• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bibi Wang Ge na ustadi wake wa kukata picha za karatasi

    (GMT+08:00) 2010-03-04 16:07:05

    Katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uyghur ulioko kaskazini magharibi mwa China, kuna wakazi wa makabila 13 yakiwemo makabila ya Wauyghur, Wakazakh, Wamongolia, Wahui, Wahan na Waman. Tokea zamani, watu wa makabila hayo tofauti wameishi pamoja kwa urafiki na mshikamano.

    Bibi Wang Ge ni mkazi wa mji wa Urumuqi ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Xinjiang, na ni stadi wa kukata picha za karatasi. Katika miaka kadhaa iliyopita, amekata picha nyingi za karatasi kuhusu hali ya mshikamano kati ya watu wa makabila mbalimbali mkoani Xinjiang.

    Picha za karatasi zinazokatwa kwa mkasi ni aina moja ya sanaa ya jadi yenye historia zaidi ya miaka elfu moja nchini China. Wasanii wanaweza kukata karatasi kuwa picha za aina mbalimbali za watu, ndege, wanyama, miti na mimea kwa kutumia mkasi tu. Picha hizo zinabandikwa kwenye madirisha na milango wakati wa sikukuu au sherehe muhimu. Hivi sasa sanaa ya kukata picha za karatasi imewekwa kwenye orodha ya mali za urithi wa utamaduni usioonekana ya Umoja wa Mataifa.

    Bibi Wang alizaliwa na kukua mkoani Xinjiang. Miaka 35 iliyopita, alikuwa mwalimu, na kuwafundisha wanafunzi masomo ya lugha ya Kichina, uchoraji na muziki. Aligundua kuwa picha za karatasi zinaweza kuwa njia nzuri ya kuwafundisha wanafunzi wake. Alisema,

    "Nilipowafundisha wanafunzi masomo mbalimbali, nilifikiri kuwa labda ninaweza kuwafahamisha vizuri zaidi kwa kuwaonesha picha za karatasi. Kwa mfano ninaweza kuwaonesha picha zilizokatwa kwa karatasi wanapojifunza namna ya kutamka herufi za maneno."

    Baadaye bibi Wang akawa mpenzi wa kukata picha za karatasi, alikata picha za herufi 26 za Kiingereza, wanyama mbalimbali, na wachezaji wanawake wa ngoma wa makabila madogo madogo. Picha hizo ziliongeza ufanisi wa ufundishaji wake, ambapo ustadi wake wa kukata picha za karatasi pia uliongezeka siku hadi siku.

    Mwaka 2000 bibi Wang alistaafu kazi, na jambo la kwanza alilofanya ni kutalii katika sehemu mbalimbali nchini China. Katika safari hiyo ya utalii iliyoendelea kwa mwaka mmoja, alikaa katika mkoa wa Shaanxi kwa muda mrefu zaidi, kwani mkoani humo kuna wasanii wengi hodari wa kukata picha za karatasi. Binti wa bibi Wang Bi Zhao Lu alisema,

    "Baada ya kurudi nyumbani, mama yangu alikuwa na hamu ya kukata picha za karatasi zenye umaalumu wa Xinjiang, kwani anataka kuonesha mila na desturi za Xinjiang kwa kupitia picha za karatasi. Kukata picha za karatasi ni kazi ya kuchosha sana macho ya watu, hivyo awali hatukumwunga mkono, lakini mama yangu alikataa kuacha."

    Katika miongo kadhaa iliyopita, bibi Wang alikata picha nyingi za karatasi kuhusu maisha ya watu wa makabila mbalimbali mkoani Xinjiang. Bibi Wang alisema,

    "Katika sehemu nyingi nchini China kuna sanaa ya kukata picha za karatasi, kwa nini mkoani kwetu hakuna? Sisi waxinjiang ni wakarimu, na tunapenda kucheza ngoma, hali hii inaweza kuoneshwa kwa njia gani? Naona sanaa ya kukata picha za karatasi ni njia nzuri. Picha hizo zinaweza kuonesha umaalumu wa mkoa wa Xinjiang, na kuwafahamisha vizuri watu wengine kuhusu vitu bora zaidi mkoani kwetu."

    Hivi sasa bibi Wang anakata picha za karatasi za "Daolang Maisilaip". Kabla ya kuanza kukata picha hizo, alifanya maandalizi kwa zaidi ya mwaka mmoja. Bibi Wang alionesha picha hizo kwa mwandishi wetu wa habari akisema,

    "Picha hizo zinaonesha hali ya wasichana na wavulana wanavyowakaribisha wageni wakiimba nyimbo na kucheza ngoma. Kichwani mwa msichana huyo ni Nang ambayo ni mkate maalumu wa kiuyghur, na wasichana wengine wanakuwa na matunda vichwani. Nimekata milia mbalimbali ili kuonesha nguo na ngoma maalumu ya kiuyghur. Picha ninayoshika sasa ni kuhusu hali ya wakazi wa makabila mbalimbali mkoani Xinjiang wanavyoishi pamoja kwa mshikamano. Ile iliyoko nyuma ni milima ya Tianshan, Huoyanshan na Bingshan."

    Baada ya kukamilika, picha hizo zitakuwa na sehemu sita na urefu wa mita 10. Hivi sasa bibi Wang amemaliza sehemu tatu. Sehemu hizo zinaonesha mila na desturi, ala za muziki za makabila mbalimbali, ngoma mkoani Xinjiang, sehemu nyingi bado hazijakamilika zitahusu hasa nguo za jadi za makabila mbalimbali mkoani humo.

    Tarehe 5 mwezi Julai mwaka jana, tukio la kimabavu lilitokea huko Urumuqi mkoani Xinjiang. Akiwa mkazi wa Xinjiang, bibi Wang alishangaa na kukasirika sana na tukio hilo. Hata hivyo anafahamu sana urafiki na mshikamano ulioendelea kwa muda mrefu kati ya watu wa makabila mbalimbali mkoani Xinjiang hauwezi kuharibika. Aliamua kukata picha nyingi zaidi za karatasi ili kuonesha na kueneza urafiki na mshikamano huo. Alisema,

    "Napenda zaidi kukata picha za karatasi siku hadi siku, kwani picha hizo zinaweza kuonesha hisia ya binadamu. Katika mkoa wetu wa Xinjiang, kuna makabila mbalimbali, na watu wa makabila hayo wanategemeana. Tunapaswa kushirikiana na kushikamana vizuri ili kueneleza nyumbani kwetu."

    Hivi sasa kukata picha za karatasi ni sehemu muhimu ya maisha ya bibi Wang. Baada ya kustaafu kazi kutoka shule, amekuwa na wakati wengi zaidi kufanya mambo anayopenda kufanya. Lakini jambo analotaka zaidi kufanya ni kuwafahamisha watu wengi zaidi kuhusu sanaa ya kukata picha za karatasi, na kuwaambia watu wa sehemu za nje kuhusu urafiki na mshikamano kati ya watu wa makabila mbalimbali mkoani Xinjiang.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako