Takwimu zilizotolewa tarehe 11 zinaonesha kuwa, mwezi Aprili kiwango cha bei ya bidhaa za matumizi kiliongezeka kwa asilimia 2.8 nchini China. Msemaji wa idara ya takwimu ya China Bw. Sheng Laiyun ametoa uchambuzi kuwa, hali hii inatokana na kupanda kwa bei ya chakula na nyumba, hata hivyo amekadiria kuwa, China itaweza kutimiza lengo la kudhibiti kiwango hicho kisizidi asilimia 3 mwaka huu.
Kwa mujibu wa takwimu mwezi Aprili kiwango cha bei ya bidhaa za matumizi nchini China kiliongezeka kwa asilimia 0.4 kuliko mwezi Machi. Bw. Sheng Laiyun amechambua sababu yake kuwa bei ya mboga ilipanda kwa kiasi kikubwa, akisema (sauti 1) "Ukame ulioikumba sehemu ya kusini magharibi na baridi iliyoathiri sehemu nyingi za China ni sababu kuu zilizoathiri mavuno ya mboga, kupanda kwa bei ya pembejeo kulisababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji na uchukuzi, hizo ndizo sababu za kupanda kwa bei ya mboga. Aidha uchumi wa China unaendelea kufufuka na mahitaji sokoni yanaongezeka, ndiyo maana ni hali ya kawaida kwa bei ya bidhaa kupanda kiasi."
Hivi sasa hatua za kuzuia mtiririko wa fedha duniani zimelegezwa na uchumi wa dunia unafufuka kwa ujumla, kwa hiyo bei ya bidhaa ghafi yakiwemo madini na mafuta imeanza kupanda, hali ambayo inalazimisha bei ya bidhaa za viwanda pia kwenye soko la China ipande. Takwimu zinaonesha kuwa, mwezi Aprili kiwango cha bei ya bidhaa za viwanda kiliongezeka kwa asilimia 0.9 kuliko mwezi Machi.
Msemaji huyo amekiri kuwa, hivi sasa China inakabiliwa na shinikizo kubwa la mfumuko wa bei, shinikizo ambalo linatokana na kupanda kwa bei ya bidhaa ghafi kwenye soko la kimataifa, mahitaji ya soko la China kuendelea kufufuka, na kiwango cha bei ya bidhaa nchini China kuendelea na mwelekeo wa kupanda tangu mwaka jana. Hata hivyo msemaji huyo amekadiria kuwa, mwaka huu inawezekana kutimiza lengo la kudhibiti kiwango hicho kisizidi asilimia 3. Amesema (sauti 2) "Serikali ya China katika ngazi mbalimbali inatilia maanani suala la bei ya bidhaa. Serikali za mikoa mingi zimechukua hatua, pia zinazingatia sana kuleta hali ya uwiano kati ya ongezeko la uchumi, marekebisho ya muundo wa uchumi na usimamizi wa mfumuko wa bei."
Takwimu hizo zilitolewa tarehe 11 pia zinaonesha kuwa, mwezi Aprili bei ya nyumba katika miji 70 mikubwa na ya ukubwa wa kati ilipanda kwa asilimia 12.8 kuliko mwaka jana kipindi kama hiki. Lakini bei ya nyumba bado haijawekwa kwenye takwimu za bei ya bidhaa za matumizi.
Benki kuu ya China kwenye ripoti iliyotoa hivi karibuni kuhusu sera ya sarafu katika robo ya kwanza ya mwaka huu, inasema itaendelea kusimamia hali ya mtiririko wa fedha na utoaji wa mikopo kwa kupitia sera ya sarafu, kuzuia bei ya nyumba isipande kwa kasi kupita kiasi na kuendelea kusimamia vizuri hali ya mfumuko wa bei.
Baadhi ya wataalamu wametoa maoni kuwa, kama kiwango cha kupanda kwa bei ya bidhaa za matumizi kitazidi asilimia 3 katikati ya mwaka huu, kuna uwezekano kuwa benki kuu ya China itaongeza kiwango cha riba na faida.
Msemaji wa idara ya takwimu ya China Bw. Sheng Laiyun ameeleza kuwa, bado kuna hali zisizo za uhakika nchini na nje ya China ambazo zitaweza kuathiri hali ya uchumi wa China. Ametoa ufafanuzi akisema, hivi sasa kumetokea dalili kuwa msukosuko wa madeni ya Ulaya unaweza kuenea zaidi, hali ambayo itaweza kuathiri usafirishaji nje bidhaa za China, na nchini China kwenye mchakato wa kufufua uchumi wake, ukuaji wa kasi wa viwanda unaleta shinikizo kubwa kwa kazi ya kupunguza matumizi ya nishati na uchafuzi na kazi ya kurekebisha muundo wa uchumi, na bei ya bidhaa itaweza kupanda zaidi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |