• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mandhari za kuvutia za majira manne ya mwaka huko Jiuzhaigou

    (GMT+08:00) 2010-02-01 17:31:26

    Mkoa wa Sichuan uko kusini magharibi mwa China ukiwa na sehemu ya mashariki ya uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet pamoja na Bonde la Sichuan, na unasifiwa kuwa ni "Mahali pazuri kama mbinguni". Katika mkoa huu kuna raslimali nyingi za utalii ambazo ni pamoja na mandhari nzuri ya milima mikubwa, mila na utamaduni murua wa makabila madogo, chakula na vitoweo maalumu vya kisichuan na opera ya Sichuan. Sasa tunawaeleza kuhusu sehemu mbalimbali zenye mandhari ya kuvutia katika majira manne ya mwaka za Jiuzhaigou, ambayo maana yake ya Kichina ni sehemu ya bonde lenye vijiji tisa, sehemu hii ni maarufu yenye mandhari nzuri ajabu ya mkoa wa Sichuan. Jiuzhaigou iko katika sehemu inayojiendesha ya makabila ya Watibet na Waqiang, sehemu ya magharibi ya mkoa wa Sichuan, China, bonde hilo la milimani lina umbo kama herufi "Y", na linakwenda ndani kwa kilomita zaidi ya 40. Sehemu hii ina vijiji 9 vya kabila la Watibet, hivyo inaitwa kuwa "Jiuzhaigou"

    Bw Nerohem Yam kutoka Israeli anapenda kutembelea sehemu mbalimbali za China, katika miaka kadhaa iliyopita aliwahi kutembelea miji ya Beijing na Shanghai pamoja na mikoa ya Zhejiang na Shanxi, na amefahamu kidogo utamaduni na mila ya China pamoja na sehemu zenye mandhari nzuri za mito na milima. Lakini baada ya kufika Jiuzhaigou, alishangazwa sana na uzuri wa huko. Alisema"Sehemu hii ni nzuri kabisa nchini China, sikuwahi kuona mandhari nzuri ya mabwawa na milima kama hii katika sehemu nyingine, mandhari ya hapa ni tofauti sana na ya sehemu nyingine."

    Jiuzhaigou imekuwa ya ajabu kutokana na maji yake. Maji ni kama roho ya Jiuzhaigou. Kwenye sehemu ya bonde ya Jiuzhaigou kuna mabwawa zaidi ya 100 yenye rangi nyingi za kupendeza yaliyoko milimani, ambayo wenyeji watibet wanayaita "Haizi".

    Maji ya Haizi ni maangavu sana, mawe, majani ma matawi ya miti yaliyoanguka majini yanaonekana kabisa; rangi ya maji yaliyoko katika mabwawa ni tofauti, baadhi yao ni ya rangi ya kijani na mengine ni yenye rangi ya manjano nyepesi inayong'ara. Kwa mfano bwawa Changhai, ambalo ni kubwa zaidi kwenye sehemu ya Jiuzhaigou, ukilitazama kwa karibu, maji yake ni ya kijani na maangavu; na ukilitazama kwa mbali maji ya juu yanaonekana kuwa na rangi ya kibuluu, maji ya bwawa ni tulivu; vivuli vya milima vinaonekana kwenye bwawa, na inaonekana kama picha moja ya kupendeza sana.

    Maji yaliyoko Jiuzhaigou karibu yote ni tulivu, lakini wakati yalipoanguka chini kutoka kwenye genge refu lenye miti mingi, yanaanguka chini moja kwa moja kwa kasi kama maporomoko ya maji na kuunguruma. Moja ya maporomoko hayo ya maji linaloitwa Nuorilang ni lenye upana mkubwa zaidi nchini China, maji yake yanaanguka chini moja kwa moja kutoka kwenye genge lenye upana wa mita zaidi ya 100, maji yake yanaonekana kama pazia moja kubwa, likiwa chini ya mwanga wa jua linatoa rangi za kupendeza kama upinde wa angani.

    Jiuzhaigou, ambayo inaitwa kuwa "mahali kama peponi", iliwekwa katika orodha ya urithi wa maumbile wa dunia na shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa mwaka 1992. Mfanyakazi wa sehemu ya mandhari ya Jiuzhaigou Bi Yang Fuying alisema, mandhari ni tofauti katika majira manne ya mwaka na zote zina umaalumu wake.

    "ikilinganishwa na sehemu nyingine za kusini, majira ya spring yanachelewa kufika kwenye sehemu ya Jiuzhaigou, na yanafika mwezi Aprili na Mei, ambapo maua mbalimbali yanachanua milimani, maua ya mipichi yakiungana na theluji zilizoanguka zinaunda mandhari nzuri ya kuvutia; katika majira ya joto, Jiuzhaigou ni mahali pazuri pa kukwepa joto, huko kuna miti mingi inayostawi pamoja na maji mengi; katika majira ya mpukutiko, sehemu zote zinakuwa na mchanganyiko wa rangi za aina mbalimbali, zinaonekana kama michoro ya rangi ya mafuta; katika majira ya baridi, sehemu zote za huko ni nyeupe, licha ya kuweza kuona mandhari nzuri, watu wanaweza kuona barafu ya buluu, ambayo iko sehemu ya Jiuzhaigou peke yake. Maji ni roho ya Jiuzhaigou, maporomoko ya maji pamoja na mabwawa ya Jiuzhaigou yanaganda kuwa barafu yenye rangi buluu, ndani ya barafu kuna vijiti vya misonobari na vitu vya chokaa, barafu inaonekana kama ambari (amber).

    Tetemeko kubwa la ardhi lilitokea Mei mwaka 2008 mkoani Sichuan, ambalo liliharibu barabara za kuingia kwenye sehemu ya Jiuzhaigou, idadi ya watalii waliotembelea huko ilipungua kwa kiasi kikubwa. Lakini baada ya kufanyika kwa ukarabati na matengenezo kwa mwaka zaidi ya moja, hivi sasa matembezi ya kutalii Jiuzhaigou siyo shida tena. Naibu mkurugenzi wa idara ya utalii ya Jiuzhaigou Bw Lin Jiashui alisema, "Baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, rasilimali za utalii bado ni nzuri, lakini idadi ya watalii ilipungua kwa haraka, idara ya usimamizi wa sehemu ya mandhari ilitumia nafasi hiyo kuboresha ujenzi wa miundo mbinu ya huko, ikiwa ni pamoja na kubadilisha mbao zilizoharibika kwenye njia iliyotengenezwa kwa mbao, ambayo iko kwenye eneo la kuangalia mazingira ya asili ya viumbe ili kuhakikisha usalama wa watalii wakati shughuli za utalii zitakaporejeshwa katika hali ya zamani. Mbali na hayo tulianzisha ujenzi mpya kuhusu sehemu kadhaa za mapumziko na vituo vya huduma vilivyoko kwenye eneo la utalii, vilevile tulifanya usanifu wa kuboresha mazingira ili kukidhi vizuri zaidi mahitaji ya watalii."

    Aidha, idara ya usimamizi ya sehemu ya Jiuzhaigou ilipanga kwa makini mpango wa utalii wa kiutamaduni katika sikukuu ili kuvutia watalii zaidi. Bw Lin Jiashui alisema"Tarehe 9 Januari ya kila mwaka, tunaandaa tamasha la utalii wa maporomoko ya maji ya barafu tukikusudia kuonesha maajabu ya barafu ya Jiuzhaigou, huu ni mwaka wa tano. Tunataka kuonesha mandhari nzuri ya utalii ya majira ya baridi ya Jiuzhaigou, hususan hali shwari ya majira ya baridi, mazingira ya barafu ya ajabu, maporomoko ya maji ya barafu, rangi za kupendeza za mabwawa katika majira ya baridi na mila na desturi za Watibet. Kwa sababu Watibet wana shughuli nyingi za kimila katika majira ya baridi, na lengo la tamasha hilo ni kuwaonesha watalii shughuli na mambo hayo katika majira ya baridi."

    Anga ya buluu, mawingu meupe, milima yenye theluji, misitu yakiungana na maporomoko ya maji, mito na mchanga vinaonekana kama ni lulu iliyodondoka kutoka mbinguni; moto wa kuni, ndafu, ngoma ya Guozhuang na hadithi za kuvutia za kale vinaonesha uchangamfu na utamaduni wa makabila ya Watibet na Waqiang.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako