili ya kichina sanifu na kijinuo, hawatasahau lugha yao ya kikabila huku wakiweza kujifunza vizuri kichina sanifu."

    Kila asubuhi baada ya vipindi viwili vya masomo, wanafunzi wanakwenda katika kiwanja cha michezo kufanya mazoezi ya mwili. Wanafunzi wa shule ya kabila la Wajinuo wanafanya mazoezi maalumu yanayochanganya vitendo vya michezo na ngoma ya kikabila. Mazoezi hayo si kama tu yanaweza kuwasaidia kujenga mwili, bali pia yanawahimiza kufahamu vizuri utamaduni wao. Mwanzilishi wa mazoezi hayo Bw. Zhao Shunping si mtaalamu wa michezo, bali ni mwalimu wa michezo ambaye amefanya kazi katika shule hiyo kwa miaka zaidi ya 10. Alisema akiwa mmoja kati ya watu wa kabila la Wajinuo, lengo lake la kutunga mazoezi hayo ni kuwafanya watoto wa kabila hilo wasisahau utamaduni wao wa kikabila. Alisema,

    "Nilianzisha mazoezi hayo kwa mujibu wa mchezo wa sanaa wa kabila letu. Tunaona kuwa ili kurithisha utamaduni wa makabila madogo madogo, tunapaswa kuwafahamisha watoto wetu umuhimu wa utamaduni wa kikabila. Baadaye bila kujali wapo sehemu gani, hawataacha utamaduni wao wa kikabila."

    Ikisaidiwa na watu wa hali mbalimbali, shule ya kabila la Wajinuo ilianzisha maktaba moja ndogo yenye vitabu mia kadhaa, na katika maktaba hiyo, wanafunzi wanaweza kusoma vitabu vya aina mbalimbali wanavyopenda. Vilevile shule hiyo pia imeandaa mafunzo ya utarizi wa kikabila, ngoma na muziki, na kuwafurahisha sana wanafunzi.

    Kati ya wanafunzi zaidi ya 700 wa shule ya msingi ya kabila la Wajinuo, zaidi ya asilimia 90 wanatoka vijiji vya tarafa ya Jinuo vilivyoko jirani, wengine wachache wanatoka tarafa nyingine na wanakaa bwenini. Kwa wanafunzi hao, walimu wanabeba majukumu mengi zaidi, kwani wao ni baba na mama zao wa hapo shuleni. Mzazi wa mwanafunzi mmoja wa shule hiyo Liu Yu alisema,

    "Watoto wetu wakiugua, kwanza walimu wanawapeleka hospitali, halafu wanatuarifu. Sisi wazazi hatuna wasiwasi wowote kuhusu watoto wetu wanapokuwa shuleni."

    Waandishi wetu wa habari walipotembelea shule hiyo, walisalimiwa na mwanafunzi mmoja baada ya mwingine. Kutokana na tabia ya wanafunzi hao, waandishi wetu wa habari waliona tabia nzuri ya watu wa kabila la Wajinuo. Shule hiyo inabeba matumaini ya mustakabili wa kabila la Wajinuo, pia imetimiza ndogo yake ya kuwasaidia watoto wa kabila hilo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako