• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wanakijiji wa Fengdu wapambana na ukame

    (GMT+08:00) 2010-04-22 14:47:50

    Kuanzia kipindi cha majira ya joto mwaka jana, sehemu tano za kusini magharibi mwa China zilikumbwa na maafa ya ukame ambayo hayakutokea hapo awali. Wilaya inayojiendesha ya makabila ya Wamiao na Wabuyi ya Qianxinan mkoani Guizhou ilikumbwa na ukame zaidi, kuanzia mwezi Agosti mwaka 2009 mvua haikunyesha kabisa. Aidha, katika kipindi hiki, hali ya hewa ya sehemu hiyo imekuwa ya joto zaidi kuliko miaka iliyopita, ambayo imesababisha hali mbaya ya ukame, na kuathiri vibaya uzalishaji wa kilimo.

    Lakini katika kijiji cha Fengdu cha Xingyi kwenye tarafa ya Qianxinan, hali ni tofauti kabisa. Wanakijiji wa Fengdu wana bahati nzuri, kwa kuwa mashamba mengi ya kijiji hicho yamekuwa ya kituo cha vielelezo vya uzalishaji wa kilimo cha kisasa mjini Xingyi, kwa hiyo miundo mbinu ya maji imekamilika zaidi kuliko vijiji vya jirani zake. Ingawa mwaka huu kuwa ukame, lakini wanavijiji hawakuacha kulima shamba hata moja. Bw. Liu Fanggui mwenye umri wa miaka 49 alikuwa anavuna viazi mashambani, alisema,

    "Katika miaka iliyopita niliweza kupata Yuan 1,000 kutokana na kuuza viazi, lakini mwaka huu niliuza viazi hivyo kwa Yuan 1,800 hivi. Tangu maafa ya ukame yatokee hadi sasa, tumevuta maji kwa mara tano kwa ajili ya umwagiliaji. Mwaka jana bei kubwa zaidi ya viazi ilikuwa Yuan 1.2 hadi 1.3 kwa kilo, lakini mwaka huu viliuzwa kwa Yuan 2.5, kama viliuzwa mijini, vinaweza kuuzwa kwa Yuan 2.6 hadi 2.8."

    Kutokana na ujenzi mzuri wa miundo mbinu ya maji, viazi vilivyopandwa na Lao Liu ni vikubwa, ambavyo vinaweza kuuzwa kwa bei kubwa. Nyumba ya bibi Chen Zhongcui ipo karibu na mashamba ya Lao Liu, na iko upande mwingine wa barabara. Lakini maji yanayotumiwa kumwagilia mashamba ya Chen Zhongcui si mazuri yakilinganishwa na ya Lao Liu yaliyoko kwenye kituo cha vielelezo vya uzalishaji wa kilimo cha kisasa, hivyo mavuno na sifa ya viazi vyake si mazuri kama ya viazi vya Lao Liu, na mapato ya kuuza viazi pia yalikuwa madogo. Alisema,

    "Mvua haikunyesha hivi karibuni, hivyo mavuno ya viazi yalipungua, na mapato pia yalipungua. Ingawa bei ya viazi imekuwa kubwa kuliko miaka iliyopita, lakini mavuno yake ni madogo. Katika miaka iliyopita, mashamba haya yaliweza kuvuna kilo 4,000 au 5,000 za viazi, lakini mwaka huu tulivuna kilo 1,500 tu za viazi. Aidha, mbegu za viazi zilikuwa ghali, Yuan 2 kwa kilo. Uzalishaji wa viazi ulipungua, tena viazi hivyo ni vidogo, hivyo haviwezi kuuzwa kwa bei nzuri."

    Bibi Li Changshu wa kijiji hicho pia alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

    "Katika miaka iliyopita tuliweza kupata Yuan 14,000 au 15,000 kwa kuuza mpunga na viazi, lakini mwaka huu mapato yetu yalikuwa nusu ya miaka iliyopita."

    Ili kupunguza hasara, wakulima wote wa kijiji cha Fengdu wanajitahidi kupanda mazao mengine ili wasipitwe na msimu wa kilimo. Kila mwezi Machi ni wakati wa kuvuna viazi na kupanda mboga, kwa hiyo familia za Lao Liu na bibi Chen Zhongcui zilikuwa na shughuli nyingi. Mama wa bibi Chen Zhongcui pia alikwenda shambani kumsaidia bibi Chen Zhongcui. Alisema kuwa walipanda nafaka kwanza, halafu walipanda viazi, baadaye walipanda mboga, hata hawathubutu kupumzika.

    Licha ya kupanda viazi, wanakijiji wengi wa huko pia walipanda ngano na mboga, lakini walishindwa kuvuna mazao hayo mawili. Ili kuhakikisha mboga na nafaka zinaweza kupandwa bila matatizo, baadhi ya wanakijiji wanaanza kuchimba kisima baada ya kupata ushauri wa wataalam. Familia ya bibi Li Changshu ilichimba kisima kimoja, na alilipa Yuan 5,000 yeye mwenyewe. Alisema,

    "Kisima huchimbwa kwenye mahali penye maji chini ya ardhi, la sivyo ni kazi bure, kwa hiyo kabla ya kuchimba inafaa kuomba ushauri kutoka kwa wataalamu wa kazi hiyo. Baada ya kuchimba kisima, ni rahisi kwetu kutumia maji."

    Bibi Li Changshu alisema kama wakichimba kisima kwa kufuata utaratibu, na kikipitishwa kwenye ukaguzi, wanakijiji wanaweza kupata ruzuku za Yuan 1,000 kutoka serikali. Lakini anachotarajia zaidi ni kunyesha kwa mvua, ili wakulima waweze kupanda mazao ya chakula. Alisema kama haitanyesha mvua ya kutosha, wakulima wanaweza tu kupanda mahindi, na mvua ya kutosha ikinyesha, wanaweza kupanda mipunga vilevile.

    Bibi Li Changshu pia alifuatilia mambo kuhusu ruzuku zinazotolewa na serikali, kwa kuwa Yuan 5,000 si pesa chache. Ofisa wa kijiji cha Fengdu Bw. Peng Zuoshu alisema,

    "Ni lazima kuendelea na uzalishaji wa mazao ya kilimo, pia ni lazima kupunguza hasara inayotokana na ukame. Hivi sasa tunawahamasisha wanakijiji wachimbe visima ili kupunguza hasara na kuendelea na uzalishaji. Gharama ya kuchimba kisima kwanza inalipwa na wanakijiji wenyewe, baadaye serikali ya mji wetu itatoa ruzuku ya Yuan 1,000 kwa kila kisima, ili kuwasaidia kufanya vizuri uzalishaji."

    Hivi sasa hali ya ukame ya kijiji cha Fengdu pia imefuatiliwa na serikali ya huko, na serikali iliwatuma maofisa wa serikali kwenda huko kushughulikia kazi ya kupambana na ukame. Naibu meya wa mji wa Xingyi Bw. Liao Fugang alisema,

    "Hivi sasa mji huo unakuza uzalishaji ili kupambana na ukame. Kazi hiyo ni pamoja na kupanda aina za mboga zinazoiva haraka, ili kuhakikisha utoaji wa mboga sokoni; na kuandaa kazi ya kupanda mbegu katika majira ya Spring, ili kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya kilimo wa mwaka kesho hauathiriwi. Wakati huohuo, tutakamilisha miundo mbinu ya maji."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako