• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Michezo ya sanaa yachangia kuleta mvuto kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai

    (GMT+08:00) 2010-06-01 11:19:35

    Maonesho ya kimataifa yanaendelea huko Shanghai, mji wa mashariki mwa China. Kwenye eneo la maonesho hayo yanayowavutia walimwengu, mbali na majumba mbalimbali yenye maonesho ya aina tofauti, maonesho zaidi ya 100 ya michezo ya sanaa yanafanyika kila siku. Iwe mchana au usiku, watalii wanapotembea kwenye eneo hilo, wakichoka wanaweza kukaa na kuburudishwa na michezo ya sanaa inayooneshwa nje ya majumba, pia wanaweza kupata burudani kwa kuingia majumbani ambapo michezo ya ngoma inaweza kuoneshwa.

    Mliyosikia ni ngoma iliyochezwa kwenye eneo la maonesho ya kimataifa. Ngoma hiyo yenye jina la "farasi" ilichezwa na wasanii wa nchi tatu za China, Cananda na Mongolia, kwa kuambatana na muziki wa kimongolia wasanii hao wanaingiza jinsi farasi wanavyoishi mbugani. Michezo hiyo ya ngoma ilioneshwa kwenye jukwaa rahisi ambalo halijafungwa vifaa vya kisasa vya maonesho, hata hivyo watazamaji wanavutiwa sana. Babu na bibi wenye umri wa miaka 70 kutoka mkoa wa Jiangxi, China walitazama maonesho hayo yaliyofanyika kwa karibu saa moja. Bibi Wang Bingru alisema ni nadra kwao kutazama maonesho ya namna hii. "Naona haya ni maonesho mazuri ya michezo ya sanaa, navutiwa sana. Toka mwanzo hadi mwisho inaonesha hadithi nzima, naweza kujionea jinsi maisha ya mbugani yalivyo, ambapo farasi wanakimbia. Maisha ya mbugani yananivutia."

    Mwaka 2007 mkurugenzi wa kundi la Hongtian ambaye pia ni mwongoza Sandra Laronde alitembelea mkoa wa Mongolia ya ndani wa China, ambapo aliwachagua wachezaji watatu wa ngoma, ambao pamoja na waimbaji wengine watatu waliotoka Mongolia, walipelekwa nchini Canada kupata mafunzo. Ngoma hiyo "farasi" iliwahi kuchezwa mwaka 2008 kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing, hivi sasa inaoneshwa kwenye eneo la maonesho ya kimataifa ya Shanghai ili watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani waburudishwe kwa ngoma hiyo.

    Bibi Sandra alisema "Nafurahia kuonesha matarajio ya nchi hizo tatu kuhusu maisha ya siku zijazo, tamaduni za aina mbalimbali, na mandhari nzuri, pia kuonesha jinsi farasi wanavyopendeza na kuwa na nguvu. Farasi ni wanyama kwenye mazingira ya asili, na mbuga zipo nchini Canada, Mongolia na kwenye mkoa wa Mongolia ya ndani wa China, lakini eneo la mbuga linapungua, na idadi ya farasi pia inapungua. Farasi ni wanyama muhimu sana. Ngoma hiyo inaonesha hadithi ya farasi kuingia kwenye ndoto ya binadamu na kuwaelimisha watu umuhimu wa kuwaheshimu farasi. Napenda kuonesha tabia ya farasi ambao ni wanyama wanaowakilisha uzuri na nguvu."

    Wachezaji wa kundi la Hongtian wanatoka nchi tofauti na kutumia lugha tofauti, kwa hiyo wanawasiliana kwa ishara za mikono wanapofanya mazoezi. Mchezaji wa China Cai Hong alisema, kushindwa kuelewana kwa lugha kunawafanya wazingatie zaidi kucheza kwa moyo. Alisema "Hatujui kuongea lugha za wenzangu, lakini cha ajabu ni kwamba tunaweza kuelewana kwa mikono. Sijui ni kwa nini. Sandra aliwaalika walimu na waongozaji kadhaa kutufundisha. Tunashirikana vizuri tukionesha hadithi hiyo kwa miili yetu na kucheza kwa moyo."

    Tofauti na kundi la Hongtian ambalo linashiriki kwa mara ya kwanza kwenye maonesho ya kimataifa, wasanii kutoka Korea ya Kusini wana uzoefu wa kufanya maonesho kwenye maonesho ya kimataifa ya awamu kadhaa zilizopita. Mkurugenzi anayeshughulikia michezo ya sanaa kwenye jumba la Korea ya Kusini Bibi Shen Jiaxi alieleza kuwa, kwenye maonesho ya kimataifa yaliyofanyika mwaka 1986 mjini Vancouver, wasanii wa Korea ya Kusini walionesha michezo ya sanaa ya aina mbalimbali za nchi hiyo mbele ya watazamaji wa nchi za magharibi.

    Alisema "Tulifanya utafiti mwingi kusudi kubuni kazi tofauti na zile za China na Japan, hususan katika nguo na uvumbuzi wa kazi zetu. Tulitafuta mambo yanayofanana katika usanii wa nchi hizo tatu, lakini pia tunalenga kuonesha uzuri na mvuto maalumu vya Korea ya Kusini. Safari hii tumekuja Shanghai na michezo ya sanaa ya aina mbalimbali, zikiwemo ngoma za jadi, michezo ya kupiga ngoma kwa mtindo wa jadi, dansi ya barabarani, dansi ya Ballet mtindo wa Jazz, muziki wa elektroniki, na maonesho ya nguo za mtindo wa kifalme."

    Kwenye maonesho ya kimataifa, kila nchi inajitahidi kutangaza utamaduni wake unaowavutia zaidi watu, ama michezo yake ya sanaa ya kisasa au sanaa zake za jadi, michezo ya sanaa na maonesho moja moja yanalenga kuwaburudisha na kuwafurahisha watazamaji, na hivyo kuwaachia kumbukumbu. Kwenye jumba la Brunei, nchi ya kusini mashariki mwa Asia, msanii Haji Sabli alikuwa anapiga ala ya muziki ya jadi. Alisema "Hii ni ala ya muziki ya wenyeji wa Brunei, inafanana na gitaa katika nchi za magharibi. Michoro iliyochorwa kwenye ala hiyo ilitokana na taswira walizopata watu walioishi huko tangu zamani. Michoro hiyo inaashiria maana fulani fulani. Watu wa kale waliheshimu wanyama na ndege wa porini, kwa hiyo walichora vitu vilivyopo akilini mwao. Mimi nina bahati nzuri kwa kuweza kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa kwa niaba ya Brunei. Napenda walimwengu wapate ufahamu mwingi zaidi kuhusu nchi yangu kupitia maonesho haya ya kimataifa."

    Kama ukitembea kwenye eneo la maonesho ya kimataifa ya Shanghai, ni hali ya kawaida kuwakuta watu wengi wakicheza ngoma kwa pamoja, ama ngoma za Afrika, au ngoma ya jadi za Russia, au ngoma za mtindo wa Mexico, muziki unaposikika watalii wanashindwa kuzuia miili yao isicheze kwa kufuata midundo ya muziki.

    Bwana Jorden Reeves na mkewe wameishi mjini Shanghai kwa miaka miwili, walipata burudani nyingi wakati wa jioni kwenye eneo la maonesho ya kimataifa. Bwana Jorden alisema "Michezo ya sanaa iliyooneshwa leo jioni ni mizuri sana. Muziki na ngoma zina mambo mapya, tunazipenda. Hii ni jioni ya furaha kweli kwetu. Kama michezo mingine ya sanaa pia ingekuwa mizuri namna hii, mimi na mke wangu hata hatutaki kusubiri, tutakuja tena siku nyingine, tuna hamu ya kutazama maonesho mengine ya michezo ya sanaa."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako