• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua0202

    (GMT+08:00) 2010-02-02 16:12:32

    Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa S.L.P 52483 Dubai Umoja wa falme za kiarabu, anasema.

    Ndugu wapedwa, Mwezi January mwaka huu wa 2010, ishara ya matumainio mazuri ya kuboreshwa zaidi uhusiano wa muda mrefu kati ya Jamhuri ya Watu wa China na nchi yangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliweza kuingia katika ukurasa mpya, pale Waziri wa biashara wa China Bw.Chen Deming alipotiliana saini na Waziri wa Fedha na Uchumi wa Tanzania Bw. Mustafa Mkulo chini ya usimamizi wa mheshimiwa Rais wetu Bw. Jakaya Mrisho Kikwete, makubaliano ya fedha Shilingi Bilioni 239 za Kitanzania ikiwa ni msaada wa China kwa miradi mbali mbali muhimu ya kuboresha uchumi na Miundo mbinu nchini Tanzania kama vile Mradi wa kuboresha Teknolojia ya Mawasiliano, Ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar pamoja na kuboresha huduma ya usafiri wa reli kati ya Bandari ya Dar -es -saalam na nchi jirani ya Zambia yaani ( TAZARA ).

    Maoni yangu nikiwa Mtanzania na pia rafiki mkubwa wa Jamhuri ya Watu wa China ni kuwa msaada huo uliotolewa katika kipindi hichi kigumu kabisa cha msukosuko wa fedha duniani, unadhihirisha jinsi gani nia na azma ya China ya kufunguwa ukurasa mpya wa Ushirikiano wake na Bara letu la Afrika, katika kulisaidia bara hilo kujikombowa kutoka enzi za ukosefu wa maendeleo na kuzorota kwa uchumi.

    Fedha hizo zilizotolewa na Jamhuri ya Watu wa China kwa Tanzania zimekuja wakati muafaka sana , ambapo Tanzania kama mataifa mengine ya Afrika imekuwa ikihitaji mno misaada ya Wafadhili katika harakati zake za kujikwamuwa kiuchumi hususani uboreshaji wa Miundo mbinu inayohitajika kama ni "chachu" ya kukuza uchumi wake.

    Wahenga wana msemo usemao " Akufae kwa dhiki ndie rafiki" hivyo Watanzania hatuna budi kuwashukuru pamoja na kuwaenzi Marafiki zetu hawa wa Jamhuri ya Watu wa China , ambao siku zote wamekuwa mstari wa mbele katika kutusaidia kwa hali na mali." UDUMU URAFIKI KATI YA CHINA NA TANZANIA "

    Tunakushukuru sana msikilizji wetu Mbarouk Msabah kwa barua yako na maoni yako juu ya misaada ambayo serikali ya China inajitahidi kutowa kwa nchi mbalimbali za Afrika hususan misaada hiyo iliyotolewa kwa Tanzania ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa Zanzibar pamoja na miradi mingine, ni jambo la furaha na jema kuona urafiki unazidi kuimarika hasa katika kipindi kigumu, na sisi tunauombea urafiki na uhusiano udumu milele. Ahsante

    Msikilizaji wetu Franz Ngogo ambaye baruapepe yake ni rasmanko2003@yahoo.com, Tarime Tanzania. anasema ndg. wa CRI, la msingi ni kuwajulisheni kuwa sherehe za maadhimisho ya miaka 45 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, zinasubiriwa kwa hamu kubwa na wale wote walioshiriki shindano hili. Hilo nimelibaini kutoka kwa wale niliowajulisha ama kuwasaidia kushiriki ima kwa kuwapa orodha ya maswali au kuwaongoza namna ya kutuma. Ambao ni Abdi Magwiza, Daud Kikoti, Magesa Gekora, Marwa Gati, Mogire Machuki, Evans Kizinga, Onesmo Mponda, na wengineo. Ninachoomba ni kuwa wavute subira. Nasema hivyo kwa maana kuwa hizo taratibu ni za nchi mbili. Lakini swali la kuwaulizeni CRI, ni je, wasikilizaji wa China nao watakuja Tanzania kushiriki na kuiwakilisha China? Hilo ni wazi kuwa kila mtu ana hamu ya kuhudhuria sherehe.

    Tunakushukuru sana Bw. Franz Ngogo kwa baruapepe uliyotuma, kuhusu wasiwasi wako wa kufanyika sherehe ya kutoa tuzo ya chemsha bongo ya maadhimisho ya miaka 45 ya uhusiano wa Tanzania na China, sisi tunapenda kukutoa wasiwasi huo kwani sherehe hiyo itafanyika ingawa hatuwezi kukupa tarehe maalum kwasababu hata sisi pia bado hatujapewa taarifa rasmi kuhusu lini itafanyika, na kwa upande wa suali lako kama kuna wasikilizaji wa China watakaokuja Tanzania kushiriki kwenye sherehe hiyo, jibu ni kwamba hakutakuwa na wasikilizaji wa China kwasababu shindano hilo lilikuwa ni kwaajili ya wasikilizaji wetu wa Afrika Mashariki.

    Barua nyingine inatoka kwa Wafula M. Godwin ambaye anatunziwa barua zake na Wambulwa M. Evans wa S.L.P 2588, Bungoma Kenya, anasema naandika barua hii kwa lengo la kuomba kusajiliwa, nilikuwa nikihangaika katika Idhaa nyingine lakini nilipoelezwa kuhusu Idhaa ya Kiswahili ya CRI, nilibadilisha na kuanza kuisikiliza, tangu wakati huo mimi ni msikilizaji maarufu wa redio hii kupitia idhaa ya Kiswahili ya KBC.

    Ningependa kuwajuulisha kuwa matangazo yenu ya kila siku yana manufaa kwa maisha yangu, matangazo na vipindi vyenu ni vya kuelimisha kila uchao, ninamshukuru Wambulwa M. Evans ambaye ni msikilizaji wenu kwa kunifahamisha kuhusu Idhaa ya Kiswahili ya CRI.

    Mwisho naomba kusajiliwa ili pia nianze kushiriki katika mashindano ya chemsha bongo, pia mimi ni sabiki wa salamu napenda na mimi nitumiwe kadi za salamu ili niwe nikiwasabahi jamaa na marafiki kupitia CRI.

    Na msikilizaji wetu mwengine ambaye naye pia anaomba kusajiliwa ni J. M. Mwana wa Amiani Kakamega Kenya, anasema pongezi nyingi kwa kazi njema yenye ujuzi mnayoifanya kupitia kwenye mitambo yenye nguvu kabisa ya CRI inayovuma kote ulimwenguni, mimi ni mgeni kwenye salamu zenu ila sio mgeni kwenye usikilizaji wa idhaa yenu, na napenda sana kusikiliza vipindi vifuatavyo-: Daraja la urafiki kati ya China na Afrika, Kuwa nami jifunze Kichina na Sanduku la barua. Ninahitaji kuwa shabiki kila wakati na kushirikianan na mashabiki pamoja na watangazaji wa Redio China Kimataifa na kusikiliza sauti zote za watangazaji wa Redio China Kimataifa.

    Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu Wafula M. Godwin na J. M. Mwana kwa barua zenu za maombi ya kutaka kusajiliwa rasmi hapa CRI, sisi tunakuambieni kuwa tayari tumeshawasajili na kukuwaorodhesha kwenye majina ya wanachama wetu, kubwa ni kusubiri wakati wowote tutakutumieni kadi za salamu na kuhusu chemsha bongo mnaweza kushiriki wakati wowote tunapoanzisha mashindano hayo.

    Msikilizaji wetu Zuhura Khavere wa S.L.P 34-40602 Ndori Kenya, anasema huku mimi ni mzima na tunawapata vyema bila ya kuwa na dukuduku lolote, pia napenda kuwamwagia salamu zangu kemkem za krismas na mwaka mpya wa 2010.

    Ama kwa hakika nitakuwa mtovu wa fadhila ikiwa sitatoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa huduma zenu kubwa kwetu sisi wasikilizaji. Ninawashukuru kwa kadi za salamu, bahasha zilizolipwa na hivi punde nimepokea picha za mabanati warembo kutoka makabila madogomadogo nchini China, bila shaka nao pia watashukuru kutambuliwa kimataifa, hivyo natoa ombi pekee la kutumiwa picha zenu pia.

    Kwa kuwa bado sijapokea orodha ya majina ya walioshinda katika chemsha bongo ya mwaka uliopita, basi bado ninayo matumaini ya kujishindia angalau shati! jamani sielewi inakuwaje sijawahi kushinda kitu chochote ilhali ninashiriki mashindano ya chemsha bongo ya kila mwaka, ajabu ni kwamba wanaoshinda ni walewale miaka nenda miaka rudi, inavunja moyo. Mwisho nawatakia mafanikio katika kazi zenu.

    Shukrani msikilizaji wetu Zuhura Khavere kwa barua yako, nasi tumefurahi kusikia kuwa umepeta barua zilizolipwa pamoja na picha za wasichana wa makabila madogomadogo nchini China, kuhusu wasiwasi wako wa kushinda kwenye chemsha bongo, tunakuambia kuwa usiwe na hofu kwani kama umejibu vizuri basi utashinda, na si kweli kuwa kila mwaka tunawapa ushindi watu haohao, wanapata ushindi kutokana na kujibu vizuri masuali tunayotoa, hivyo kwa kila atakayejibu vizuri basi tutampa haki yake.

    Msikilizaji wetu Nelson Charles Ombogo wa S.L.P 38-50301 Bunyore Kenya, anasema napenda kutoa pongezi nyingi kwa CRI, kwa kazi nzuri, tunawapokea kwa njia safi na nitafurahi kama mtaweza kunitumia kalenda ya mwaka 2010.Ahsante.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako