• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Jumba la Makumbusho la Historia ya Maandishi ya lugha ya Kichina

    (GMT+08:00) 2010-04-19 17:32:44

    Mwishoni mwa mwaka 2009 Jumba la Makumbusho la Historia ya Maneno ya Kichina lilizinduliwa rasmi huko Anyang mkoani Henan, ambao ni mji maarufu kwa kuwa chimbuko la maandishi ya asili kabisa ya Kichina yaliyoandikwa kwenye magamba ya kobe na mifupa. 

    Bibi Zhang Qian anayefanya kazi katika hospitali mjini Anyang juzi juzi alitembelea jumba hilo. Akiwa na hisia nyingi alisema, ingawa yeye ni Mchina na anatumia lugha ya Kichina kila siku, lakini hana ujuzi kuhusu historia ya maandishi ya lugha ya Kichina, jumba hilo linamwezesha kufahamu kwa kina lugha ya taifa lake na maandishi yake. Anasema,

    "Kabla ya kuzuru jumba hili, nilikuwa sifahamu maandishi ya lugha ya Kichina ninayotumia sasa yalikuwaje, ila tu naona baadhi ya maneno yanaandikwa tofauti katika mitindo tofauti, sikufikiri zaidi ni nini sababu za tofauti hizo. Baada ya kutembelea makumbusho hayo kwa kuangalia maandiko ya awali yalivyooneshwa na kufahamishwa na mwelezaji, nimeelewa mchakato wa mabadiliko ya maandishi hayo."

    Inasemekana kwamba katika miaka zaidi ya elfu tano iliyopita ofisa Cang Xie wa enzi ya Huangdi alivumbua maneno ya kuandikwa ya Kichina badala ya kukumbuka mambo kwa kufunga mafundo ya kamba kabla ya hapo. Baada ya mabadiliko ya miaka elfu kadhaa, hivi leo maneno ya kuandikwa ya Kichina yamekuwa moja na maandishi yanayotumika zaidi duniani. Maandishi hayo licha ya kuwa yamerekodi historia ndefu na utamaduni mkubwa wa China, bali pia yamekuwa alama ya utamaduni wa China inayovutia watu wengi. Hiyo ni moja ya sababu ya kuzinduliwa kwa jumba hili la makumbusho.

    Mkurugenzi wa jumba hilo Bibi Hu Yanyan alieleza kwamba usanifu wa jumba hili ulitokana na maandishi kwenye magamba ya kobe na mifupa na vyombo vya shaba nyeusi vya kale ili kuonesha mzizi wa utamaduni wa taifa la China." Alisema,

    "Jumba hili lina kimo cha mita 32, ghorofa nne juu ya ardhi na ghorofa moja chini ya ardhi. Sura ya jumba hilo inafanana na kasri la kale la enzi ya Shang iliyoanzia mwaka 1600 K.K. hadi mwaka 1046 K.K. ikionesha umuhimu wa enzi hiyo katika mchakato wa maendeleo ya utamaduni wa China."

    Jumba hilo limegawanyika katika kumbi tano na sehemu 15, vitu vya kale ndani ya jumba hilo vikiwa ni pamoja na maandishi yaliyoandikwa kwenye magamba ya kobe na mifupa, kwenye vyombo vya shaba nyeusi na maandishi yaliyoandikwa kwenye mabamba ya mianzi na vitambaa vya hariri, vitu vya kuonesha historia ya mchakato wa mabadiliko ya maandishi ya lugha ya Kichina na historia ya usanii wa kuandika Kichina, na maandishi ya lugha za makabila madogo madogo na yalivyostawi hivi leo. Mkurugenzi wa jumba hili Bibi Hu Yanyan alisema, kazi muhimu ya jumba hilo ni kueneza elimu kwa umma na hasa kwa vijana kuwafanya wajionee jinsi maandishi ya lugha ya Kichina yalivyokuwa na nguvu kubwa ya uhai, mshikamano wake na uwezo wake wa ushawishi. Anasema,

    "Kazi kubwa ya jumba hili ni kutoa elimu na kuieneza katika jamii. Ukumbi wa kwenye ghorofa ya pili unapendwa zaidi na wanafunzi, kwa sababu huko wanafunzi wanaweza kujionea mvuto wa maandishi ya lugha ya Kichina kwa kupitia kuandika wenyewe kwa kalamu au kuchonga kwa kisu, hivyo wanafunzi wanaunganisha elimu waliyopata darasani na vitu halisi vya utamaduni."

    Jumba hilo ambalo lilifunguliwa siku chache tu zilizopita, limekuwa kivutio kikubwa mjini Anyang, watazamaji wanamiminikia huko hata kufikia karibu elfu nne kwa siku. Bibi Zhang Qian akiwa mmoja wa wapenda maandishi ya lugha ya Kichina anachukulia kutembelea jumba hilo kama ni fursa adimu, alimwambia mwandishi wa habari akisema,

    "ukiangalia kwa nje jumba hilo linavutia, kwanza hili ni jumba la ngazi ya taifa kwa usanifu wake na ulinzi wake wa ndani, pili vitu vya utamaduni vilivyomo ndani ni vingi na vinatuwezesha sisi watu wa kawaida kufahamu kwa kina mchakato mzima wa mabadiliko ya maandishi ya lugha ya Kichina, na mwelezaji anatueleza kwa undani. Hili ni jumba la makumbusho ambalo halitakiwi kuwa na kiingilio kwa wote, watazamaji wanatakiwa kujulisha kabla ya kulitembelea jumba hilo, kila siku watu wanasimama kwenye misururu, ikionesha kuwa watu wengi wanataka kuelewa historia ya maandishi ya lugha ya Kichina toka mwanzo kabisa yalivyokuwa kwenye magamba ya kobe na mifupa."

    Inafahamika kwamba maonesho yanayofanyika sasa ni mradi wa kipindi cha kwanza, na mradi wa kipindi cha pili ambacho umekuwa mbioni kuandaa ni shughuli za maingiliano ya wataalamu na utafiti. Ili kulifanya jumba hilo liwe na hifadhi na maonesho ya vitu vya kale na utafiti kwa ujumla, jumba hilo limewaalika wataalamu wengi wawe washauri kupanua athari na kuhimiza maingiliano na utafiti.

    Mtaalamu wa isimu mwenye umri wa miaka 104 Zhou Youguang ni mjumbe wa kamati ya usimamizi wa shughuli za jumba hilo, anaona kwamba kujenga jumba hilo ambalo ni la pekee la kuonesha historia ya maandishi ya lugha ya Kichina lina umuhimu mkubwa katika kuimarisha utamaduni wa sasa wa China. Anasema,

    "Ni jambo la maana sana kuanzisha jumba hilo, ushirikiano wa kuanzisha jumba hilo la makumbusho ni mzuri kutoka kwa raia, wataalamu na serikali. Kuhusu utamaduni wa taifa tunatakiwa mambo mawili yazingatiwe, moja ni kurithi utamaduni wa jadi, na lingine ni kujifunza kutoka kwa utamaduni wa zama za hivi sasa, yote hayo mawili ni muhimu. Kuimarisha utamaduni wa China hakumaanishi kutilia mkazo utamaduni wa kale na kupuuza wa sasa, bali ni kuutumia utamaduni wa kale kuchangia utamaduni wa sasa, wala siyo kuufanya utamaduni wa kale uwe wa sasa. Hii ni kanuni ambayo lazima tuishikilie."

    Alilotetea Mzee Zhou Youguang la "kutukuza utamaduni wa kale bila kupuuza utamaduni wa leo" ni lengo linalofuatiliwa na jumba la historia ya maandishi ya lugha ya Kichina yaani kulifanya jumba hilo liwe kituo cha utafiti wa maandishi ya lugha ya Kichina na maingiliano ya kiutamaduni duniani, kurithi na kueneza maandishi ya lugha ya Kichina na kuhimiza maingiliano ya utamaduni kati ya China na nchi za nje.

    Katika miaka ya hivi karibuni "joto la lugha ya Kichina" na "joto la utamaduni wa China" limeufanya lugha ya Kichina na maandishi yake viwe vinafuatiliwa sana duniani. Kwa mujibu wa makadirio, mwaka 2010 watu watakaojifunza lugha ya Kichina katika nchi za nje watafikia milioni mia moja. Hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka 2009 kulikuwa na vyuo vya Confucius 282 na madarasa ya Confucius 241 katika nchi 87.

    Mkurugenzi wa kituo cha maingiliano ya utamaduni kati ya China na Brazil Bibi Simone de la Tour anaona kwamba pamoja na jumba la historia ya maandishi ya lugha ya Kichina, vyuo vya Confucius na vituo vingine vya utamaduni vya China katika nchi za nje vyote ni chanzo kwa watu wa nchi za nje kuifahamu historia na utamaduni wa China. Anasema,

    "Vituo hivyo ni muhimu sana, kwa mfano nchini Brazil ni watu wachache sana wanaoifahamu China na utamaduni wake, wengi hawajui Confucius ni nani, hawafahamu utamaduni mkubwa wa China, kwa hiyo kuna haja ya kueneza utamaduni huo ili watu wengi waifahamu China na kujifunza utamaduni wake. Hapa duniani hakuna utamaduni uliokamilika, kwa hiyo hali nzuri ya kiutamaduni hapa duniani ni kuwepo kwa tamaduni tofauti kwa pamoja na kusaidiana."

    Jumba hilo ni kama kamusi kubwa ya lugha na maneno ya Kichina. Siku hizi lugha ya Kichina na maandishi yake yanatiliwa maanani kuliko zamani, kwa hiyo kuanzishwa kwa jumba hilo ni hatua kubwa kwa ajili ya kueneza duniani utamaduni wa China na huku utamaduni, lugha ya Kichina na maandishi yake pia yatakuwa na mvuto wake katika maingiliano ya utamaduni kati ya China na nchi za nje.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako