• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Urithi wa Utamaduni Usioonekana wa China"-Taa za Mapambo za Beijing

    (GMT+08:00) 2010-02-08 17:12:08

      

    Taa za Mapambo ambazo pia zinaitwa Taa za Sikukuu zimekuwa na historia ya zaidi ya miaka 1,800 nchini China, na ni mapambo muhimu yanayochangia mazingira ya sherehe za sikukuu. Mchana, taa hizo zinazotundikwa mbele ya milango zinaleta mazingira ya furaha, na usiku, taa hizo zinazowaka zinaleta mazingira ya kifahari. Kuna taa za mapambo za aina nyingi katika sehemu tofauti nchini China, lakini Taa za Mapambo za Beijing ni za aina ya kipekee zenye mtindo wa utukufu wa kifalme. Hivi leo serikali imeziweka Taa za Mapambo za Beijing katika orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana wa China.

    Katika kijiji cha Xigu wilayani Pinggu Mashariki mwa Beijing kuna kituo kimoja cha kutengenezea Taa za Mapambo za Beijing, eneo la kituo hicho ni mita za mraba 2000, Bw. Li Banghua ambaye ni mrithi wa ufundi wa kutengeneza taa hizo anasimamia na kufundisha ufundi huo katika kituo hicho. Alisema baada ya kurithishana kizazi kwa kizazi hivi leo Taa za Mapambo za Beijing zimekuwa nzuri zaidi kutokana na ufundi wake mkubwa, vifaa vyake, mtindo wake na ufahari wake. Mzee Li Banghua alisema,

    "Beijing ulikuwa mji mkuu wa enzi sita za kifalme, kila enzi ilikuwa na mafundi wake wengi waliokusanya ujuzi wa kutengeneza taa kutoka sehemu nyingine mbalimbali na kuutumia katika utengenezaji wa taa hizo, kwa hiyo Taa za Mapambo za Beijing ni nzuri kabisa nchini kutokana na usanifu wake, ufundi wake na vifaa vyake, utengenezaji wa taa hizo una masharti magumu."

    Bw. Li Banghua mwenye umri wa miaka 60 alizaliwa katika ukoo uliorithi sanaa za mikono, toka alipokuwa mtoto alipenda sanaa ya uchoraji na sanaa za mikono, baadaye alifundishwa na mwalimu wake Li Dongxue aliyekuwa mtengenezaji wa taa nyekundu kubwa za kasri zilizotundikwa kwenye roshani ya lango la Tian An Men, katika miongo kadhaa iliyopita alibobea katika ufundi wa matengenezo hayo. Hivi leo bwana huyo pamoja na marafiki zake wanajitahidi kuwafundisha vijana zaidi ya kumi ufundi huo na kuwapatia ajira wakulima zaidi ya mia moja katika kituo chake.

    Hivi sasa kundi la Li Banghua linaweza kutengeneza taa za aina kumi kadhaa, na zote ni kazi za mikono za ufundi wa jadi. Taa zenye maumbo ya wanyama zilizotengenezwa na kundi hilo zinatengenezwa kwa mujibu wa deasturi na vitendo vya wanyama, sura zao za kutembea, hata misuli ya wanyama ilionekana wazi kwa nyuzi za chuma.

    Bw. Li Banghua alisema, taa moja iitwayo "Ndege Wote Wamwabudu Phoenix" ilitiwa lehemu karibu elfu kumi, huu ndio ufundi wa kutengeneza Taa za Mapambo za Beijing. Na Bw. Li Banghua anajivunia zaidi na taa ya Mashua ya Dragoni aliyotengeneza katika miaka ya 80 ya karne iliyopita. Alisema,

    "Ni wazo gani lililonisukuma kutengeneza taa hiyo? Wakati huo nchi yetu ilikuwa imeanza kufanya mageuzi, taifa lilikuwa linastawi kwa nguvu kama dragoni. Taa hiyo ina urefu wa mita 2.6 na kimo chake ni mita 1.5, umbo la taa hiyo ni la dragoni na ndani yake kuna matabaka mawili, katika kila tabaka kuna sanamu za farasi na watu, mishumaa inapowaka sanamu hizo zinazunguka kutokana na hewa joto, sanamu za watu zilitengenezwa kwa kitambaa cha hariri, na nyuzinyuzi zinazoning'inia chini ya taa zilisokotwa kwa ustadi maalum, taa hiyo inaonekana ya heshima na kifahari kabisa."

      Taa hiyo ya dragoni ilipata tuzo kubwa, tokea hapo Bw. Li Banghua akiwa na kundi lake alitilia maanani zaidi uvumbuzi wa ufundi. Hivi sasa badala ya mishumaa na taa za umeme anatumia taa za LED ambazo hazina joto, na voti imekuwa wati 3 kutoka 220, maendeleo ya teknolojia licha ya kuwa yamehakikisha usalama bila ya joto, pia yamebana matumizi ya umeme. Zaidi ya hayo Bw. Li Banghua alivumbua ufundi wa kuifunga taa kitambaa, kwamba anahakikisha kitambaa hakichujuki kwenye jua na kinaponyeshewa na mvua nje ya nyumba.

      Utengenezaji wa taa za mapambo unataka ustadi mkubwa kwa kazi ya kila aina, taa kama hizo hutundikwa katika Sikukuu ya Taa na katika siku nyingine hazitumiki sana, kwa hiyo kutokana na mahitaji madogo, ufundi wa matengenezo hayo unakabiliwa na hatari ya kutoweka. Bw. Li Banghua alisema ana matumaini kuwa kituo chake kitaweza kutengeneza taa za aina nyingi zaidi zinazokwenda na wakati ili kuwavutia vijana wengi kwenye ufundi huo wa jadi. Akisema,

      "Nikiwa mrithi wa ufundi wa kutengeneza Taa za Mapambo za Beijing nina jukumu la kurithisha ufundi huo, naona umri wangu unaniruhusu kufanya hivyo. Ufundi huo umekuwa na miaka mingi, ni jukumu langu kurithisha vijana ufundi huo kwani taa za mapambo zinaashiria mwangaza na mustakbali wetu."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako