• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mtaalamu wa mambo ya kale wa China Bw. Yu Xiaoxing

    (GMT+08:00) 2010-04-12 17:02:02

    Mji wa Zhengzhou uliopo katikati ya China ni moja kati ya miji mikubwa minane ya kale nchini China, katika mji huo kuna sehemu 26 za mabaki ya kale ya ngazi ya taifa. Kutokana na ugunduzi mkubwa uliofanywa na wataalamu wa mambo ya kale, mji huo umekuwa unavutia kutokana na utamaduni mkubwa wa kale. Bw. Yu Xiaoxing ni moja kati ya wataalamu hao wa kale ambaye ni wa kizazi cha kwanza kabisa tangu Jamhuri ya watu wa China ianzishwe.

    Bw Yu Xiaoxing ana umri wa miaka 68, ni mrefu wa wastani na ana mwili wa kukakamaa, wakati wote anapoongea huonesha tabasamu. Mwaka 1960 kikundi cha kutafuta mabaki ya kale kilianzishwa katika mji wa Zhengzhou, Bw Yu Xiaoxing alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa kwenye kikundi hicho, tokea hapo amejihusisha na mambo ya kale mwaka nenda mwaka rudi, na sasa ni karibu miaka 50 imepita. Bw. Yu Xiaoxing anakumbuka wazi jinsi mazingira ya kazi yalivyokuwa magumu mwanzoni mwa shughuli za kikundi chake. Anasema,

      "Kazi ya kutafuta mabaki ya kale hufanyika nje ya mji, kama sehemu tulipokuwa tunafanya kazi si mbali na mjini basi tulienda kwa baiskeli, kama ilikuwa ni mbali tulienda kwa basi, kila mahali tulikaa huko kwa siku kumi hivi, hata kwa miezi kadhaa, na chakula tulikipata kutoka kwa wenyeji wa huko."

      Mji wa Zhengzhou ni mji mkuu wa Mkoa wa Henan, utamaduni wake wa hali na mali uliovumbuliwa na watu wa kale ni mkubwa kuliko ulivyofikiriwa na ulivyoandikwa kwenye nyaraka za kale. Katika miaka kadhaa iliyopita, Bw. Yu Xiaoxing aliwahi kusimamia uchimbuaji wa mabaki yaliyoyeyusha madini ya chuma katika Enzi ya Han iliyokuwa kati ya mwaka 202 K.K. hadi 220 B.K., hekalu la Dahai wilayani Xingyang, mabaki ya kazi ya kukalibu katika wilaya ya Chucun na msingi wa hekalu la Kaiyuan mjini hasa Zhengzhou pamoja na mabaki mengi mengine madogo madogo.

      Kila alipogundua mabaki ya kale, Bw. Yu Xiaoxing alionesha heshima kubwa kwa uwerevu wa wahenga. Aliposimamia uchimbuaji wa mabaki ya kuyeyusha chuma aligundua sepetu moja ndogo, alisema,

    "Sepetu hiyo ya Enzi ya Han ilikuwa nyembamba kiasi cha milimita mbili tu, kutokana na kupakwa madini kwenye pande mbili, sepetu hiyo ilikuwa ngumu kama chuma cha pua."

    Ugunduzi huo wa mabaki ya kuyeyusha madini ya chuma yaliufanya mji wa Zhengzhou ujulikane mara moja miongoni mwa wataalamu na ulisababisha Mkutano wa Kimataifa wa Taaluma ya Uyeyushaji wa Madini ya Chuma ufanyike katika mji wa Zhangzhou mwaka 1986. Bw. Yu Xiaoxing alisema,

    "Wataalamu walishangaa walipoona mabaki hayo ambayo tanuri moja linaweza kuyeyusha madini na kupata chuma tani moja kwa siku, ujazo wa tanuri ni mita 50, na linaweza kukifanya chuma kiwe chuma kilichoweza kufulika, lakini ufundi huo wa kupata chuma kilichoweza kufulika haukupatikana mpaka mwaka 1941 nchini Uingereza, lakini China ilipata ufundi huo kabla ya Uingereza kwa miaka 1900."

    Bw. Yu Xiaoxing kwa furaha alifungua daftari la kumbukumbu kuhusu ugunduzi wa mabaki ya kale, ndani ya daftari hilo karibu nusu ya mabaki yaligunduliwa naye au alisimamia ufukuaji wake. Kati ya magunduzi hayo, moja ni ugunduzi uliowashangaza sana wataalamu wa mambo ya kale. Alisema

    "Kiwanda cha Chakula cha Xiangyang kilitaka kufunga mashine moja kubwa, ambapo viligunduliwa vitu kadhaa vya kale kwenye shimo lililopo chini ya ardhi kwa kina cha mita tano, nilikwenda kuangalia nikaona kumbe ni vyombo vya kupikia vyenye umbo la mraba au duara na ukubwa tofauti, ambavyo kwa Kichina vinaitwa "Ding", na vyombo vya pombe, kati ya vyombo hivyo, kikubwa zaidi kina kimo cha mita moja."

    Vyombo vilivyofukuliwa kutoka kwenye shimo vilikuwa 13 na vyote ni vya shaba nyeusi, na chombo kilicho kikubwa zaidi cha kupikia chenye umbo la mraba kimehifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Mji wa Zhengzhou. Mwaka 1984 Bw. Yu Xiaoxing alipewa uhamisho akashika kazi katika Ofisi ya Mambo ya Kale ya Mji wa Zhengzhou, ili kushughulikia kazi ya kuhifadhi mji huo wa kale

    Tarehe 5 Novemba mwaka 2004 ilikuwa siku muhimu kwa mji wa Zhengzhou, siku hiyo mkuu wa Shirikisho la China la Wataalamu wa Miji ya Kale Bw. Zhu Shiguang alitangaza kuwa mji wa Zhengzhou umekuwa moja kati ya "Miji Minane ya Kale ya China" sawa na miji ya Xi'an, Beijing, Luoyang, Kaifeng, Nanjing, Hangzhou na Anyang. Hayo ni matokeo makubwa sana katika historia ya maendeleo ya taaluma za miji ya kale.

    Kuchaguliwa kwa mji wa Zhengzhou kuwa mji wa kale kuliwafariji sana wataalamu wa mambo ya kale wa kizazi cha kwanza wa China. Bw. Yu Xiaoxing alistaafu mwaka 2004, lakini kutokana na ushabiki wake anaendelea kushiriki katika mambo ya kale kutokana na utaalamu wake mkubwa. Mwaka 2006 sensa ya tatu ya kutafuta mabaki ya kale ilianza, kutokana na mwaliko Bw. Yu Xiaoxing alishiriki kwenye shughuli za sensa hiyo katika mji wa Zhengzhou, kwani maisha yake hayawezi kuachana na kazi ya mambo ya kale, ana matumaini kuwa vijana wataweza kukamilisha utafiti wa mabaki ya kale ya mji wa Zhengzhou, mji ambao ulikuwa ni mji mkuu wa Enzi ya Shang toka mwaka 1600 K.K. hadi mwaka 1046 K.K. Anasema,

    "Kwa kuwa mwanasayansi wa mambo ya kale nimejitosa katika shughuli za mabaki ya kale kwa miaka 50 hivi, nikiwa pamoja na wenzangu tumegundua mabaki mengi na kuthibitisha kuwa mji wa Zhengzhou ulikuwa mji mkuu wa kwanza katika Enzi ya Shang. Sasa nimestaafu, ni matumaini yangu kuwa vijana wataendelea kujitahidi kugundua na kutafiti kuhusu mji huo. Naamini kwamba watakuwa na ugunduzi mkubwa zaidi."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako