• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Urithi wa Utamaduni Usioonekana wa China" -Opera ya Huangmei

    (GMT+08:00) 2010-03-02 15:46:33

    Opera ya Huangmei

    Opera ya Huangmei ni moja kati ya opera tano muhimu nchini China. Hapo awali, opera hiyo ilitokea katika wilaya ya Huangmei mkoani Hubei, na ilikuwa inaitwa "nyimbo za Huangmei" au "nyimbo za kuchuma chai", lakini hivi leo opera hiyo imeenea zaidi katika mji wa Anqing mkoani Anhui na wilayani Huangmei mkoani Hubei. Baada ya kuendelezwa katika miaka zaidi ya mia moja iliyopita, hivi sasa opera hiyo imekuwa moja ya opera muhimu nchini China. Michezo ya opera hiyo inavutia sana kutokana na maonesho ya kuigiza na kuimba, na mambo yanayoelezwa katika opera hiyo ni ya maisha ya watu wa kawaida. Michezo maarufu ya opera hiyo ni pamoja na "Ndoa ya Malaika", "Mama mkwe wa Mfalme" na "Mapenzi kati ya Mvulana Mchunga Ng'ombe na Malaika Mfuma Vitambaa".

      Katikati ya karne ya 19, nyimbo walizoimba wachuma chai katika wilaya ya Huangmei mkoani Hubei zilienea hadi katika wilaya jirani ya Huaining mkoani Anhui, na zikachanganywa na miondoko ya nyimbo za wilayani humo na kuwa opera hiyo ya Huangmei, hili ndio chimbuko la opera hiyo. Baadaye mji wa Anqing mkoani Anhui ukiwa kama kituo, opera hiyo iliendelezwa kwa zaidi ya miaka mia moja, ikawa opera muhimu katika mkoa wa Anhui na moja ya opera maarufu nchini China.

      Kutokea kwa opera hiyo kumebadilisha historia ambayo kabla ya hapo opera zote nchini China zilikuwa zinaeleza mambo ya matajiri na maofisa wakubwa wakubwa tu, yenyewe ikawa aina ya opera inayoelezea maisha ya "makabwera", kutokana na hali hii opera hiyo ilipata nguvu kubwa ya ustawi.

      Lakini opera hiyo ilianza kusitawi zaidi baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949. Mwaka 1952 kundi la Opera ya Huangmei la Mji wa Anqing lilikwenda mjini Shanghai kufanya maonesho, mwaka 1954 lilifanya maonesho mengine katika tamasha la taifa la michezo ya opera nchini China, kisha Kundi la Mkoa wa Anhui la opera hiyo lilianzishwa rasmi, na wakati huo huo filamu za "Ndoa ya Malaika" na "Mama Mkwe wa wa Mfalme" zilipigwa na kuoneshwa kote nchini. Tokea hapo opera hiyo inayoeleza maisha ya "makabwera" imekuwa ikikamilika siku hadi siku na kuenea kote nchini China na hata nchi za nje.

    Opera ya Huangmei

      Baada ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za utamaduni, wasanii wa kizazi kipya wa opera hiyo wamekomaa, michezo ya opera hiyo kama vile ya "Malaika wa Saba na Kijana Dong Yong" ilitengenezwa kuwa filamu na kuoneshwa katika televisheni, ikajulikana kwa kila familia na kupata tuzo za aina mbalimbali. Hivi sasa vikundi vya opera ya Huangmei vya mji wa Anqing wilayani Huangmei vinaonesha michezo yao zaidi ya mara mia moja kwa mwaka katika mikoa zaidi ya 20 nchini China, na kwa mwaliko vilikwenda Hong Kong, Taiwan na hata Japan kufanya maonesho. Mwigizaji mashuhuri wa opera hiyo Han Zaifen anasema,

    "Hivi sasa opera ya Huangmei inapendwa sana nchini China na ina watazamaji wengi, hii ni fahari ya mkoa wetu wa Anhui. Nchi moja ikiwa na ustawi kiuchumi tu haimaanishi kuwa ina nguvu kubwa, hadi iwe na ustawi wa kiutamaduni. Naamini kwamba opera ya Huangmei itakuwa na mustakbali mzuri zaidi, pengine opera hiyo itakuwa usanii usioweza kukosekana katika utamaduni wa China."

    Siku chache zilizopita opera hiyo imekuwa na jumba lake la makumbusho. Jumba hilo ambalo ni la kipekee nchini China lilizinduliwa katika maskani yake mjini Anqing. Jumba hilo lina eneo li mita za mraba elfu 9, licha ya kuwepo kwa filamu za zamani kama "Ndoa ya Malaika" pia kuna zana za kisasa zinazooneshwa kwa skrini kubwa kwa kuguswa tu na kidole, kwa kiasi fulani jumba hilo linaonesha safari ya opera hiyo ya Huangmei iliyowekwa katika urithi wa utamaduni usioonekana wa China. Mkuu wa jumba hilo Bw. Yao Zhongliang anasema,

    "Kuzinduliwa kwa jumba hili la makumbusho ya opera ya Haungmei kuna maana kubwa, kwa sababu jumba hili limetoa mchango usio na mbadala. wa kuonesha na kusukuma maendeleo ya opera ya Huangmei nchini China. Watu wengi hawafahamu historia na mchakato wa maendeleo ya opera hiyo na hasa historia yake inayong'ara. Tokea jumba hili lifunguliwe, watu wameanza kufahamu historia ya opera hiyo, huu ni mchango mkubwa wa kuenzi opera hiyo."

      Kuendeleza opera hiyo kwa uvumbuzi na kuitilia moyo wa zama hizi kumekuwa ni nia ya pamoja ya waigizaji wa opera hiyo. Tuna matumaini kwamba michezo mingi zaidi ya opera hiyo inayoendana na wakati itatokea.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako