• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kutembelea mlima Qixia katika majira ya Mchipuko

    (GMT+08:00) 2010-05-03 19:55:50

    Katika mji wa Nanjing mkoani Jiangsu kuna msemo mmoja unaosema "wakati mzuri kabisa kutembelea mlima Niushou ni majira ya Mchipuko, na wakati mzuri kabisa wa kutembelea mlima Qixia ni majira ya mpukutiko". Mwishoni mwa majira ya mpukutiko wa majani miti ya maple hubadilika kuwa ya rangi nyekundu kali, mlima Qixia una miti mingi sana ya maple, hivyo katika wakati huo karibu sehemu yote ya mlima Qixia inakuwa nyekundu, mandhari hiyo nzuri inaufanya mlima Qixia ujulikane sana nchini China.

    Lakini usije ukafikiri kuwa wakati mzuri pekee wa kutembelea mlima Qixia ni katika majira ya mpukutiko wa majani, hata ukitembelea mlima huo katika majira ya Mchipuko pia utafurahi sana. Watu wanaotembelea mlima Qixia katika majira ya Mchipuko mara kwa mara wanashangazwa sana wanapoona majani mekundu ya maple.

    Mara tu baada ya kuingia kwenye bustani ya mlima Qixia, unaweza kuona kwa mbali miti michache maple yenye majani mengi mekundu. Lakini ukienda mbele zaidi kwa kufuata njia ya kuingia mlimani, mandhari ya mlimani inabadilika na kuwa ya rangi ya kijani. Baada ya kwenda mbele zaidi kwa mita 100 au 200 hivi, kwenye sehemu njia inapopinda, utaona msitu mkubwa wa miti ya maple yenye majani mekundu, kivutio hiki kinaitwa "Shuanghongyuan". Hali hii ya kushangaza inaweza kuonekana kwenye sehemu nyingi za mlima Qixia, na inawafurahisha sana watalii. Mtalii mmoja alisema:

    "Mandhari ya hivi sasa pia ni ya kupendeza, ni tofauti ya ile ya majani mekundu mlimani wakati wa majira ya mpukutiko, lakini ninaona furaha sana na ninaburudika. Kuna majani ya miti ya maple ya rangi nyekundu, ambayo ni mekundu hata katika majira ya Mchipuko, mandhari yake inalingana na ya majira ya mpukutiko."

    Majani ya mti wa maple ni ya rangi nyekundu iliyokolea tangu majani yanapochipua. Miti ya maple ya rangi nyekundu ilianza kuota kwenye mlima Qixia toka zamani. Miti hiyo ilianza kupandwa katika bustani ya mlima Qixia miaka zaidi ya kumi iliyopita. Majani ya maple nyekundu yanayochipua katika majira ya Mchipuko ni mapya, rangi yake ni mbichi na inapendeza zaidi. Mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi wa bustani ya mlima Qixia Bw Li Hong alisema, "Majani mekundu katika majira ya Mchipuko ni mazuri zaidi kuliko yale ya majira ya mpukutiko, iwe kwa rangi au kwa majani yenyewe. Kwa sababu majani yanapochipua yanakuwa kama mtoto mchanga, rangi yake ni nyekundu mbichi, tena majani yanakuwa hayajaharibika. Pengine baada ya kupita majira ya joto na mpukutiko majani au kuliwa na wadudu, ama yanaweza kuharibika kidogo, lakini majani ya sasa bado ni mazima na hayajaharibika hata kidogo."

    Wapendwa wasikilizaji, kama mnavutiwa na majani hayo mekundu, basi ni vizuri kutembelea sehemu ya mlima Qixia, na kuona mandhari tofauti ya majani ya maple nyekundu katika majira ya Mchipuko. Wakati mnapoangalia majani ya maple, myaangalie kutoka chini kuelekea jua, katika hali hiyo majani yanakuwa mekundu na yanapendeza zaidi. Mbali na miti ya maple nyekundu, kuna sehemu moja nyingine nzuri, kwenye mlima huu, ambayo ni hekalu la Qixia lililojengwa zaidi ya miaka 1,600 iliyopita. Hekalu hilo lilijengwa mwaka 483, na ni sehemu ya chimbuko la dhehebu la Sanlunzong la dini ya kibuddha. Hekalu hilo lilipanuliwa katika enzi ya Tang, na kuwa moja kati ya mahekalu manne maarufu ya dhehebu hilo. Kila mwaka katika mkesha wa sikukuu ya Mchipuko, wakazi wa mji wa Nanjing wanakwenda huko kugonga kengele kubwa na kuomba baraka katika mwaka mpya.

    Katika hekalu la Qixia kuna "hazina tatu", ambazo ni mnara wa kuwekea majivu ya maiti ya Buddha Sakyamuni, mtelemko wa mlima wa mawe wenye sanamu za Buddha elfu moja na jiwe la kumbukumbu la Mingzhengjun. Kila moja ya mabaki hayo ya utamaduni lina hadithi yake.

    Hazina inayochukua nafasi ya kwanza ni jiwe la kumbukumbu la Mingzhengjun, ambalo lilijengwa zaidi ya miaka 1,300 iliyopita. Inasemekana kuwa jiwe hili lilijengwa na mfalme Li Zhi wa enzi ya Tang na Malkia Wu Zhetian, ambaye ni malkia pekee mwanamke katika historia ya China, ili kutoa shukrani kwa mtawa mmoja wa hekalu la Qixia. Mtaalamu wa utafiti wa historia ya hekalu la Qixia Bw Zhao Jun alisema

    "Hili ni jiwe la kumbukumbu la enzi ya Tang lililohifadhiwa vizuri zaidi kwenye sehemu ya Nanjing, maneno ya kumbukumbu yenyewe yako 2,376, na yaliyoko kwenye jiwe hilo ni 13 tu yamepungua. Kwenye jiwe hilo kuna mistari mingi myeupe ya maua ya plum, watawa wa hekalu hili wanaliita jiwe la maua ya plum, ambalo ni moja kati ya mawe kumi ya ajabu ya Nanjing, mistari myeupe iliyoko kwenye jiwe hilo inatokana na kisukuku cha mayungiyungi ya baharini,kwenye jiwe hilo kuna visukuku vya viumbe na mimea zaidi ya elfu 20, kwa hiyo jiwe lenyewe lina thamani kubwa. Maneno mawili ya Qixia ni hati ya mkono iliyoandikwa na mfalme Li Zhi wa enzi ya Tang, kwa hiyo kibanda cha jiwe la kumbukumbu kinaitwa kibanda cha mfalme."

    Hivi sasa kibanda hicho kiko mbele ya lango la hekalu la Qixia, na kinahifadhiwa kwa uangalifu na watawa wa hekalu hilo. Hazina ya pili ni mnara ulijengwa kwa mbao na wenye msingi wa mawe wa kuwekea majivu ya maiti ya Budha mkuu Sakyamuni, ambao uliteketezwa katika vita, mnara huo wa sasa ulijengwa upya hapo baadaye. Hazina ya tatu ya hekalu la Qixia ni sanamu za Buddha elfu moja iliyoko kwenye mtelemko wa mlima, kaskazini mashariki mwa hekalu hilo, sanamu hizo za mawe ni za kipekee za dini ya kibuddha zilizoko Nanjing za kipindi cha Liuchao katika historia ya China. Sanamu kubwa na ndogo za mawe zote zilichongwa kwa kufuata mtelemko wa mlima na zinapendeza sana.

    Mbali na vivutio vilivyoelezwa hapo juu, mlima Qixia una vivutio vingine zaidi ya 30, ikiwa ni pamoja na michoro ya malaika wanaoruka angani, chemchemi ya paa mweupe na bonde la maua ya mipichi, hususan bustani ya mfalme Qian Long, inasemekana kuwa mfalme Qian Long alikaa kwenye sehemu ya Qixia mara 5 katika mara sita alizofanya matembezi katika sehemu ya kusini ya China, hivyo sehemu hii inaitwa bustani ya mfalme. Katika historia ya China, wafalme 19 waliwahi kutembelea mlima Qixia. Kivutio kikubwa kwenye mlima huu ni mahali alipoangalia mto mfalme wa kwanza wa enzi ya Qin.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako