• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hali ya wanafunzi wengi wenye umri mdogo kusoma katika nchi za nje yafuatiliwa nchini China

    (GMT+08:00) 2010-04-13 16:31:59

    Mwaka jana wanafunzi wapatao laki 2.3 wa China walikwenda nje kuendelea na masomo yao, idadi ambayo imeongezeka kwa asilimia 30, na kati ya wanafunzi hao wahitimu wa shule za sekondari walichukua asilimia kubwa. Hivi sasa kituo cha kutoa huduma kwa wanafunzi wanaosoma nje katika wizara ya elimu ya China kiliandaa maonesho ya 15 ya kimataifa kuhusu mambo ya elimu hapa Beijing. Vyuo vikuu karibu 500 kutoka nchi na sehemu 30 duniani vilishiriki kwenye maonesho hayo. Kwenye maonesho hayo, wanafunzi wengi wa sekondari ya juu pamoja na wazazi wao walitembelea mabanda mbalimbali ya vyuo vikuu, wakichunguza taarifa za masomo na kuchagua vyuo vikuu vinavyowafaa. Kijana Ma Zhiwei anayesoma mwaka wa kwanza wa sekondari ya juu alikuwa ni mmojawapo. Alisema:

    "napanga kufanya maandalizi kwa pande mbili, yaani kushiriki kwenye mtihani wa taifa wa kujiunga na vyuo vikuu au kwa ajili ya kusoma nchi za nje. Elimu ya nchini China inatoa shinikizo kubwa zaidi, na elimu ya nje ni kamili zaidi. Kwa hiyo huenda nitasoma masomo ya sayansi katika nchi kama Marekani, Canada au Singapore."

    Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shule ya sekondari ya chuo kikuu cha Umma cha China Bi Wang Xuan ameamua kusoma shahada ya kwanza katika nchi ya nje, na safari hii alikwenda kuwasiliana na Chuo kikuu alichochagua. Bi Wang Xuan alisema:

    "nimesoma shule ya sekondari na sekondari ya juu nchini China, kwa hiyo nataka kusoma chuo kikuu katika nchi za nje, nitaweza kuona mambo mengi zaidi. Napendelea kusoma katika vyuo vikuu vya Marekani, kwa kuwa vina shughuli nyingi baada ya masomo na vinatilia maanani mambo wanayopenda wanafunzi wakiwa nje ya darasa."

    Kwa mujibu wa takwimu husika, zamani wanafunzi wa shahada ya pili na ya udaktari walikuwa wanachukua asilimia kubwa ya idadi ya wanafunzi wa China wanaosoma nje, lakini katika miaka miwili iliyopita wanafunzi wa shahada ya kwanza na hasa wanafunzi wa sekondari ya juu wanaokwenda kusoma Marekani, Canada na Australia wameongezeka kidhahiri. Mshauri kuhusu mambo ya kusoma katika nchi za nje wa kampuni ya mambo ya elimu ya Jiahuashida ya Beijing Bi. Shi Nan alisema:

    "zamani asilimia 80 ya wanafunzi waliosoma nje walisomea shahada ya kwanza, lakini hivi sasa nusu ya wanafunzi hao wanakwenda nchi za nje kusoma sekondari ya juu, na wanafunzi kama hao wanaendelea kuongezeka."

    Imefahamika kuwa kuna sababu nyingi zinazosababisha hali hiyo. Kwanza ni shinikizo la mtihani wa taifa kama walivyotaja Ma Zhiwei na Wang Xuan. Hivi sasa kila mwaka wanafunzi wapatao milioni 10 wanashiriki kwenye mtihani wa taifa wa kujiunga na vyuo vikuu nchini China, wanafunzi wanaofaulu kwenye mtihani wanaweza kupata fursa ya kusoma katika vyuo vikuu maarufu. Pili wazazi wengi wanapenda kuwekeza katika elimu ya watoto wao. Hata kama wakishindwa kupata udhamini wa masomo, ada ya kusoma katika nchi za nje ya Yuan laki moja kwa mwaka pia si mzigo mkubwa kwa familia zenye hali nzuri kiuchumi. Aidha, kutokana na kuinuka kwa mtizamo wa watu kuhusu mambo ya elimu, kusoma katika nchi za nje si kama tu ni kwa ajili ya kupata shahada tu, bali pia vijana wanaweza kuongeza upeo wao na kuinua nguvu yao ya ushindani katika kipindi kizuri cha kujiendeleza katika maisha yao. Mzazi mmoja wa mwanafunzi alisema:

    "jamii ya hivi sasa inataka watu wawe na mtizamo wa kimataifa kuhusu mambo mbalimbali, naona elimu ya msingi waliyopata wanafunzi nchini China imetosha. Wanafunzi wataweza kusoma mambo mengi mapya na ujuzi wa kisasa zaidi katika nchi za nje."

    Mshauri wa kampuni ya elimu ya Jiahuashida ya Beijing Bi. Shi Nan alisema:

    "zamani baadhi ya watu waliona kuwa wanafunzi baada ya kuhitimu katika vyuo vikuu kwanza wanapaswa kupata ajira nchini China, halafu kama wakitaka kujiendeleza, wanaweza kusoma shahada ya pili katika nchi za nje. Lakini hivi sasa hali imebadilika, watu wanaona kuwa watoto wakienda nje mapema zaidi, wanaweza kuzoea vizuri zaidi utaratibu wa elimu wa nchi za nje, kama wakijifunza vizuri lugha za nje, pia itawasaidia kupata nafasi nzuri kwenye ushindani baada ya kurudi China."

    Ingawa wanafunzi wenye umri mdogo kusoma katika nchi za nje kuna manufaa dhahiri, lakini hatari yake pia haiwezi kupuuzwa. Mshauri wa mambo ya kusoma katika nchi za nje wa kampuni ya New Oriental ya Beijing Bw. Tian Wang alichukua mfano wa kuwapeleka watoto kusoma Marekani, akisema,

    "Nchini Marekani kuna mambo mengi yenye ushawishi. Kwa mfano, vitendo vya uhalifu vinatokea mara kwa mara nchini humo, na inapaswa kuzingatiwa kama akili za watoto zimepevuka au la. Kuna baadhi ya watoto wenye umri mdogo baada ya kupelekwa nchi za nje, hawakupata elimu nzuri, bali waliathiriwa na tabia mbaya. Kwa hiyo tunawashauri wazazi wa watoto wazingatie kwa makini kabla ya kuwapeleka watoto nje, wasifuate mkumbo."

    Mwaka jana shule binafsi na madarasa mengi ya mafunzo ya lugha ya vyuo vikuu zilifilisika, walioathiriwa vibaya zaidi ni wanafunzi wa sekondari wa China walisoma katika nchi za nje, hali ambayo imewapigia kengele ya hatari watu wa China. Kuhusu hali hiyo, mshauri Bi. Shi Nan alisema:

    "ni lazima wazazi wawe na mtizamo wazi na kuchagua chuo kikuu sahihi, wanaweza kufuatilia tovuti ya usimamizi wa vyuo vikuu vya nje iliyoanzishwa na wizara ya elimu ya China, yenye orodha ya vyuo vikuu vyote vya nje vinavyotambuliwa na serikali ya China."

    Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya elimu ya China, mwaka 2009 idadi ya wanafunzi waliorudi nchini baada ya kumaliza masomo katika nchi za nje ilikuwa laki 1.1, ambayo imeongezeka kwa asilimia 60 kuliko mwaka jana. Zaidi ya asilimia 80 kati yao ni wanafunzi waliojilipia ada ya masomo. Wanafunzi wengi hata walishindwa kupata ajira baada ya kurudi nchini China, hali ambayo ni tofauti kabisa na matarajio yao. Mshauri wa mambo ya kusoma katika nchi za nje Bi. Shi Nan anaona kuwa vijana walioamua kusoma katika nchi za nje wanapaswa kuchagua masomo kwa makini na kuweka mpango kamili wa ajira, ambayo itawasaidia kupata maendeleo kwa utulivu zaidi baada ya kuhitimu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako