• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Waandishi wa habari wadogo kwenye eneo la maonesho ya kimataifa ya Shanghai

    (GMT+08:00) 2010-06-10 14:21:00

    Msichana Yu Shiyao mwenye umri wa miaka 12 ni mwanafunzi wa darasa la 6, lakini hii ni mara yake ya kwanza kuja kwenye eneo la maonesho ya kimataifa ya Shanghai, lakini sio kwa ajili ya kutembelea kama walivyo watoto wengine, bali yeye ni mwandishi wa habari wa gazeti la watoto wa Shanghai. Chini ya uongozi wa walimu wao, msichana Yu Shiyao na wenzake walitumia lugha ya Kiingereza kuwahoji watalii wa kigeni kuhusu hisia zao za kutembelea maonesho ya kimataifa. Walitaka kutoa toleo maalum la gazeti kuhusu maonesho ya kimataifa, ili wasomaji watoto wa sehemu mbalimbali nchini China waweze kuona mvuto wa maonesho ya kimataifa ya Shanghai.

    "Chokoleti ya Ubelgiji ni maarufu duniani, kwa maoni yako kwa nini watu wanapenda chokoleti ya Ubelgiji?

    Naona kwa kuwa chokoleti nyeusi ya Ubelgiji ni nzuri kabisa duniani."

    Yu Shiyao aliyekuwa anakusanya habari katika jumba la maonesho la Ubelgiji, alifuatilia sana maoni ya watalii wageni kuhusu Ubelgiji, na kitu gani kitaletwa na maonesho ya Ubelgiji kwa China. Msichana huyo alisema "amefanya kazi" kwa miaka mitatu katika gazeti hilo, lakini mara nyingi alikusanya habari kwa lugha ya Kichina. Ili kukusanya habari kwa lugha ya Kiingereza kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai, yeye na wenzake waliandaa muhtasari wa mahojiano kwa Kiingereza na kufanya mazoezi mara kwa mara. Yu Shiyao ambaye ni mkuu wa kituo cha Puxi cha gazeti hilo aliona kuwa mahojiano hayo yana maana kubwa. Alisema,

    "Gazeti letu lina shule ya kufundisha mambo kuhusu habari, kuimarisha uwezo wetu, ili tuweze kuwahoji watu maarufu au kukusanya habari wakati wa shughuli kubwa. Kwenye maonesho ya kimataifa tunakusanya habari kwa lugha mbili, zamani tulitumia lugha ya Kichina tu, lakini sasa tunatumia Kichina na Kiingereza. Kabla ya kukusanya habari tuliandaa mada mbalimbali, halafu tunafuata mada hizo na kuwahoji wageni, kwa kufanya hivyo uwezo wetu wa kufanya kazi sisi wenyewe utaimarishwa."

    Kijana Sam Lynn alikuja mjini Shanghai kutoka London mwaka mmoja uliopita. Yeye ni mwalimu wa gazeti hili la watoto wa Shanghai. Bw. Sam alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa walianza maandalizi miezi miwili iliyopita, licha ya kuwafundisha watoto hao lugha ya Kiingereza, pia wanawafundisha kuandika habari. Aidha, ili kuambatana na kauli mbiu ya maonesho hayo "miji bora, maisha bora", Bw. Sam pia aliwasaidia waandishi wa habari hao watoto kuorodhesha masuala yanayohusu maendeleo ya miji, ili waweze kukusanya habari vizuri zaidi. Alisema,

    "Hii ni mara yetu ya kwanza kukusanya habari kwenye eneo la maonesho ya kimataifa, na lengo letu ni kukusanya habari kwa kutumia lugha ya Kiingereza kadiri tuwezavyo. Bila shaka kila mtu amechagua suala analofuatilia, kwa mfano, baadhi ya watoto wanafuatilia suala la uchafuzi wa mazingira, wengine wanafuatilia suala la maliasili ya maji, na pia kuna watoto ambao wanafuatilia majumba mbalimbali ya maonesho. Masuala hayo yote yanahusiana na kauli mbiu ya "miji bora, maisha bora", na watoto wanataka kufahamu namna ya kupunguza uchafuzi na kuboresha sifa ya maji, ili kuifanya miji iwe mizuri zaidi. Katika jumba la maonesho la Ubelgiji, suala tunalofuatilia ni kwamba Shanghai na Ubelgiji zinaweza kubadilishana uzoefu gani kuhusu ujenzi wa miji."

    Wasikilizaji wapendwa, labda hamfahamu sana gazeti hilo la watoto la China, lakini gazeti hilo linajulikana sana kwa vijana na watoto wengi wa China. Kazi za ukusanyaji habari, uhariri na uchapishaji wa gazeti hilo zote zinafanywa na watoto wenye umri wa chini ya miaka 15. Katika miaka zaidi ya 20 iliyopita baada ya gazeti hilo kuanzishwa, limetoa fursa nyingi kwa vijana na watoto wanaotaka kushughulikia kazi za habari, na limewaandaa waandishi wa habari wengi hodari.

    Mwandishi mdogo wa habari mwenye umri wa miaka 10 Tan Tian alisema, ingawa hakujiunga muda mrefu na gazeti hilo, lakini anapenda sana kuwasiliana na watu tofauti kupitia kukusanya habari. Alisema zamani alikuwa hathubutu kuongea na watu asiowajua, lakini siku hizi tabia hiyo imebadilika kidogo, na alitarajia kupata ujuzi mwingi zaidi kutokana na mazoezi ya ukusanyaji habari kwenye maonesho ya kimataifa. Alisema,

    "Kutokana na kuja hapa, naweza kupata ujuzi mwingi zaidi kuhusu maonesho ya kimataifa, pia naweza kuwahoji watu wengine. Niliwauliza watalii maswali kuhusu jumba la maonesho la Japan, kwa mfano niliwauliza kuwa wanaweza kujifunza mambo gani kwenye jumba la maonesho la Japan. Napenda kufanya mazoezi, ambayo pia yanaweza kunifanya nithubutu zaidi mbele ya watu, na kujifunza ujuzi mwingi zaidi."

    Mtalii kutoka Serbia Bw. Zoran Netkovic aliyeulizwa maswali na waandishi wadogo wa habari alisema, alifurahi sana kuhojiwa na watoto hao kwa lugha ya Kiingereza kwenye majumba ya maonesho. Aliona kuwa hatua hii sio tu inaweza kuimarisha uwezo wa vijana na watoto, bali pia itasaidia maendeleo katika nchi ya siku za mbele. Bw. Netkovic alisema,

    "Inapendeza, naona kuwa hatua hii itawanufaisha vijana na watoto hata maendeleo ya nchi, watoto wanaweza kuwahoji wageni kwa Kiingereza, na kufahamu mawazo ya wengine, hili kweli ni wazo zuri."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako