• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Jumba la maonesho la Hispania

    (GMT+08:00) 2010-04-19 17:24:18


    Hispania ni nchi yenye uchangamfu na vivutio vingi, historia na sanaa za nchi hiyo vinawavutia sana watu. Mchezo wa kupambana na maksai, ngoma, gitaa na soka... vyote vinawafurahisha watu. Jambo la kufurahisha ni kuwa maonesho ya kimataifa ya Shanghai yatakayoanza baada ya siku chache zijazo yatawaletea watu fursa ya kuwa karibu na nchi hiyo.

    Jumba la maonesho la Hispania liko katika sehemu ya C kwenye eneo la maonesho ya kimataifa ya Shanghai, ni moja kati ya majumba makubwa kwenye maonesho hayo. Umbo la jumba la Hispania lina mtindo wa kisanaa kama mihenzirani iliyosukwa, limechanganya mtindo wa kale na wa kisasa. Kwenye sehemu ya nje, jengo hilo limefunikwa na vipande zaidi ya 8,500 vilivyosukwa vya mihenzirani ya rangi, ukitazama kutoka mbali inafanana na sehemu ya chini ya sketi ndefu ya Flamenco ya Hispania. Msanifu wa jumba la maonesho la Hispania Bi Benedetta Tagliabue alisema, wazo la usanifu huo linatokana na hali ya uchangamfu ya Hispania. Alisema"Tuliposanifu tulikusanya fikra nyingi za Hispania katika jengo hilo, Hispania ni nchi yenye hamasa na uchangamfu mkubwa, hivyo tulizingatia kuonesha hali ya uchangamfu ya nchi hii, watu wanapoingia katika jumba hili wataona vivutio vingi."

    Kwenye uzio wa jengo la Hispania, mihenzirani ya rangi mbalimbali inaonesha shairi la Kichina; ndani ya jumba la maonesho, mwanga wa jua unaingia kwa kupitia nafasi zilizopo kwenye mihenzirani. Watazamaji wataona kama wanatembea kwenye barabara za miji ya Hispania, na kuona historia na busara za watu wa nchi hiyo. Njia ya kutumia mihenzirani tu kuunganisha utamaduni wa mashariki na magharibi, busara na uvumbuzi huu hakika vitawapa watazamaji kumbukumbu nyingi nzuri. Balozi wa China nchini Hispania Bw Zhu Bangzhao, alipolitembelea jumba la maonesho la Hispania kwa mara ya kwanza, alisema "Umbo la jumba la Hispania ni kama kikapu kilichosukwa kwa mihenzirani, ninaona linapendeza na kunivutia sana. Nimefahamishwa kuwa walipofanya usanifu wa jengo waliingiza sanaa ya maandiko ya maneno ya Kichina na shairi, huu ni ushahidi wa kuimarishwa kwa mfululizo kwa maelewano na maingiliano ya nchi mbili."

    Katika maonesho ya kimataifa ya miaka yote iliyopita, maudhui ya maonesho ni kitu kinachozingatiwa zaidi na nchi washiriki katika majumba yao. Jumba la Hispania likifuata kauli-mbiu ya "Miji yetu kizazi baada ya kizazi", linaeleza mabadiliko ya miji ya Hispania kwa mitazamamo ya watu mbalimbali.

    Mwelekezaji maarufu wa upigaji filamu za sinema wa Hispania Bw Bigas Luna alikabidhiwa kazi ya kupanga maonesho ya sehemu ya kwanza inayoitwa "Kutoka maumbile hadi miji". Anafahamisha watu hali ya siku za kale nchini Hispania kwa kutumia njia ya kuonesha ukweli na mambo ya kubuni, anaeleza ufahamu wake kuhusu "chanzo", yaani mwanzo kabisa wa dunia. Atawaonesha watazamaji hali tofauti ya Hispania kwa kutumia teknolojia ya sauti na video. Bw Luna alisema, "Watu wataona ufanisi wa sanaa ya sauti na video mara tu baada ya kuingia kwenye maonesho. Sauti zote ni kama za kweli kabisa, watu wanaona wenyewe wako katika mazingira yale, hata sakafu inaweza kutetemeka. Kupita kwenye sehemu ya kwanza kunahitaji dakika 7, vitu vyake ni vya kuvutia sana."

    Sehemu ya pili ya jumba la maonesho la Hispania inaitwa "Kutoka miji ya wazazi wetu hadi miji ya sasa", sehemu hii inawaonesha historia ya zama za karibuni, kumbukumbu ya kipande hiki cha historia kinaoneshwa kwa sanaa ya mashairi, ambapo zitaelezwa aina muhimu za sanaa. Sehemu ya tatu ya maonesho inaitwa "Kutoka miji yetu ya sasa hadi miji ya vizazi vya baadaye", msanifu wa maonesho atawafahamisha mambo mengi watazamaji wanaotembelea jumba hilo mara ya kwanza kwa teknolojia ya sauti na video, ili kuonesha matarajio ya watu kuhusu maendeleo ya miji ya baadaye, sehemu hii maonesho ni yenye vivutio na ya kufurahisha.

    Katika kipindi cha maonesho ya kimataifa, watu wataona vyakula vingi vya jadi ya sehemu ya Mediterranean. Mpishi wa kutoka Hispania Bw Pedro Larumbe atapika chakula halisi cha Hispania kwa watazamaji. Bw Pedro Larumbe alisema "Watazamaji wote wataweza kupata nafasi ya kuonja chakula halisi cha Hispania, ikiwa ni pamoja na wali uliopikwa na chakula cha baharini, chapati ya viazi na vyakula vingine vyepesi."

    Sehemu nyingine ni maonesho ya nyimbo na ngoma. Michezo mbalimbali ya sanaa ya utamaduni pia ni vitu vinavyotiliwa mkazo kwenye maonesho ya nchi hiyo. Ili kuwawezesha watazamaji wa China waifahamu vizuri Hispania, kwa uchache kabisa jumba la Hispania linanuia kuonesha michezo ya sanaa mara moja kila mwezi kwenye maonesho ya kimataifa au kwenye majumba makubwa ya michezo ya Shanghai. Mbali na hayo, kuna kiwanja kimoja kidogo ndani ya jumba la maonesho la Hispania, litakalokuwa na shughuli mbalimbali za kiutamaduni kila siku katika kipindi cha maonesho ya kimataifa. Wakati ule jumba la maonesho la Hispania litaleta wasanii mashuhuri kutoka nchi yake kuonesha michezo ya opera, ngoma ya Flamenco na muziki wa Kilatin, ambapo watu wataweza kuona vivutio halisi vya Hispania.

    Mwakilishi mkuu wa serikali ya Hispania kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai Bi Taine alisema, ujenzi wa jumba la maonesho la Hispania unakaribia kumalizika, katika hatua ijayo watatekeleza kwa makini mpango uliowekwa ili kukamilisha maandalizi mbalimbali kwa wakati kwa kushirikiana na idara ya maonesho ya kimataifa ya Shanghai, ili watazamaji waweze kuona jumba la maonesho la Hispania linalopendeza sana katika kipindi cha maonesho ya kimataifa ya Shanghai.

    Balozi wa China nchini Hispania Bw Zhu Bangzhao alisema, maonesho ya kimataifa ya Shanghai yameipatia Hispania fursa nzuri kuonesha utamaduni wa aina nyingi pamoja na wazo zuri la uvumbuzi, jambo ambalo litaimarisha msingi wa utamaduni kwa ajili ya urafiki wa kudumu wa watu wa nchi hizi mbili. Alisema"Naona, maonesho ya kimataifa ya Shanghai yatatoa fursa kwa Hispania kuwaonesha watu wa China utamaduni wake wa aina mbalimbali, historia na maendeleo yake, hii itaongeza ufahamu wa watu wa China kuhusu Hispania, kuwaweka karibu zaidi watu wa nchi hizi mbili na kuimarisha msingi wa utamaduni kwa ajili ya kukuza uhusiano wa nchi mbili."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako