• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maonesho ya Maingiliano ya Utamaduni wa zama za kale kati ya China na Ulaya yafanywa katika Jumba la Makumbusho la Beijing

    (GMT+08:00) 2010-03-22 11:21:56

    Maonesho makubwa mawili yanafanyika kwa pamoja katika Jumba la Makumbusho la Beijing, maonesho ya kwanza ni kuhusu historia ya mmisionari Matteo Ricci wa Italia alipokuwa nchini China kueneza utamaduni wa Ulaya zaidi ya miaka 400 iliyopita, na mengine ni maonesho ya vyombo vya kauri vya China vilivyokuwa vinauzwa katika nchi za Ulaya katika karne ya 18. Maonesho hayo mawili yanayofanywa kwa pamoja yanaonesha wazi hali nzuri ya maingiliano ya utamaduni kati ya China na Ulaya katika zama za kale.

    Mmisionari wa Italia Matteo Ricci alikuja China mwishoni mwa karne ya 16, wakati ambapo nchi za Ulaya zilikuwa zikistawi kwa nguvu kutokana na kufanya Harakati za Kufufua shughuli za usanii na mapinduzi ya sayansi, na China ilipokuwa ikitawaliwa na mfalme Wanli wa Enzi ya Qing. Kutoka Italia, nchi iliyo mbali na China, Matteo Ricci alileta kioo cha pembetatu nchini China, saa ya kivuli cha jua, saa yenye kengele, elimu za hisabati, unajimu na jiografia, na aliwajulisha maofisa na wasomi wa Enzi ya Ming mashine ya hali ya juu, picha za rangi ya mafuta zinazoonesha vitu jinsi vilivyo na "Kitabu cha asili cha Hesabu za Maumbo". Kwa mujibu wa kitabu cha kiada cha historia kinachotumika nchini China, Matteo Ricci ni mzungu wa kwanza kuleta sayansi na vitu vya sanaa nchini China.

    Mwaka huu wa 2010 utakuwa ni mwaka wa 400 toka Matteo Ricci afariki dunia na ni mwaka wa 40 toka China na Italia zianzishwe uhusiano wa kibalozi, na pia ni mwaka wa utamaduni wa China nchini Italia. Maonesho yaliyopewa jina la "Matteo Ricci --- Mjumbe wa Maingiliano ya Utamaduni na Sayansi kati ya China na Ulaya Mwishoni mwa Enzi ya Ming" yanafanyika katika Jumba la Makumbusho la Beijing kwa ushirikiano wa China na Italia. Naibu mkurugenzi wa Idara ya Mabaki ya kale ya Utamaduni ya China Bw. Zhang Bai kwenye ufunguzi wa maonesho hayo alisema,

    "Mmisionari wa Italia Matteo Ricci alikuja China kueneza sayansi za Ulaya za unajimu, hisabati, jiografia, akawaamsha wasomi wenye fikra za kisasa, na kuwapa hamasa ya kutafiti na kujifunza elimu za Ulaya. Miaka 400 iliyopita Matteo Ricci akiwa mjumbe wa utamaduni wa Ulaya alifanikiwa kujenga daraja la maingiliano ya utamaduni kati ya China na Italia, na leo hii baada ya miaka 400, vitu adimu vya utamaduni na sanaa vya nchi mbili vilivyokuwa katika enzi hizo vimekutanishwa tena."

    Italia ilichagua kwa makini vitu zaidi ya 70 kwa ajili ya maonesho hayo ikiwa ni pamoja na picha zilizochorwa na Raphael na Titian, vitabu kuhusu ujenzi na sayansi na teknolojia vikionesha mafanikio mapya baada ya Harakati za Kufufua shughuli za usanii zilizofanyika kati ya karne ya 16 na 17. Vitu zaidi ya 60 vya China yakiwemo mapambo ya nguo, picha za kuchorwa, usanii wa maandiko ya Kichina na sanamu za Buddha vimeshirikishwa kwenye maonesho vikionesha kiwango cha utamaduni na sanaa katika karne hizo.

    Mwanasayansi wa Taasisi ya Utafiti wa Mabaki ya Kale Bw. Yang Hong alisema, kwa kuangalia vitu vinavyooneshwa kwenye maonesho mawili watazamaji wanaweza kuelewa dunia ilivyokuwa wakati huo. Alisema,

    "Kwa kuangalia vitu vinavyooneshwa kwenye maonesho yote haya mawili, watu wanaweza kufahamu hali ilivyokuwa katika nchi za Mashariki na Magharibi, Matteo Ricci kwa kazi yake kubwa aliunganisha pamoja utamaduni wa pande mbili, ingawa alikuwa ni mmisionari, lakini mchango wake mkubwa alioutoa ni kujulisha utamaduni wa Ulaya."

    Mtazamaji mwenye umri wa miaka 14 Song Dawei alisema, anamjua Matteo Ricci kutokana na kusoma kitabu cha historia, ana matumaini kuwa katika siku za usoni yeye mwenyewe ataweza kwenda nje ya nchi kujionea mengi. Anasema,

    "Naona vitu vilivyoletwa na Matteo Ricci ni vizuri sana, sikufikiria kwamba vitu kama hivyo vilikuwepo katika enzi hizo za kale. Ni vizuri kuwa na maingiliano ya vitu vizuri ili pande mbili zipate maendeleo."

    Maofisa wa Italia nchini China pia wana matumaini kuwa maonesho hayo yatasukuma mbele maingiliano ya kiutamaduni na kirafiki kati ya serikali za nchi mbili na wananchi wao, Bw. Gian Mario Spacca alisema, fikra za Matteo Ricci za kusukuma mbele maingiliano ya utamaduni kati ya Mashariki na Magharibi zinatakiwa ziendelezwe hadi sasa. Alisema

    "Naona Matteo Ricci alikuwa na fikra kwamba pande mbili zikiwa na tofauti kubwa zinahitaji zaidi kuwa na maingiliano, tutaendelea kufuata fikra hizo za Matteo Ricci, kwa upande mmoja tunakubali kuwa kuna tofauti kati yetu, kwa upande mwingine tumekuja hapa na elimu zetu na matumaini yetu ni kufanya mazungumzo na maingiliano."

      Vyombo vya kauri ni moja ya mavumbuzi makubwa katika China ya kale. Maonesho mengine yanayofanywa pamoja na maonesho ya historia ya Matteo Ricci alipokuwa nchini China ni "Maonesho ya Vyombo vya Kauri vya Enzi ya Qing vilivyokuwa vikiuzwa Nje ya China". Vyombo vya kauri karibu 200 vilivyotengenezwa katika Enzi ya Qing iliyoanzia mwaka 1644 hadi 1911 na hasa katika karne ya 18, vilikuwa na mchango mkubwa kwa uchumi, uchoraji wa picha na maingiliano ya utamaduni kati ya China na Ulaya. Kwa mujibu wa takwimu zisizokamilika, katika karne ya 18 vyombo vya kauri vya China vilivyosafirishwa kwenda Ulaya havikupungua milioni 60.

    Naibu mkurugenzi wa Jumba la Makumbusho la Beijing Bi. Yao An alieleza kwamba jumba lake kwa makusudi limepanga maonesho hayo mawili yafanyike kwa pamoja. Alisema,

    "Mwishoni mwa Enzi ya Ming mmisionari Matteo Ricci alikuja China, lakini wakati huo China ilikuwa na ushawishi gani kwa nchi za nje? China haikupokea tu vitu vilivyoletwa kutoka nchi za nje, pia ilieneza utamaduni wake nje ya China, ndio maana tunafanya maonesho ya vyombo vya kauri vilivyouzwa nchi za nje. Katika Enzi ya Qing hali ilikuwaje kwa vyombo vya kauri vilivyouzwa nje ya nchi? Machoni mwa wazungu vyombo vya kauri vya China vilikuwa na thamani kubwa. Kila walipoona merikebu zenye matanga mengi zikionekana kwa mbali kutoka kwenye gati, basi walifahamu kwamba vyombo vya kauri vya China vinakuja. Vyombo vya kauri vya China vilikuwa vinapendwa sana na familia za matajiri na wafalme."

      Vyombo vya kauri vya China vilivyouzwa katika nchi za nje vilitengenezwa kutokana na walivyopenda wazungu, na vilikuwa tofauti na vyombo vilivyouzwa hapa China kwa rangi na maumbo. Kwenye vyombo hivyo kuna michoro ya mtindo wa Kichina inayowavutia wazungu, michoro hiyo ni ya ndege na maua, mandhari ya asili na inayohusu maisha ya watu."

      Mtaalamu wa vyombo vya kauri Bw. Hu Yanxi aliandika kitabu kimoja kinachoeleza mvuto na athari za vyombo vya kauri vya Enzi ya Qing kwa nchi za nje, alisema,

    "Kabla ya mwaka 1710 vyombo vya kauri vya China vilikuwa tunu katika nchi za Ulaya, kwa sababu wakati huo Ulaya haikuweza kutengeneza vyombo vya kauri, mwanzoni vyombo vilivyouzwa huko vilikuwa sawa na vilivyouzwa nchini, baadaye wazungu walitoa maombi yao ya kuonesha maisha ya Wachina. Wakati huo hakukuwa na kamera, kwa hiyo kwenye vyombo vya kauri ilichorwa michoro ya kueleza maisha ya Wachina."

    Bw. Hu Yanxi alisema, michoro ya maua na ndege kwenye vyombo vya kauri iliwavutia sana wazungu, kwa hivyo vyombo hivyo ni vitu vinavyowakilisha utamaduni wa China. Aliongeza kuwa, "Mvuto wa utamaduni wa China wenye miaka elfu tano una ushawishi mkubwa kwa jamii ya tabaka la juu barani Ulaya."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako