• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Urithi wa Utamaduni Usioonekana wa China" --Sikukuu ya Mwaka Mpya ya Kabila la Walisu "Kuoshi"

    (GMT+08:00) 2010-03-15 19:57:28

    Katika sikukuu ya Mwaka Mpya wa jadi wa China au "Sikukuu ya Spring", watu wa makabila yote ya China hufanya shamrashamra za kila aina na kufanya matambiko kwa miungu na mababu zao wakikaribisha mwaka mpya na kuomba mavuno mazuri. Utamaduni huo pia unafuatwa na watu wa makabila mengi madogo madogo mkoani Yunnan kusini magharibi mwa China. Licha ya Sikukuu ya Spring, watu wa makabila madogo madogo mkoani Yunnan wana sikukuu yao wenyewe ya mwaka mpya. Kabila la Walisu ni moja kati ya makabila hayo, kwa matamshi ya lugha ya kabila hilo "Kuoshi" maana yake ni sikukuu ya mwaka mpya, utamaduni wao wa namna ya kusherehekea sikukuu hiyo umewekwa katika orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana wa China.

    Hapo awali Walisu waliishi katika sehemu ya mpaka kati ya mikoa ya Sichuan na Yunnan, baadaye walihamia kwenye bonde la Mto Nujiang kaskazini mwa mkoa wa Yunnan na mwaka 1954 walianzisha wilaya inayojiendesha ya Walisu. Katika historia, watu wa kabila hilo wamewahi kutumia maneno ya aina tatu ya kuandikwa. Mtaalamu wa mila na desturi za kabila la Walisu Bw. He Yongxiang anaeleza,

    "Kabila la Walisu ni kabila lililovuka moja kwa moja kutoka mwishoni mwa jamii ya asili ya kabila hilo mpaka jamii ya leo. Utamaduni wa kabila hilo ikiwa ni pamoja na maisha, uzalishaji mali, itikadi na namna ya kusherehekea sikukuu, bado uko katika hali ile ile ya mwishoni mwa jamii ya jadi, kwa hiyo hali hiyo ambayo ni tofauti kubwa kati ya utamaduni wao wa asili katika jamii ya sasa inavutia sana."

    Hali ya hewa ya wilaya wanayoishi Walisu pia ni ya ajabu, watu husema "hali ya anga ni tofauti kila baada ya kilomita kadhaa", kutokana na uzoefu, Walisu wamepata ujuzi wa kushughulikia mimea tofauti kutokana na majira tofauti. Wamevumbua kalenda yao wenyewe kwa mujibu wa mabadiliko ya majira, na kila mwaka maua ya cheri yanapochanua ni sikukuu ya "Kuoshi" yaani sikukuu yao ya Mwaka Mpya. Bw. He Yongxiang alisema, "Neno 'Kuoshi' linatokana na maneno mawili ya kichina: Kuo na Shi, 'Kuo' maana yake ni mwaka, 'Shi' maana yake ni kusherehekea na kutambika, maneno hayo mawili yakawa neno moja Kuoshi, maana yake ni kusherehekea Mwaka Mpya."

    Tarehe 20 Desemba ya kila mwaka ni siku ya "Kuoshi", lakini bado haijajulikani siku hiyo ilianzia lini, wazee wa kabila hilo wanasema, tokea karne ya 17 wamekuwa na mila ya kusherehekea "Kuoshi".

    Kila mwaka baada ya wazee wenye heshima kuamua siku ya "Kuoshi", kila familia huwaarifu jamaa wanaofanya kazi katika sehemu nyingine warudi nyumbani, na wanakuwa kwenye pilikapilika za maandalizi ya sikukuu. Katika siku ya kwanza ya Mwaka Mpya kila familia huandaa unga wa mchele unaonatanata uliotiwa maji katika kinu kikubwa kwa ajili ya chapati, na vishindo vinasikika hapa na pale. Katika sikukuu ya "Kuoshi" wanafamilia wanakaa nyumbani bila kutoka kuwatembelea jamaa na marafiki zao, kwa kuwa wanahofia baraka za familia yao zitaondoka na wageni waliokuja nyumbani, na chapati ya kwanza waliyopika ni lazima itumike kufanya tambiko. Bw. He Yongxiang anasema,

    "Walisu wanaona haifai kumiliki mavuno ya mwaka mzima, kwa hiyo kwanza wanawafanyia tambiko babu zao kwa chakula kwa maana ya kuwashukuru kuwapitisha mwaka salama na wapate mavuno mazuri na hali nzuri katika mwaka mpya."

    Baada ya shughuli za kufanya tambiko kwa siku tatu, siku ya nne wanaanza kutoka nyumbani kuwatembelea jamaa na marafiki. Wasichana na wavulana wanachukua fursa hii kujipatia wachumba wao. Walisu wana desturi za "kuoga katika majira ya Spring", wanakwenda penye chemchemi ya moto kuoga wakiwa na chakula na mahema, ambapo wanakusanyika pamoja na kuoga ili kuondoa maradhi na kuongeza nguvu za kujikinga na maradhi. Pamoja na hayo, kila kijiji hufanya shamrashamra za kila aina kama vile kucheza bembea, kufyatua mishale, kushindana kuimba na kunywa pombe.

    Pombe ni kitu muhimu katika matambiko yao, na pia ni kinywaji kisichoweza kukosekana wakati wa kuwakirimu wageni. Kuna aina mbili za pombe wanayotengeneza, moja ni tindi, na nyingine ni mvinyo mtamu wenye rangi kama maziwa na haina nguvu, tindi ni pombe kali na haina rangi. Kwa mujibu wa mila na desturi, mwenyeji anatakiwa kujimiminia pombe glasi yake kisha anamwaga kiasi sakafuni ikimaanisha kuwafanyia mababu zao tambiko, baadaye anakunywa, na baada ya yote hayo anawamiminia wageni na kuwapa kwa mikono miwili.

    Katika siku za "Kuoshi" jambo linalovutia na kutia hofu ni mchezo wa "kupanda mlima wa visu na kupitia bahari ya moto", pia unaitwa "kuparamia mlingoti wa visu". "Kupanda mlima wa visu" una maana ya kupanda mti wenye urefu wa mita zaidi ya kumi, visu 36 vinafungwa kwenye gogo la mti huo kwa ncha juu, mtu anapanda mti huo bila viatu na baada ya kufika mwisho anatundika kitambaa chekundu na kutupa mbegu, baada ya kushuka atapitia "bahari ya moto" yaani atapita makaa yanayowaka akionesha ushupavu wa Walisu. Mkuu wa Kundi la Nyimbo na Dansi la Kabila la Walisu Bw. Yang Yuanji anaeleza,

    "'Mchezo wa kupanda mlima wa visu na kupita bahari ya moto' unatokana na hadithi ya kale inayomwelezea shujaa Wang Ji wa kabila hilo aliyeuawa na maadui katika mapambano dhidi ya wavamizi, alikuwa mwenye ushupavu wa kuthubutu 'kupanda mlima wa visu na kupita bahari ya moto'. Walisu wanafanya mchezo huo kila mwaka ili kumkumbuka shujaa huyo."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako