• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wageni watapata huduma za afya zitakazotolewa na upande wa tatu wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai

    (GMT+08:00) 2010-03-29 15:03:09

    Kama tujuavyo, maonesho hayo yatakayofunguliwa tarehe 1 Mei yanatazamiwa kuwavutia watalii milioni 70 kutoka nchi mbalimbali duniani. Je, watalii wakikumbwa na ajali au kusumbuliwa na tatizo la kiafya wakati wanapotembelea maonesho ya kimataifa, watasaidiwa vipi? Katika kipindi cha leo, tutawaelezea jinsi huduma za afya zitakazotolewa na upande wa tatu wakati wa maonesho hayo zitakavyowasaidia watalii.

    Kwa nini tunasema huduma hizo zinatolewa na upande wa tatu? Kwa sababu huduma hizo hazitolewi moja kwa moja na hospitali na zahanati, bali zitatolewa na baadhi ya makampuni ya kitaalam.

    Wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai, makampuni hayo yatatoa huduma mbalimbali za afya kwa watalii wanaohitaji msaada, zikiwemo huduma ya kuwatuma wahudumu wa afya kwenye sehemu walizopo watalii, na kutoa matibabu papo hapo, au huduma ya kutoa ushauri wa kitaalam kwenye simu na kuwaambia watalii ni nini kinachotakiwa kufanywa kwa wakati huo. Hata watalii watapata huduma husika wakati wanapokwenda kuonana na madaktari au wanapolazwa hospitalini. Umaalum wa huduma za aina hiyo ni kwamba zitapatikana kwa urahisi na kuwafikia wagonjwa haraka. Watalii kutoka nchini na nchi za nje wanachohitaji kuwa nacho ni kadi ya pesa aina ya Mastercard tu, ndipo wataweza kupata huduma hizo.

    Bw. Deng Juhan anafanya kazi kwenye kampuni moja inayotoa huduma za afya za aina hiyo. Amefahamisha kuwa

    "Wateja wa Mastercard wa nchi za nje wakihitaji msaada wowote wa kiafya wakati wa maonesho ya kimataifa, watapata huduma kwa lugha mbili ambazo ni Kiingereza na Kichina, na huduma hizo zitapatikana kwa saa 24 kwa siku."

    Hapo awali huduma za aina hiyo ziliwahi kutolewa wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008, ambapo watazamaji wa michezo mbalimbali walihudumiwa vizuri. Wakati ule, watu wenye tikiti za michezo hiyo waliweza kupata huduma za afya bila malipo. Kama mtazamaji akikumbwa na ajali, kulikuwa na gari la kubebea wagonjwa iliyompeleka hospitali, ambapo aliweza kupata huduma ya kwanza ya Yuan zisizozidi elfu tano, kiasi ambacho ni sawa na dola 730 za kimarekani. Wakati wa Michezo ya Olimpiki, huduma ya aina hiyo ilisifiwa sana na watalii kutoka nje ya China.

    Hivi sasa, mfumo wa huduma zinazotolewa na upande wa tatu umekuwa ukiendelezwa kwa kasi, kiasi kwamba umekuwa na mtandao mkubwa wa huduma na raslimali nyingi za matibabu. Kwa mfano kampuni ya HealthLink Service ambayo makao makuu yake yako mjini Beijing, ina madaktari 139 walioingia mkataba nayo katika miji 37, ambao wanajua Kiingereza na kuweza kutoa huduma wakati wowote. Huduma za kampuni hiyo zinapatikana kwenye hospitali zaidi ya elfu 1 zilizoko katika miji 52 kote nchini China, pamoja na miji ya kisiwa cha Taiwan. Naibu mkuu wa kampuni hiyo Bibi. Piao Xinji alisema:

    "Wakati kampuni yetu ilipoanzishwa, kituo cha kupokea simu cha kampuni yetu kilikuwa kimesajiliwa kwenye mfumo wa ISO9001. Madaktari na wauguzi wetu wote wana vyeti vya kutoa huduma ya kwanza vilivyotolewa na Shirika la Moyo la Marekani, na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya kwanza kwa watu wanaozimia au watu ambao wana matatizo ya moyo kusimama ghafla."

    Watalii wa nchi za nje wanaotembelea China hukabiliwa na tatizo la kutojua Kichina, ambalo huwaletea shida nyingi wakati wanapokaa hapa nchini. Wakati wanapohitaji huduma ya afya, kuwasaidia kwa kutumia lugha wanayofahamu ni muhimu sana.

    Wapokeaji simu kwenye kituo cha simu ambacho kiko wazi kwa saa 24 kwa siku wote ni wauguzi wanaojua Kiingereza, nao madaktari wanaotoa huduma ya afya pia wanajua Kiingereza. Mtalii akipata tatizo la kiafya, anachohitaji kufanya ni kupiga nambari 120 ambayo ni nambari ya simu ya kuomba huduma ya kwanza.

    "Unataka baba yako alazwe hospitali nyingine?"

    "Ndiyo"

    "Hospitali unayotaka kumpeleka iwe na huduma ya matunzo ya saa 24, si ndiyo?"

    "Ndiyo, baba yangu anahitaji matunzo ya saa 24."

    Mgeni mmoja anaongea na mpokeaji simu, akitaka baba yake atolewe kwenye hospitali moja iliyoko Mji wa Jinchang, kaskazini magharibi mwa China, na apelekwe kwenye hospitali nyingine yenye mazingira mazuri zaidi na wahudumu wa afya wanaojua Kiingereza. Kituo hiki cha kupokea simu kilichoko mjini Beijing kiliwasiliana mara moja na hospitali zilizoko mjini Jinchang, na kupendekeza kwa mgeni huyo kuhusu hospitali inayofikia matakwa yake na kumsaidia kumpeleka baba yake kwenye hospitali hiyo.

    Tatizo lingine linalowakabili wageni wakati wanapopewa huduma ya afya nchini China ni namna ya kulipa gharama za matibabu. Bibi. Piao Xinji anaondoa wasiwasi huo wa wageni akisema watalii wanaweza kulipa gharama za matibabu kwa kutumia kadi ya pesa aina ya Mastercard. Alisema:

    "Katika miji na hospitali zinazoshirikiana nasi, hakuna haja kwa wateja wetu kuzilipa hospitali moja kwa moja, sababu sisi tutatoa hati ya dhamana kwa hospitali zilizowahudumia wateja wetu, na sisi ndio tunaozilipa hospitali."

    Wasikilizaji wapendwa wakati utakapotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Shanghai, kama ukihitaji msaada wowote wa kiafya, mkumbuke, piga nambari ya simu ya huduma za afya za dharura, ambayo ni 120, mara moja utapata maagizo ya kitaalam na huduma mbalimbali za afya.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako