• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji

    (GMT+08:00) 2010-04-27 19:44:36

    Msikilizaji wetu Geoffrey Wandera Namachi wa Eveready security Guard S.L.P 57333 Nairobi Kenya, ametuandikia barua akisema mwezi mei mwaka huu wa 2010 ni mwezi unaosubiriwa kwa hamu kubwa kwani mji wa Shanghai unatarajiwa kuandika historia ya kupokea wageni wengi wakiwemo wageni mashuhuri kutoka ndani na nje ya China.

    Shanghai ni mji ambao umepewa fursa au jukumu la kuandaa maonesho ya kimataifa ya mwaka huu wa 2010, kulingana na habari ama taarifa ambazo nimezikusanya, nchi 192 na mashirika 50 ya kimataifa yatashiriki kwenye maonesho hayo ya Shanghai. Kwa taarifa zaidi ni kuwa maonesho hayo yenye kauli mbiu ya miji bora na maisha bora, yatakuwa ni maonesho makubwa zaidi yatakayouwachia mji wa Shanghai historia kubwa. Si hayo tu bali maonesho hayo yatauwachia mji huo urithi muhimu.

    Shanghai ni eneo lililo na historia ya kipekee, ingawa Shanghai ni mji mwenyeji wa maandilizi, lakini miji mingine pia huenda ikatembelewa na wageni, miji hiyo ni kama vile Nanchang, Guangzhou, Chengdu, Nanjing, Lanzhou na mingineyo. Hii ni fursa nzuri kwa nchi za Afrika kushiriki kwenye maonesho hayo, ili wapate kujifunza mambo mengi muhimu kutoka kwa China.

    Afrika ni bara ambalo lina kila aina ya rasilimali, lakini upungufu wa Afrika ni teknolojia ya uvumbuzi na kujiendeleza, hata hivyo China ni nchi mwenyeji wa maonesho hayo ambapo ina fursa nzuri ya kuonesha maendeleo yake ya toka enzi za zamani. Mwisho tukutane Shanghai.

    Shukrani nyingi msikilizaji wetu Geoffrey Wandera Namachi kwa maoni yako murua kabisa kuhusu maonesho ya kimataifa ya Shanghai ni kweli kabisa hivi sasa maonesho hayo yanasubiriwa kwa hamu kubwa sana ambapo zimesalia siku chache tu yafunguliwe. Maonesho haya ni makubwa kufanyika nchini China hivyo kama ulivyosema yataacha urithi mkubwa sana pamoja na kumbukumbu kubwa nchini China.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Ali Khamis Kimani wa S.L.P 169-40602 Ndori Kenya, yeye anasema nachukua fursa hii kuwasalimu na nategemea kwamba mnaendelea kuchapa kazi vilivyo. Dhumuni la barua hii ni kutaka kukujulisheni kuwa ninaendelea kuwapata kwa njia nzuri kabisa ingawaje mara kwa mara huwa ni usiku saa nne, wakati ambao ninakuwa nimechoka hoi bin taabani.

    Aidha nimepokea kadi za salamu, bahasha zilizolipwa na hivi karibuni kalenda ya mwaka huu wa 2010. hata hivyo katika siku za karibuni mliweza kunitupa kapuni kwani imechikua siku nyingi kusikia barua na hata kadi za salamu zikisomwa, jambo hili lilinitia tumbo joto nisijue la kufanya kutokana na mapenzi yangu kwa Redio China Kimataifa. Mwisho ningependa kujua ni lini washindi wa chemsha bongo kuhusu miaka 45 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania watatangazwa. Mliniomba anuani yangu ya posta ili mnitumie zawadi, nauliza je bado, mpaka lini? Ahsanteni.

    Ahsante sana Bw Ali Khamis Kimani kwa barua yako na tunapenda kukutoa hofu kuwa hatujakusahau wala kukutupa kapuni, na usiwe na wasiwasi, tarehe ya kutoa zawadi kwa washindi wa chemsha bong kuhusu maadhimisho ya miaka 45 tanga China na Tanzania zianzishe uhusiano wa kibalozi itaamuliwa hivi karibuni, kutokana na mpango wa ziara ya watu wetu wanaohusika, tunadhani siku hiyo haitachelewa sana katika miezi miwili ya hivi karibuni. Tunaomba wasikilizaji wetu watuelewe, kwani kazi husika ya maandalizi siyo rahisi kufanyika kwa muda mfupi.

    Msikilizaji wetu Albert Misian wa S.L.P 1246 Kisii Kenya anasema mimi ningependa kutoa shukurani kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kishwahili ya Redio China Kimataifa kwa kazi mliyofanya mwaka uliopita wa 2009 na ni shukrani kubwa sana na Mungu awabariki muendelee hivyohivyo mwaka huu wa 2010, vilevile sitasahau kwamba vipindi vyenu na matangazo tunavipokea kwa njia iliyo safi kabisa hapa Kisii Kenya, tunaomba tu mje kututembelea mje muone vile sisi tunavyoishi na mjifunze utamaduni wetu pia muweze kuona jinsi Kisii ilivyo na milima na mabonde na vitu vyote vya kuvutia na kupendeza. Ahsanteni sana.

    Na sasa ni zamu ya bwana Kilulu Kulwa wa S.L.P 161 Bariadi Shinyanga Tanzania yeye ametuletea barua akisema nimekuwa nikisikiliza na kufuatilia mara kwa mara vipindi vyenu, sisi wasikilizaji tunafurahi tunaposikia mnakaribisha wageni mbalimbali kutoka Afrika na kufanya mazungumzo nao, na hivyo kutupatia ufahamu na utambuzi kuhusu mawazo mazuri ya viongozi wetu kwaajili ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano baina ya China na nchi zetu za Afrika, ikiwemo Tanzania.

    Katika kipindi cha daraja la urafiki kati ya China na Afrika cha tarehe 18 mwezi wa 12 mwaka 2009, mlituletea mahojiano baina ya mwandishi wa habari wa idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa na makamu mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Mapinduzi kwa upande wa Tanzania bara Bw. Pius Msekwa ambapo alikuwa ameitembelea China akiwa mgeni rasmi wa chama. Ni dhahiri kwamba mzee Pius Msekwa alieleza vizuri katika mahojiano hayo na tulifurahi sana kutokana na maelezo yake yaliyothibitisha kwamba uhusiano kati China na Tanzania utaendelea kuwa imara pasi na shaka yoyote.

    Kuhusu utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa au tabia nchi alizungumzia mikakati ya Tanzania kama taifa, inavyojitahidi kupanda miti kama njia endelevu ya kuhifadhi mazingira na pia alizungumzia lengo la maisha bora kwa kila mtanzania na kuwa na dhamira njema ni hatua kubwa sana ya kuelekea kwenye mafanikio ya kweli. Mimi naamini kwamba, kuwa na wazo au fikra kwamba lazima watanzania wote wawe na maisha bora ni mchakato mzuri na muhimu sana unaoweza kuzaa nguvu chanya na muafaka itakayotupeleka kwenye neema na mafanikio hayo.

    Tunamshukuru sana mzee wetu Pius Msekwa ambaye kwa kweli ni hazina na chemchem ya hekima na busara kwa mustakabali wa siasa za taifa letu la Tanzania. Kutokana na umahiri na uzoefu wake ambapo amelitumikia taifa kwa nyadhifa mbalimbali kwa muda mrefu sana hadi sasa akiwa ni makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi taifa. Ni matarajio yetu kwamba Redio China Kimataifa itaendelea kutembelewa na wageni kutoka pembe zote za dunia wakiwemo viongozi mbalimbali waandamizi, wakuu wa nchi, viongozi mashuhuri na hata wanadiplomasia, na hasa mwaka huu ambapo wageni wengi wataitembelea China wakati wa maonesho ya kimataifa ya Shanghai. Kwasababu hii tunategemea kusikia mengi kutoka Shanghai na kote nchini China kupitia CRI. Ahsanteni sana.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Albert Misian kwa barua yako na Bwana Kilulu Kulwa kwa maoni yako kuhusina na ziara ya makamu mwenyekiti wa taifa kwa upande wa Tanzania bara Bwana Pius Msekwa,na kama alivyosisitiza Bwana Pius Msekwa nasi pia tunasema kuwa ni wajibu wa kila mtu duniani kuhakikisha kuwa mazingira yanapewa kipaumbele katika utunzaji pia tunapenda kukuomba tu endelee kutuandikia maoni, ushauri na hata kama una dukuduku kuhusu matangazo yetu. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako