• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bw. Israel Epstein, mwandishi wa habari maarufu aliyejionea maendeleo ya China

    (GMT+08:00) 2010-01-21 15:31:23

    Bw. Israel Epstein alikuwa mwandishi wa habari maarufu aliyejulikana nchini China. Yeye alichaguliwa kuwa ni mmoja kati ya marafiki kumi wakubwa wa kigeni waliotoa mchango mkubwa kwa China na kupendwa zaidi na watu wa China katika miaka 100 iliyopita.

    Bw. Epstein alizaliwa mwaka 1915 katika familia ya Wayahudi iliyofuata Umarx huko Warsaw, Poland. Wazazi wake waliwahi kukamatwa na kufukuzwa kutokana na kushiriki kwenye mapinduzi. Alipokuwa na umri wa miaka miwili, aliambatana na wazazi wake kuja China kupitia Japan.

    Bw. Epstein alisoma na kuishi mijini Haerbin na Tianjin. Alipokuwa mtoto alishuhudia vitendo mbalimbali vya kimabavu vya mabeberu kuikalia China na kuwatendea vibaya Wachina, na kuionea huruma China. Alipokuwa mwandishi wa habari kwenye medani ya vita, alitoa habari nyingi halisi kuhusu jinsi wanajeshi na wananchi wa China walivyopambana na wavamizi kwa ujasiri.

    Ili kufahamisha kwa haraka mambo aliyoyaona katika maeneo yaliyokombolewa, alikwenda nchini Marekani kuandika makala. Katika kipindi hicho, yeye pamoja na mkewe waliwaongoza watu wa hali mbalimbali kufanya maandamano, ili kuipinga Marekani kuingilia kati mambo ya ndani ya China, na kutafsiri kwa Kiingereza wimbo wa Kwaya ya Mto Manjano.

    Mwaka 1951 kutokana na mwaliko wa waziri mkuu wa zamani wa China Zhou Enlai na bibi Song Qingling, Bw. Epstein alirudi mjini Beijing, na kuwa mhariri mtendaji wa gazeti la Ujenzi wa China, yaani gazeti la China Today ya hivi leo, ambalo lilitafsiriwa kuwa la lugha mbalimbali na kuuzwa katika nchi na sehemu zaidi ya 100 duniani. Gazeti hilo linaonesha sura mpya ya China ya hivi leo kwa wakati na kwa pande zote. Wakati huo, alifahamiana na bibi Huang Huanbi. Bibi Huang alisema,

    "Kuanzia mwaka 1960 nilikwenda kwenye ofisi za gazeti la China Today lililoanzishwa na bibi Song Qingling, zamani gazeti hilo liliitwa Ujenzi wa China, kwa kiingereza liliitwa "China iko kwenye ukarabati". Bibi Song Qingling alisema, haifai kutumia jina hili, kwa kuwa hatuwezi kukarabati kila siku, tunapaswa kubadili jina hilo. Baada ya bibi Song Qingling kufariki dunia, gazeti hilo lilibadili jina lake na kuitwa China Today. Nilianza kufanya kazi katika gazeti hilo mwaka 1960, na Bw. Esptein alianza kufanya kazi hapa mwaka 1951, yeye alikuwa mmoja kati ya waanzilishi wa gazeti hilo. Kuanzia hapo tulifanya kazi katika sehemu moja."

    Kutokana na kuwa na matumaini ya pamoja na kufanya kazi kwa pamoja walianza kupendana. Bibi Huang Huanbi alisema, shughuli za Bw. Epstein ziko nchini China, alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

    "Nadhani jambo ambalo alikuwa hawezi kusahau ni, kama alivyoeleza kwenye kitabu chake cha kumbukumbu alichoandika kiitwacho "China nilivyoiona", alikusanya habari huko Yan'an mwaka 1944, wakati huo, Yan'an ilikuwa imewekewa vizuizi na Chama cha Guomindang, na habari hazikuweza kutolewa kwa nje. Aliondoa vizuizi na kuwaandaa waandishi wa habari wa nchi za nje kwenda Yan'an, lakini hakika Chama cha Guomindang kilikuwa na wasiwasi, hivyo kilituma watu wake wengi na kuunda kikundi cha waandishi wa habari wa nchini na wa nchi za nje. Baada ya kukusanya habari, aliweza kuona pale mwanzo wa China mpya, watu wa China walipambana na wavamizi wa Japan kwa ujasiri, kwa hiyo aliandika kwenye kitabu chake kwamba, anaamini kuwa watu wa China walikuwa wanaweka msingi wa kujenga China mpya katika dunia mpya ya siku za usoni."

    Wakati ule akiwa mwandishi wa habari wa magazeti ya New York Times na The Times ya Marekani, alishiriki kwenye kikundi cha waandishi wa habari wa nchini na wa nchi za nje kilichotembelea sehemu za kaskazini magharibi za China, waliondoa vizuizi na kwenda Yan'an. Katika makala yake, Bw. Epstein aliandika alivyoona mwenyewe kuwa: ngano na mtama uliokoma ukionesha kuwa mavuno yanatarajiwa; maharagwe, pamba na mkonge vilionekana hapa na pale.

    Katika barua yake aliyoituma nyumbani kwao, Bw. Epstein aliandika hivi: "Nimeiona China ya hapa Yan'an kuwa ni tofauti kabisa na China iliyotawaliwa na Chama cha Guomindang. China ya hapa Yan'an haina njaa, watu wana hamasa ya ushindi. Yan'an inawafanya watu waione China ya siku za usoni hivi leo."

    Bw. Epstein alishuhudia hali ya vita, pia alikaribisha zama za amani pamoja na watu wa China. Katika maisha yake ya miaka 90, miaka 82 alikuwepo nchini China. Alishuhudia mabadiliko makubwa ya China, na aliona majivuno kwa maisha yake nchini China.

    Mke wake bibi Huang Huanbi alisema, Bw. Epstein alifuatilia sana ujenzi wa mambo ya kisasa wa China. Alisema,

    "Mwanzoni hakufahamu baadhi ya mabadiliko, lakini baadaye alifahamu na kuyasifu mabadiliko hayo. Tulipokwenda nje alisema, sasa China imekuwa nzuri zaidi. Alifuatilia sana kurudisha mamlaka ya China kwa Hongkong, siku ile nzima alitazama TV kuhusu mambo hayo. Pia alikuwa na matumaini kuwa China bara na Taiwan zitaunganishwa tena mapema. Vilevile alifuatilia Tibet, na aliwahi kuandika kitabu kiitwacho Mabadiliko ya Tibet. Alisema kama akiwa na nafasi na afya nzuri, ataandika kitabu kingine. Hata alipolazwa hospitali, aliwaambia viongozi na wenzake kuwa, ana matumaini kuwa anaweza kwenda Tibet kwa garimoshi baada ya kupona."

    Bw. Epstein alifariki dunia mwaka 2005 nchini China. Aliwahi kwenda Tibet kwa mara 4, ingawa matumaini yake ya kwenda Tibet kwa garimoshi hayakutimizwa, lakini akiwa rafiki wa watu wa China, amemaliza kazi yake ya kuijulisha China kwa dunia.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako