• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Urithi wa Utamaduni Usioonekana wa China"-Tamasha la Mashua ya Dragoni Yenye Sanamu za Miungu katika Mji wa Huangshi China

    (GMT+08:00) 2010-01-25 16:51:23

      

    Katika mji wa Huangshi wa mkoa wa Hubei, katikati ya China, kila mwaka kabla ya siku ya tarehe 5 ya mwezi wa 5 kwa kalenda ya kilimo ya China, hufanyika Tamasha la Mashua ya Dragoni Yenye Sanamu za Miungu. Hili ni tamasha linalofanyika kwa ajili ya kuomba Mungu awabariki watu wa sehemu hiyo na kuwapa amani na afya njema, na kumkumbuka mshairi mzalendo wa zama za kale Qu Yuan, kila mwaka watu wanaoshiriki kwenye tamasha hilo wanafikia elfu kumi kadhaa, na tamasha hilo limekuwa na historia ya zaidi ya miaka 2,500 katika mji huo.

      "Tamasha hili lina shamrashamra nyingi na kuwa na uchangamfu sana kuliko sherehe za Mwaka Mpya wa jadi, mimi na familia yangu tunashiriki kila mwaka."

    Mashua ya dragoni yenye sanamu za miungu inatengenezwa kw

    a namna ya kipekee, ina urefu wa mita 7, upana wa mita 2 na kimo chake ni mita 5, ni mashua yenye kibanda na hupambwa kwa michoro, na ina sanamu za miungu wanaoonekana kama wako hai.

      Inafahamika kwamba mashua hiyo inatengenezwa kwa mabua ya majani ila msingi wake tu ndio unatengenezwa kwa mbao, sehemu ya nje inafungwa kwa kitambaa chekundu na sehemu ya bodi ya mashua inatengenezwa kwa mianzi. Kazi ya kutengeneza kichwa na mkia wa dragoni ni kubwa, ambayo inahitaji mianzi mirefu 108 inayoshikamana imara, lakini kazi kubwa zaidi ni kutengeneza sanamu za miungu 108 zinazowekwa ndani ya mashua hiyo.

      Baada ya matengenezo kukamilika, mashua hiyo inafanyiwa tambiko kabla ya kupelekwa mtoni, ikimaanisha kumalizika kwa tamasha hilo la siku 40. Kuhusu sherehe za kupeleka mashua kwenye mto unaotumiwa kwenye tamasha hilo Bi. Zhou Lusheng anaeleza

      "Siku ya kupeleka mashua mtoni ni siku ambayo tamasha hili linakuwa limepamba moto. Asubuhi mapema watu wanajitokeza kushiriki kwenye sherehe hiyo wakiwa wamevaa mavazi ya sikukuu."

      Wakazi wanainua mashua hiyo na kuitembeza kote mjini, kisha inafanyiwa sherehe ya kuwekwa mtoni. Katika kuitembeza mashua hiyo, inapopita karibu na familia moja, familia hiyo inapaswa kuwasha udi, mishumaa na fataki kwa ajili ya kuomba mashua hiyo ifukuze magonjwa ya mlipuko, na kuirushia mashua hiyo mchele na majani ya chai ili kumshukuru mshairi mkubwa Qu Yuan kwa mambo yote mema aliyowafanyia.

      Tamasha la Mashua ya Dragoni Yenye Miungu linapofanyika inakuwa ni siku ambazo majira ya joto yanakaribia kufika, ambapo hewa inakuwa ya unyevunyevu, vijidudu vya kuambukiza magonjwa vinazaliana na maambukizi yanaenea, kwa hiyo licha ya kuwa watu wanafukiza dawa za mitishamba kufukuza vijidudu na kunywa pombe ya mchele na kuoga kwa maji ya dawa za mitishamba ili kujikinga na maradhi, nao pia wanatumia tamasha hilo kuomba Mungu awabariki. Shughuli za aina hizo mbili zote zinalenga kufukuza magonjwa ya mlipuko na maafa.

      Mkazi Dong Liangcai alisema, kabla ya miaka ya 40 ya karne iliyopita, washiriki wa tamasha hilo, licha ya wakazi wa mji huo na sehemu za jirani, pia kulikuwa na watu kutoka miji mikubwa ya Beijing, Shanghai na Guangzhou. Tokea tamasha hilo lianze kufanyika tena mwaka 1984 limeendelea kila mwaka na washiriki wamefikia elfu kumi kadhaa.

      Tarehe 2 Juni mwaka 2006 tamasha hilo liliwekwa katika orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana wa China. Profesa wa Kituo cha Kuhifadhi Utamaduni Usioonekana wa China mkoani Hubei Bw. Wu Zhijian anasema kwamba huu ni utamaduni wa jadi wenye umaalumu wa kieneo, na unatakiwa kuhifadhiwa na kuendelezwa. Anasema,

      "Kuuhifadhi utamaduni huo maana yake ni kama kuhifadhi nguvu yetu sisi wenyewe, sawa na tunavyowatunza wanyama pori na mazingira ya asili. Hii ni nguvu ya sehemu yetu Huangshi na Mkoa wa hubei, pia ni nguvu ya nchi yetu China."

      Hivi sasa mji wa Huangshi unafanya juhudi kubwa ili kustawisha tamasha hilo, naibu mkurugenzi wa Ofisi ya Utamaduni ya Mji wa Huangshi Bw. Li Weiping anasema,

      "Tumepanga mambo manne tutakayofanya, moja ni kutunza mazingira pembezoni mwetu, pili ni kutunza na kukarabati vifaa vya kufanyia sherehe za tamasha hilo, tatu ni kurithisha utamaduni huo na nne ni kujenga jumba la kuonesha utamaduni huo."

      Hivi sasa mji wa Huangshi unadhamiria kuutangaza utamaduni huo duniani na kuomba uwekwe katika urithi wa utamaduni usioonekana duniani. Ni dhahiri kwamba utamaduni huo ukikubaliwa na shirika la elimu,sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO, uchumi wa mji wa Huangshi na shughuli za utalii vitapata maendeleo ya kasi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako