• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Msanii anayerithisha utamaduni wa kikabila mkoani Xinjiang, Mchonga sanamu Zhang Xinmin

    (GMT+08:00) 2010-02-01 17:28:09

      

    Katika mji wa Urumqi, mkoani Xinjiang China, kuna bustani moja iliyowekwa sanamu zaidi ya 60. Kati ya sanamu hizo inayovutia zaidi ni sanamu yenye mtindo wa utamaduni wa kikabila mkoani humo, hii ni sanamu iliyopewa jina la "Dansi ya Batamaji", ambayo ilichongwa na Bw. Zhang Xinmin, ambaye ni mkurugenzi wa Shirikisho la Wachongaji la Mkoa wa Xinjiang. Bw. Zhang Xinmin alisema alichonga sanamu hiyo kutokana na wazo alilopata kwenye aina moja ya dansi ya kabila la Wa-uyghur inayoiga vitendo vya wanyama wa aina mbalimbali. Sanamu ya "Dansi ya Batamaji" ikionesha wachezaji kadhaa wanaomfuata batamaji mmoja wakimwiga jinsi batamaji huyo anavyotembea.

      Bw. Zhang Xinmin alizaliwa mwaka 1932 katika familia ya kawaida mjini Xian mkoani Shanxi. Mama yake ni mwenye ustadi wa kukata picha kwa karatasi na pia ni hodari wa kutarizi maua, chochote kilichotariziwa na mama huyo kilipendeza sana. Bw. Zhang Xinmin alipenda kuchora picha toka alipokuwa mtoto kutokana na ushawishi wa mama yake.

      Bw Zhang Xinmin alihitimu katika Chuo Kikuu cha Uchongaji wa Sanamu cha Xibei mwaka 1955, na alianza kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mkoa wa Xinjiang alipokuwa na umri wa miaka 23. Katika muda wake wa zaidi ya miaka 30 ya ufundishaji, aliwaandaa wanafunzi wengi hodari. Tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita, kutokana na juhudi kubwa wachongaji walichonga sanamu nyingi, uchongaji mkoani Xinjiang ulikuwa umeingia katika kipindi cha maendeleo ya kasi, na shughuli za uchongaji zinatoa mchango mkubwa kwa ajili ya kuendeleza utalii na mapambo ya majengo mijini mkoani Xinjiang. Hivi sasa ukitembelea miji na wilaya mkoani humo hutakosa kuona sanamu zinazolingana na utamaduni wa huko. Bw. Zhang Xinmin alisema,

      "maendeleo ya uchumi yameharakisha maendeleo ya utamaduni, kwa hiyo baada ya miaka ya 80 ya karne iliyopita ujenzi wa utamaduni umepata maendeleo ya kasi."

      Mwaka 2008 kulikuwa na sanamu zaidi ya 60 zilizochongwa na wachongaji 30 wa mkoa huo na kuoneshwa katika Jumba la kuhifadhi vitu vya Sanaa la Mji wa Urumqi, watazamaji walimiminika kwenda kutazama na kupiga picha mbele ya sanamu hizo.

    Mwaka 2009 Tamasha la Kimataifa la Uchongaji wa Sanamu lilifanyika katika mji wa Urumqi na kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya shughuli za uchongaji mkoani kufikia kiwango cha juu. Kutokana na tamasha hilo mji wa Urumqi umepata heshima katika mambo ya utamaduni na limeupatia mji huo sanamu nyingi. Hivi leo sanamu hizo zenye mitindo tofauti zimewekwa katika bustani ya sanamu, wakazi wanaweza kuzifurahia sanamu hizo bila kulipa. Maonesho hayo ni matokeo ya juhudi za Bw. Zhang Xinmin. Akisema,

      "Nilitumia muda mrefu kuandaa maonesho hayo, kwani mambo mengi yalinizonga yakinisubiri niyashughulikie, lakini baadaye mambo yakapangwa kwa utaratibu, hivi sasa nimepata wasaidizi vijana ambao wote ni wachapakazi, kazi yangu ni kutoa ushauri tu."

      Alipozungumzia kazi yake ya uchongaji Bw. Zhang Xinmin alikuwa na hisia nyingi. Alisema alitumia miaka mingi kujifunza usanii wa uchongaji, kufanya utafiti na kuenzi uchongaji wa kikabila mkoani Xinjiang, kwa miaka mingi alikuwa na matumaini ya kuja kwa maendeleo ya shughuli za uchongaji mkoani humo. Hivi sasa anapotaja maendeleo yaliyopatikana, mzee huyo mwenye mvi alishindwa kujizuia kuonesha furaha yake, akisema,

      "Mtindo wa utamaduni wa kieneo na wa kikabila unapewa kipaumbele na wachongaji wetu wa Mkoa wa Xinjiang, ukitaka sanamu zako zifanikiwe katika ushindani wa uchongaji wa sanamu mkoani humo ni lazima ufanye juhudi za kudumisha mtindo wa utamaduni wa kieneo na wa kikabila katika kazi yako, la sivyo utashindwa kabisa. Tunaamini kwamba vitu vya sanaa ya kikabila ni vitu vinavyovutia duniani, ni lazima utengeneze vitu vinavyopendwa na wananchi."

      Msanii wa Shirikisho la Wachongaji la Mkoa wa Xinjiang Bw. Li Manzhong anakubaliana sana na maoni hayo ya Bw. Zhang Xinmin, Alisema,

    "Katika miaka ya hivi karibuni, niliona sanamu nyingi zilizochongwa na wasanii wa sehemu mbalimbali nchini China, sanamu hizo ziligusa sana hisia zangu. Mimi nashughulikia uchongaji wa vitu vya matumizi halisi, mkoani Xinjiang kuna makabila mengi mbalimbali, na utamaduni wa makabila hayo unaweza kutusaidia katika kazi zetu za uchongaji, kama tutaweza kuelewa vizuri tamaduni za makabila mbalimbali, tutapata mengi ya kusaidia kazi ya uchongaji wa vitu vya matumizi halisi kwenye jamii, nina hakika kwamba kama tutapiga hatua zaidi, uchongaji wa sanamu mkoani Xinjiang utapata maendeleo zaidi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako