• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0413

    (GMT+08:00) 2010-04-13 16:26:53

    Kwanza tunapenda kuwaletea ripoti tuliyotumiwa na waandishi wetu wa habari walioko Nairobi Kenya kuhusu maoni ya wasikilizaji juu ya vipindi vya Kiswahili vya CRI .

    Msikilizaji wtu Johnstone Ambale anapongeza Radio China Kimataifa kwa vipindi murua vya Kiswahili. Anasema vipindi hivyo vilionyesha kimasomaso juhudi zinazofanywa na wahusika kuhakikisha kuwa lugha hiyo inapewa umuhimu mkubwa nchini Kenya. Radio Chini kazi yenu yapendeza.

    Chacha Rioba Kimwama kutoka Kahawa barracks anapongeza Radio China Kimataifa kwa kutufanya sisi wakenya kuelewa tunachofaa kufanya ili tuboreshe Kiswahili. Napenda jinsi chuo kikuu cha Moi cha Kenya kinavyofanya kuhakikisha kuwa jamii inakienzi Kiswahili. Vyuo vingine vinafaa kuiga. Hongera radio China.

    Omurunga Alwanga kutoka Makongeni Nairobi anaanza kwa kupongeza Radio China Kimataifa kwa kazi safi. Anasema vipindi vya lugha ya Kiswahili vilimfanya aanze kujifikiria yeye mwenyewe iwapo anajiendeleza kwa misamiati au la.Napenda maoni ya mwalimu wa Chuo cha Moi kuwa jamii inafaa kuhusishwa kila mara panapotokea majina mapya ya Kiswahili.

    Councellor Mkukhanga kutoka Khayega, magharibi mwa Kenya anasema heko Radio China Kimataifa kwa vipindi vya kuelimisha. Ninyi ndio pekee mnaotuelimisha ukilinganisha na vituo vingine vya habari. Kwa kweli vipindi vya Kiswahili vilinipa motisha kwa kuzidi kufanyia utafiti lugha ya Kiswahili. Endeleeni na moyo huo huo.

    Mhadhiri Timothy Arege wa Idara ya Kiswahili katika chuo kikuu cha Catholic Nairobi anasema naivulia kofia Radio China Kimataifa kwa kukumbusha wana-afrika mashariki umuhimu wa kujivunia lugha ya Kiswahili.Vyombo vingine vya habari vinafaa kuiga mfano huo. Hongera watangazaji wa Radio China Kimataifa na iwapo mnataka ufafanuzi wa lugha niko tayari kufanya hivyo. Ndio maana nimeapa kuendelea kuwa shabiki sugu wa Radio China Kimataifa.

    Mwanafunzi Mwaniki kutoka Namangan anasema kweli vipindi vya Kiswahili vimenisaidia kuelewa umuhimu wa lugha hiyo maishani. Nilifurahia haswa pale mwandishi alipomnukuu mhadhiri mmoja akisema wanashawishi serikali itumie lugha hiyo kwenye mahojiano ya kikazi. Hiyo ni hatua ambayo imenifanya kama mwanafunzi nitakapomaliza masomo ya sekondari nisomee shahada ya lugha ya Kiswahili. Tuko pamoja na Radio China Kimataifa.

    David Gibuka Paul kutoka Isebania anasema heko Radio China Kimataifa kwa vipindi vya Kiswahili vilivyosisimua. Nilidhani Kiswahili kinadidimia hapa Kenya lakini kumbe nilikuwa nakosea .Natoa shukrani zangu kwa wakereketwa wa lugha nchini Kenya kwa jitihada zao kuhakikisha kuwa Kiswahili kinaenziwa nchini Kenya. Pia naomba washirikiane na wenzao kutoka Tanzania ili tupate maneno mapya ambayo yamepitishwa na kamati kuu.

    Ibrahim Oruko anaanza kwa kusema yeye ni mwandishi wa habari kwa lugha ya kiingereza nchini Kenya na hivi sasa anaendelea kuboresha Kiswahili chake. Hii ni kutokana na kutaka kuanza kuripoti habari kwa lugha ya Kiswahili. Nilipendezwa na jinsi wakereketwa wa lugha hiyo walivyopendekeza yanayofaa kutekelezwa na serikali na jamii kwa jumla ili lugha hii ienee vyema. Nilishanga kusikia Kiswahili hivi sasa kimepenya hadi nchini Libya. Hongara kwa kazi njema Radio China Kimataifa.Radio China Kimataifa hoyee!

    Ahmed kutoka Malindi Kenya anasema yeye akiwa mtu wa pwani anajivunia sana lugha ya Kiswahili. Anaongeza kuwa iwapo lugha hiyo itaenea jinsi wakereketwa wanavyosema basi huenda akatafuta kazi ya kufunza katika nchi hizo. Sikuamini nilipomsikia mhadhiri akisema lugha ya Kiswahili inazungumzwa hadi katika nchi ya Msumbiji. Iwapo ni kweli basi hiyo ni hatua kubwa. Haata hivyo hongera Radio China Kimataifa kwa vipindi vya kuelimisha.

    Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu wa Nairobi Kenya kwa maoni yao kuhusu matangazo ya Kiswahili ya CRI. Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kusikilizaji vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo ili tuviandae vizuri zaidi.

    Msikilizaji wetu Jim Godfrey Mwanyama wa S.L.P 1097 Wundayi Kenya, anasema pokeeni wingi wa salamu kutoka kwangu, marafiki, na wote tunaoshirikiana kusikiliza idhaa hii, kwa kweli idhaa hii ni nambari moja kwa matangazo yake motomoto. Mwisho nawatakia kheri na mafanikio katika mwaka huu.

    Na sasa ni zamu ya msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa S.L.P 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ambaye ametuletea barua akisema nina furaha kubwa kuandika barua hii ili kutoa shukurani nyingi kwa watumishi wote wa Redio China Kimataifa katika idhaa na idara mbalimbali tofauti zikiwa na malengo ya pamoja kutuhudumia sisi wasikiklizaji wote wa CRI, kutoka kila pembe ya dunia. Aidha natoa shukurani na pongezi maalumu kwa mkuu wa Redio China Kimataifa kutokana na salamu zake za mwaka mpya alizotoa tarehe mosi Januari mwaka huu wa 2010. Hotuba hiyo ya mkuu wa CRI kwa watumishi na wasikilizaji wake wote ilikuwa ni nzuri na ya kusisimua sana ambapo ilisheheni maudhui yenye kujenga imani na matarajio mazuri kwetu, sisi wasikilizaji wa idhaa mbalimbali za lugha 59 tofauti zinazotangazwa na Redio China Kimataifa ikiwemo lugha tukufu ya Kiswahili.

    Redio China Kimataifa ni chombo kikubwa zaidi cha upashanaji habari duniani kilichopo nchini China chenye malengo muafaka na mipango endelevu ya kutuelimisha, kutuhabarisha na kutuburudisha kwa ukamilifu sisi wasikilizaji wake kwa kiwango cha juu sana. CRI ni chombo madhubuti cha habari za kuaminika na ubora unaokidhi matakwa ya wasikilizaji wake.

    CRI imetushirikisha sisi wasikilizaji wake kwa njia mbalimbali, ikiwemo mashindano ya ujuzi ya chemsha bongo kuhusu matukio muhimu na vivutio vingi vya utalii katika mikoa kadhaa ya China takriban kila mwaka. CRI kutokana na shughuli zake za uhakika imejijengea sifa njema, heshima maridhawa na umaarufu mkubwa siyo tu barani Asia, lakini pia barani Afrika na dunia nzima.

    Zaidi ya hayo CRI imekuwa daraja kubwa ambalo linawaunganisha watu wa China na wa nchi na mataifa mengine duniani, inafanyakazi njema muhimu na ya maana kubwa sana hata kupelekea uhusiano na maingiliano ya kiuchumi na kiutamaduni baina ya wananchi wa China na jamii nyingine kote ulimwenguni. Nikiwa msikilizaji wa CRI na rafiki wa China kutoka Afrika nitaendelea kuwa msikilziaji muaminifu wa CRI, bila kusita katika mwaka huu na karne hii Mwenyezi Mungu atakavyoniongoza, kunilinda na kunijaalia .

    Ninapotamatisha barua yangu hii ninawasalimu sana wafanyakazi wote wa CRI na wananchi wote wa China wakiwemo ndugu zenu wa Taiwan, Macao na HongKong nikiwatakia furaha, amani, umoja na mshikamano katika kuijenga nchi yenu tukufu ya China.

    Ahsanteni sana pia karibuni sana Afrika, hususan Afrika Mashariki ambako watu wake wamejaa ukarimu na upendo na vilevile zipo fursa na vivutio vingi vya utalii nchini Tanzania bara na visiwani, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, na mambo mengine mengi katika eneo hili la maziwa makuu, wakiwemo wanawake na wasichana warembo wa kiafrika kama ilivyo kwa wasichana na wanawake warembo wa kichina katika makabila mbalimbali nchini China ambapo ni hazina kubwa.

    Tuwashukuru sana wasikilizaji Jim Godfrey na Bw. Kilulu Kulwa kwa maoni yenu maridhawa kabisa kuhusu kazi zetu za kuhabarisha, kuburudisha, kuelimisha n.k, na kwa niaba ya mkurugenzi wa CRI na watumishi wengine wote tunamwabia Bw. Kilulu Kulwa kuwa tunapokea pongezi alizotoa, aidha tunafurahishwa sana na maelezo na maoni yako unayotoa kuhusu Redio China Kimataifa pamoja na China kwa ujumla, tunakusihi usisite kutuandikia zaidi. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako