• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0406

    (GMT+08:00) 2010-04-06 16:38:44

    Msikilizaji wetu Khaoya N. Norman wa S.L.P 4365 Kitale Kenya anasema napenda kuchukua fursa hii ya pekee kuandika barua hii nikiwa na furaha nyingi.

    Kwa upande wa elimu mimi ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya juu ya Bungoma, pia napenda kuwadokeza kwamba mimi napendelea sana wakati wa mapumziko kusoma, kutazama televisheni, kusafiri na vilevile kupata marafiki wapya, na hili ndilo hasa lengo kuu la barua hii, mbali na hayo pia napenda kusikiliza Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa.

    Pia napenda kuwahimiza kuwa kila mnapotekeleza mambo yoyote itawagharimu bidii hasa upande wa kielimu, kwani mtaka cha mvunguni sharti ainame. Jambo la mwisho ambalo napenda kuwahimiza ni kuwa mara tu tunavyojuana ndivyo mapya tunavyopata, nilitambulishwa na mjomba wangu Ayubu Mutanda kwa CRI, tafadhali ningependa pia kujumuishwa na marafiki kutoka huko China, nambari yangu ya simu ni +254727315911, na anuani yangu ya barua pepe ni normankhaoya@yahoo.com na mwisho napenda kuwatakia nyote kila la heri kwa mwaka huu.

    Na barua nyingine inatoka kwa BIBI Halima Ijeiza wa S.L.P14-40602 Ndori Kenya, yeye kwanza anasema namshukuru Maulana kwa fursa hii ya kuwasiliana nanyi, awali ya yote pokeeni salamu zangu za dhati huku nikitaraji kuwa mwaendelea vyema na pilikapilika za kila siku.

    Nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa zawadi za mara kwa mara kutoka kwenu, hivi karibuni nimepokea zawadi za kalenda ya mwaka 2010, bahasha iliyolipwa na kadi za salamu, nashukuru kwa haya mawasiliano ya mara kwa mara jambo ambalo linatia moyo sana endeleeni hivyohivyo kwani asiyekujua hakuthamini.

    Jambo ambalo limenifurahisha na kunitia moyo ni kusikia kuwa hivi karibuni serikali ya China imetoa msaada wa mashine ambayo ina thamani kubwa kwa vijana wetu wanaotoa huduma kwa taifa, jambo hili linaonesha uhusiano mzuri ulioko kati ya serikali yetu na ya China, salamu na shukurani kwa wananchi wote wa China, idumu nchi ya China, idumu nchi yetu ya Kenya.

    Shukurani nyingi wasikilizaji wetu Khaoya N. Norman na BIBI Halima Ijeiza kwa barua zenu mlizotutumia, na kuhusu barua ya Khaoya N. Norman ya kutaka kuunganishwa na marafiki wa China, sisi tunasema kwa vile umetupatia anuani yako basi tutajitahidi kuitoa kwa marafiki wa China na mwisho tunawaomba muendelee kututumia maoni yenu.

    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa S.L.P 161 Bariadi Shinyanga Tanzania, leo anaanza kwa kusema nawashukuru kwa moyo wa dhati wafanyakazi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa kwa habari, vipindi na matukio muhimu mnayotutangazia na tunamatumaini makubwa kwamba mtaendelea na moyo huo wa kutuhudumia sisi wasikilizaji wenu kwa ukamilifu.

    Leo napenda kuzungumzia kuhusu tetemeko kubwa la ardhi lilitokea tarehe 14 Januari mwaka huu wa 2010 huko nchini Haiti ambapo lilisababisha maafa makubwa ya watu kupoteza maisha, majengo kuporomoka, hasara kubwa ya mali ikiwemo miundo mbinu muhimu na kupelekea kuvurugika kwa mfumo wa kila siku wa maisha ya wananchi wa Haiti.

    Sisi watu wa nchi nyingine tulijuulishwa na kuhabarishwa kwa kina tukio hilo na athari kubwa zilizojitokeza kufuatia maafa yaliyosababishwa na tetemeko hilo nchini Haiti, serikali ya China ilichukua hatua za dharura na za haraka ambapo ilituma kikosi cha uokoaji ambacho kiliwasili tarehe 16 Januari na ndege kubwa ya shirika la ndege la China ikiwa imebeba vifaa na misaada mbalimbali ya kibinaadamu kwa ajili ya kuwasaidia wahanga mbalimbali wa tetemeko hilo.

    Kwa mujibu wa ripoti na vyanzo kadhaa vya habari ikiwemo Redio China Kimataifa, kikosi hicho kutoka China kimefanya kazi kubwa na nzito ya uokoaji na kutafuta miili na watu waliofunikwa na vifusi vya majengo yaliyoanguka. Uamuzi wa China kwenda nchini Haiti kuwasaidia wananchi wa huko ni jambo la kutia moyo na faraja sana kwa jamii yoyote iliyostaarabika katika nchi yoyote ile. Ni ukweli uliowazi kwamba China ni nchi pekee iliyojipambanua na nchi nyingine nyingi zilizioendelea na zinazoendelea kwani mara tu yanapotokea maafa au janga lolote katika nchi nyingi duniani bila kusita wala kuchelewa inachukua hatua za haraka na kwa wakati za uokoaji wa maisha ya watu na mali. Hali hii inajenga imani na matumaini makubwa kwa serikali ya China na wananchi wake katika jumuiya ya kimataifa, hivyo tunaishukuru na kuipongeza sana kwa moyo huo na vitendo hivyo maridhawa vya huruma na utu wa hali ya juu.

    Aidha tunaishukuru pia Marekani kwa misaada na juhudi kubwa ilizoonesha kwenye zoezi hilo la uokoaji na kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo la ardhi nchini Haiti. Kwa ujumla nchi nyingi na mashirika mbalimbali yaliguswa na kuhuzunishwa sana na maafa hayo na pia tunawapongeza kwa misaada mbalimbali ya kibinaadamu waliyotoa kuisaidia Haiti.

    Mashirika na asasi za kiraia kama vile msalaba mwekundu, hialali nyekundu n.k zitaendelea kutoa misaada kadiri ya uwezo wao. Na ninatoa pole kwa familia za wananchi wanane wa China ambao wamepoteza maisha yao kwenye tetemeko hilo la Haiti, tunatoa pole kwa wananchi wote wa Haiti waliopoteza ndugu zao na mali zao, pia tunatoa pole kwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Bw. Ban Ki Moon kwa msiba wa kumpotoza afisa mwandamizi wa umoja huo, Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hicho kigumu cha huzuni na majonzi makubwa.

    Zaidi ya hayo juhudi na mikakati ya China ambayo haijikiti tu kwenye shughuli za uokoaji wa majanga kama ya matetemeko ya ardhi lakini pia China imejidhatiti na kubobea katika masuala mengi yenye manufaa makubwa kwa wanadamu, ikiwemo mipango na miradi mbalimbali ya ustawi na maendeleo nchini China, barani Afrika na katika dunia nzima. Nawatakia mafanikio zaidi na usalama wakutosha katika kujenga nchi yenu. Ahsante sana.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Kilulu Kulwa kwa maoni na maelezo yako kuhusu China kushiriki haraka zaidi kwenye shughuli za uokoaji mara tu lilipotokea tetemeko la ardhi huko Haiti, kwa kweli maafa ya Haiti yalikuwa ni ya dunia nzima na nchi yoyote ilipaswa au inapaswa kutoa msaada wa haraka, ndio maana China iliamua kuchukua hatua za haraka kuwasaidia ndugu wa Haiti.


    1 2
    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako