• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Benki zasaidia wanawake kujiendeleza kibiashara nchini Kenya

    (GMT+08:00) 2010-03-11 14:28:08

    Katika karne ya 21 wanawake wa Afrika na kote ulimwenguni wako mbioni kujiendeleza kiuchumi kwa kufanya biashara. Serikali nyingi na mashirika ya fedha yametenga hazina maalum ili kufadhili kwa njia ya mikopo biashara za wanawake.

    Kwenye makala haya tutakueleza wajibu unaotekelezwa na benki kusaidia wanawake kujiendeleza kibiashara hapa nchini Kenya. Makala yetu yanaanzia nyumbani kwa Anna Njeri ambaye hufanya biashra ya kuuza maziwa.

    Anna Njeri ameamka tayari kumkamua ng'ombe wake. Yeye ni mmoja kati ya maelfu ya wanawake wa Kenya ambao wamenufaika na mikopo kutoka benki na kujiendeleza kiuchumi. Tunapofika nyumbani kwake tunaona wateja wa kununua maziwa tayari wakisubiri bidhaa hiyo. Amekuwa akifanya biashara hii kwa muda wa miaka kumi.

    Lakini biashara yake haikuwa nzuri hapo awali hadi pale alipopata mkopo kutoka kwa benki moja ya humu nchini na kununua ng'ombe wa gredi ambaye anatoa maziwa kwa wingi. Alisema:

    Mapema mwaka wa 2000 benki za hapa nchini Kenya zilianzisha vitengo maalum kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanawake. Tukitayarisha makala haya tulitembelea benki moja humu nchini ili kupata maelezo kuhusu vile wanawake wamekuwa wakiomba mikopo ya kufanya biashara.

    Benki ya Equity ambayo ilianzisha hazina ya mkopo wa wanawake iitwayo wanawake katika biashara yaani women in Business. Hazina hiyo ilianzishwa na benki hiyo kwa ushirikiano na serikali ya Kenya na shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP.

    James Mwangi ni mkurungezi mkuu wa benki ya equity, anasema asilimia 54% ya wateja wake ni wanawake wanaochukua mikopo ya kufanya biashara kufuatia kuanzishwa kwa hazina hiyo.

    Eunice Njeri ni mama muuguzi na mwenye zahanati ya Marura nursing home. Katika siku za mwanzo za kazi yake hakuwa na vifaa mwafaka za kufanya kazi. Kwa hivyo kama walivyofanya kinamama wengine, aliamua kwenda kwa benki na kuomba mkopo ili kupanua huduma kwenye zahanati yake. Kufuatia mkopo huo sasa anaweza kuhudumia wagonjwa kwa njia ya kisasa kwani alinunua mitambo na vifaa vinavyohityajika. Anaelezea vile alivyofaidika na mkopo huo.

    Anna Njeri anasema anaona tofauti kubwa kwenye biashara yake baada ya kupata mkopo huo, sasa anaweza kuelimisha watoto wake na kujikimu kimaisha.

    Kabla ya kupata mikopo kutoka kwa Benki, wanawake hupata ushauri jinsi watakavyowekeza na aina ya biashara itakayowafaa. Hii inawasaidia kutumia pesa kwenye biashara mwafaka itakayoleta faida kwa haraka ili kuwawezesha kulipa tena mikopo.

    Bwana Denis Musau ni afisa wa utoaji mikopo katika benki ya Equity. Anaeleza kuhusu idadi ya wanawake wanaoomba mkopo kila mwezi na ushauri wa kibiashara wanaotoa kwa wanawake.

    Aidha benki zinawashauri wanawake kuchukua mikopo mingine baada ya kulipa kikamilifu ile ya kwanza ili kupanua biashara zao.

    Bi. Anne Njeri anauza lita arobaini za maziwa kila siku na hivyo basi ataweza kulipa kwa haraka mkopo wake. Anasema angependa kupata mkopo mwingine kupanua zaidi kilimo cha ufugaji.

    Kufikia sasa karibu asilimia 45 ya wanawake wanafahamu kuhusu mikopo ya biashara na wanaweza kuomba pesa kutoka kwa benki. Asilimia nyingine 40 hawajapata ufahamu wa kutosha kuhusu mikopo hii ya kujiendeleza na kwa hivyo benki tofauti zimeajiri maafisa wa nyanjani ili kutoa ufahamnu kwa vikundi vya kinamama kuhusu mikopo ya biashara.

    Serikali ya Kenya ilianzisha chama cha maendeleo ya wanawake mwaka wa 1952 kuwasaidia kujiendeleza katika vikundi, kulinda haki zao na kushiriki katika uongozi. Hadi leo chama hicho kina zaidi ya vikundi 700 vya wanawake na zaidi ya wanawake milioni tatu walio wanachama.

    Kujihusisha kwa wanawake katika biashara kupitia kwa mikopo ya benki ni ufanisi mkubwa sio tu kwa familia zao bali pia kwa taifa kwa jumla. Ili kuwawezesha wanawake kunufaika vilivyo kutokana na mikopo ya biashara, benki zimeweka viwango vya chini vya riba ili kuvutia idadi kubwa ya wanawake wanaoomba mkopo.

    Takwimu za shirika la Umoja wa mataifa la maendeleo yaani UNDP zinaonyesha kwamba asilimia 48% ya wanawake walio katika maeneo ya mashambani wanaishi chini ya dola moja kwa siku. Vilevile takwimu hizo zinaonyesha kuwa asilimia 63% ya wanawake wanaoishi mijini hutumia dola moja katika maisha yao ya kila siku. Hata hivyo asilimia 85% ya biashara ndogondogo zinamilikiwa na wanawake ambao wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha na maarifa ya kufanya biashara.

    Kenya ina watu milioni 38.3 hivi. Kati ya idadi hiyo ya watu kuna wanawake milioni 19.38. Watu wanaongezeka kwa kasi ya asilimia 2.6%.

    Hivyo basi mpango wa benki, serikali na Umoja wa Mataifa kuanzisha hazina maalum za biashara kwa wanawake ni hatua muhimu ambayo itawezesha asilimia 50.6 ya wanawake kuinua kiwango chao cha maisha na kuboresha uchumi wa taifa kwa jumla.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako