• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0504

    (GMT+08:00) 2010-05-04 15:32:10

    Msikilizaji wetu Zuhura Khavere wa S.L.P 34-40602 Ndori Kenya ametuletea barua akisema pokeeni mkono wangu wa heri katika mwaka huu wa 2010, na hatuna budi kumshukuru Maulana kwa kutuvusha kutoka mwaka 2009 hadi 2010 salama salimini.

    Lengo la barua hii ni kuwajuza kuwa ninafurahia mawasiliano baina yetu, ingawa sijapata nafasi maalumu katika chemsha bongo yoyote ya kunifanya nije kuitembelea China hususan kwenye studio zenu, lakini nafurahia huduma zenu zote.

    Pia nashukuru kwa zawadi za kalenda ya mwaka 2010, kadi za salamu, bahasha zilizolipwa na picha za mabinti warembo kutoka makabila madogomadogo nchini China. Mimi nimeuanza mwaka huu kwa bahati nzuri natumai kuwa mtaendelea kuviboresha vipindi vyenu, hususan kipindi cha chemsha bongo, aidha zawadi zenu ziwe angalau na thamani kubwa. Ahsanteni

    Nasi tunakushuru sana Bi Zuhura Khavere kwa barua yako, sisi tunakuomba usichoke kushiriki kwenye chemsha bongo zetu tunazotayarisha kwani pengine siku moja utabahatika kupata nafasi ya mshindi maalum na kuweza kuja kuitembelea China.

    Na sasa ni barua ya Bwana Ramadhani Khamis wa S.L.P 14-40602, Ndori Kenya, anasema salamu nyingi kutoka kwangu, natumai mmeuanza mwaka huu vyema mbali na kuwa panda shuka za maisha haziishi.

    Napenda kuwajulisheni kuwa nawapata vyema kupitia redio na kwa njia hii ya barua. Naomba kutoa shukurani zangu kwenu kwa kunitumia kadi za salamu na bahasha iliyolipwa, sasa naomba kutumiwa kalenda ya mwaka huu na jarida lolote la ama China Today au China Pictoria.

    Kabla sijakamilisha barua yangu hii napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa serikali ya China kwa kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kupeleka msaada na usaidizi nchini Haiti, huu ndio utu na ujirani mwema hata kama ni wa mbali, shukurani pia ziwaendee wale wote waliotoa misaada huko Haiti.

    Ahsante sana Bwana Ramadhani Khamis kwa maoni yako ambayo yanaonesha jinsi gani unavyopendelea watu duniani waishi vizuri kwa kusikilizana na kusaidiana, kama ilivyofanya China kwa Haiti, na hii inaonesha jinsi China inavyojali sana nchi nyingine ziwe matajiri au masikini na kusaidiana wakati tunapofikwa na matatizo ndio urafiki mwema, waswahili wanasema urafiki unashinda undugu, na akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Ahsante.

    Msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi wa Eveready Security Guard S.L.P 57333 Nairobi Kenya, anasema ni vyema kuwa nimepata fursa nyingine ya kuwaandikia barua nikitumai kuwa CRI inaendelea vizuri kuchapa kazi na kusukuma mbele gurudumu la umoja na mawasiliano na vilevile kuendelea kuinua na kuinyanyua bendera ya urafiki halali. Huu ni mwaka wa 2010 ambapo sisi kama marafiki tena ni wasikilizaji wa CRI tunatarajia mambo mengi muhimu yatakayotuelimisha ama vipindi vitakavyotuchangamsha.

    Hivi sasa ulimwengu unakumbwa na mambo na mabadiliko mbalimbali pamoja na changamoto chungunzima ambazo zinatatiza mshikamano na usalama wa dunia nzima, ingawa CRI inatuhitaji sisi wasikilizaji na sisi pia tunaihitaji CRI ili kwa pamoja tuweze kusonga mbele hatua kwa hatua. Naamini kuwa mwaka huu CRI itaboresha matangazo yake ili kukidhi maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wake na nina imani kubwa na hilo.

    Mwisho naitakia CRI kila la heri pamoja na maonesho ya kimataifa ya Shanghai mafanikio mwanana kabisa.

    Tunakushuru sana msikilizaji wetu Geofrey Wandera Namachi kwa barua yako, Redio China Kimataifa kila siku inapenda kuwafurahisha wasikilizaji wake na ndio maana tunaandaa vipindi mbalimbali vya kuwavutia wasikilizaji hata hivyo tutaendelea na maandalizi hayo, hivyo msikilizaji wetu usiwe na wasiwasi kwa hilo. Ahsante.

    Na sasa ni barua kutoka kwa Philip Nga'ang'a Kiarie anayetunziwa barua zake na Kiarie Ndumbi wa S.L.P 601, Maragua Kenya, anasema naomba kuchukua fursa hii kutoa pongezi zangu kwa wafanyakazi wa Redio China Kimataifa kwa kuandaa shindano la chemsha bongo kuhusu vivutio vya utalii mkoani Sichuan ambalo limemalizika na baada ya uthibitishaji wasikilizaji 30 wa idhaa ya Kiswahili ya CRI walipata ushindi wa nafasi mbalimbali.

    Hata hivyo mimi kama msikilizaji mashuhuri nilishiriki kwenye shindano hilo na nilipata fursa nzuri ya kuwa mmoja wa washindi wa nafasi ya pili. Baadhi ya zawadi nilizopokea kwenye bahasha ni cheti, bahasha zilizolipwa, kadi za salamu na fulana.

    Lakini la kushangaza ni kwamba barua yangu ilipofika kwenye kituo cha posta nilitumiwa kadi ya kudai barua hiyo kwenye kituo hicho cha posta. La kusikitisha ni kwamba nilipoenda na kadi ile niliambiwa kuwa barua yangu imekaa kwenye kituo hicho cha posta kwa siku 12, ilinibidi nilipe shilingi 250 za Kenya, nilipojaribu kuuliza niliambiwa kuwa haikuwa barua bali ni kifurushi.

    Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kushauriana na wahusika ili siku zijazo lisitokee tena tatizo hilo, tafadhali muwe mnajumuisha nambari ya simu kwenye anuani yangu ambayo ni +254721942179. Nitazidi kushiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo na kutosheka pamoja na kufurahia ushindi wangu. Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa idumu milele.

    Kwanza tunakupa pole sana Bw. Philip Nga'ang'a Kiarie kwa usumbufu wote huo ulioupata, kuzungumza nao hao watu wa posta itakuwa vigumu kidogo kwa upande wetu ila tunakuahidi kuwa tutakapotuma mzigo wowote tutajitahidi kuweka nambari yako ya simu ili iwe rahisi kwao kukupata.

    Na msikilizaji wetu Nyongesa J. Amos wa S.L.P 3479 Kitale anasema mimi ni mzima ingawa nilishikwa na mtihani wangu wa taifa wa kidato cha nne ambao ulikuwa mgumu kidogo, naendelea na pilika pilika za maisha nisije kuyakumbuka yale ya nyuma.

    Jambo moja linalonikera ni hali ya hewa kubadilika ghafla, kwani huku kwetu kunanyesha mvua kubwa sana. Mimi nikiwa laazizi mkuu wa CRI naendelea kufurahia na kuridhishwa na hudunma zote za CRI, huduma hizo ndizo zinazonipa hamu na tamaa ya kutembelea nchi ya China siku moja. Kupitia picha nilizotumiwa kutoka huko China nimeweza kujua baadhi ya tamaduni na familia mbalimbali za China kwa mfano Zang Zu, Dong Zu, Yao Zu, Yi Zu na nyingine nyingi.

    Kwangu mimi huduma za CRI zina upekee unaoniridhisha kwa hiyo ni huduma zinazofaa tuzo ya sifa kubwa. Mwisho ningependa kuwatakieni heri na mafanikio ya mwaka mpya, na kwa wasikilizaji wote wa CRI ningependa kuwakumbusha tu kwamba Redio China Kimataifa ndio fimbo ya karibu, tusije tukajikita kwenye idhaa nyingine zozote, kwani fimbo ya mbali haiui nyoka.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Nyongesa J. Amos kwa maoni yako, sisi tunafurahi sana tukiona tunaridhisha wasikilizaji wetu, hivyo tunakuomba wewe na wasikilizaji wetu wengine wote muendelee kusikiliza matangazo yetu ambayo yanakuleteeni vipindi mbalimbali murua kabisa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako