• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Watu wa Afrika wafanya juhudi ili maisha ya siku za mbele yawe mazuri zaidi

    (GMT+08:00) 2010-06-17 10:39:03

    Jumba la maonesho la pamoja la Afrika

    Tarehe 3 Juni ilikuwa ni siku ya heshima ya kamati ya Umoja wa Afrika. Kwenye eneo la maonesho ya kimataifa ya Shanghai, jumba la maonesho la pamoja la Afrika liliwaonesha watu Afrika halisi, na kuwawezesha wafahamu zaidi nchi za Afrika na maisha ya watu wa huko. Ingawa watu wa Afrika bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini pia wanafanya juhudi na kuamini kuwa maisha yao ya siku za mbele yatakuwa mazuri zaidi.

    Bara la Afrika labda ni geni kwa watu wengi, lakini baada ya kuingia kwenye jumba la maonesho la pamoja la Afrika, watu wanaweza kugundua kuwa, ndani ya jumba hilo, kila nchi ina umaalum wake. Kwa mfano jumba la maonesho la Mauritius linaonesha mandhari nzuri ya nchi hiyo ya visiwa, na kwa ujumla jumba hilo linaonekana kama ni bahari yenye rangi ya buluu. Kwenye maeneo mawili ya maonesho "visiwa vyenye mandhari nzuri" na "nyumba ya jadi", watu wanaweza kuona juhudi zinazofanywa na Mauritius ili kuhifadhi mabaki ya kihistoria na kuwepo kwa utamaduni mbalimbali. Aidha, kwenye jumba la maonesho la pamoja la Afrika kuna gulio la Afrika, ambapo watu wanaweza kuona na kununua bidhaa mbalimbali zenye umaalum wa Afrika, pia wanaweza kufahamu zaidi maisha ya watu wa Afrika.

    Msimamizi wa kampuni ya Senegal inayoshughulikia mambo ya hifadhi ya mazingira na uuzaji bidhaa kwa nje Bw. Serigne Aliou Diop alifahamisha kuwa, kama walivyo watu wa nchi nyingine, maisha ya watu wanaoishi katika miji ya nchi za Afrika pia yameathiriwa na msukosuko wa fedha duniani, lakini maisha yao bado ni ya gharama za chini. Bw. Diop alisema,

    "Kama zilivyo nchi nyingi za Afrika, Senegal pia imeathiriwa na msukosuko wa fedha duniani, ambao unaongeza gharama za maisha kwa watu wa Dakar. Lakini kwa ujumla sisi tunaishi maisha ya gharama za chini."

    Kama tujuavyo, sababu mbalimbali za kihistoria na kijiografia zinaifanya Afrika ikabiliwe na matatizo mengi, kama vile ukosefu wa maliasili ya maji na chakula. Lakini watu wa Afrika hawaachi matarajio yao kuhusu miji bora. Mwakilishi mkuu wa Umoja wa Afrika kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai Bw. Nadir Merah alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, ingawa bara la Afrika linakabiliwa na changamoto, lakini watu wa Afrika siku zote wanatarajia kuishi maisha mazuri zaidi. Alisema,

    "Tunajua kuwa Afrika inatafuta fursa ya kujiendeleza. Bila shaka tunakabiliwa na changamoto nyingi. Lakini jambo muhimu ni kwamba, nchi za Afrika zinapaswa kujipatia maendeleo, na watu wanapaswa kuwa na chakula cha kutosha, mazingira mazuri zaidi ya kuishi na kupata elimu nzuri."

    Lakini si rahisi kutimiza lengo la maisha bora wanayotarajia watu wa Afrika, katika miaka mingi iliyopita, watu wa Afrika wamekuwa wakitafuta njia mwafaka ya kujiendeleza. Machoni mwa Waafrika wengi, maendeleo ya China ni mfano mzuri wa kuigwa. Mwanafunzi kutoka Cote d'Ivoire anayesoma nchini China Bw. Grafoute Amoro anaona kuwa, Afrika inaweza kuiga uzoefu wa China wa kujiendeleza. Alisema,

    "Nina matumaini kuwa nchi yangu inaweza kujifunza kutoka kwa China na watu wake kuhusu namna ya kuendeleza nchi yao kwa kasi. Naona kuwa ingawa ni kweli tunahitaji fedha, lakini tunachohitaji zaidi ni wazo na uzoefu wa China."

    Kwa kuwa kiwango cha maendeleo cha nchi za Afrika ni tofauti, hivyo sio tu serikali za nchi mbalimbali za Afrika na wananchi wao wanahitaji kufanya juhudi, bali pia zinahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa. Kwa hiyo kazi ya Umoja wa Afrika inapaswa kuzingatiwa. Waafrika wengi wana matarajio makubwa kwa Umoja wa Afrika katika kuboresha mazingira ya maisha na kuinua kiwango cha maisha yao. Msimamizi wa kampuni ya Senegal Bw. Diop alisema,

    "Tuna matarajio makubwa na Umoja wa Afrika, kwani hivi sasa tunatilia maanani mawasiliano ya kiuchumi kati ya kanda mbalimbali. Umoja wa Afrika una kazi nyingi, kwa kuwa hivi sasa ushirikiano wa kikanda si wa kina, na bado hatuna soko la pamoja, hivyo tunapenda umoja huo uweze kutimiza lengo hilo."

    Mwakilishi mkuu wa Umoja wa Afrika kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai Bw. Nadir Merah alisema, ingawa si muda mrefu tangu Umoja wa Afrika uanzishwe, lakini umetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi 53 wanachama, na umepata mafanikio katika kuepusha migogoro ya kikanda na kuhakikisha utoaji wa chakula. Bw. Merah alisema Umoja wa Afrika umetunga mkakati wa maendeleo ya muda mrefu, kutokana na msaada wa jumuiya ya kimataifa, Afrika hakika itashinda matatizo mbalimbali. Bw. Merah alisema,

    "Hivi sasa tuna mpango wa kimkakati wenye nguvu kubwa, pamoja na uhusiano mzuri kati yetu na nchi nyingi duniani ikiwemo China, nadhani tunaweza kuondoa changamoto zinazotukabili."

    Maonesho ya kimataifa ya Shanghai yanayokusanya busara kutoka nchi mbalimbali duniani kuhusu maendeleo ya miji katika siku za baadaye, yamezipa nchi za Afrika fursa nzuri ya kuonesha umaalum wake na kuiga uzoefu wa nchi nyingine duniani kuhusu maendeleo ya miji. Mjumbe wa kamati ya Umoja wa Afrika anayeshughulikia mambo ya biashara na viwanda bibi Elisabeth Tankeu alisema,

    "Tunatarajia kwamba kupitia maonesho ya kimataifa ya Shanghai, kamati ya Umoja wa Afrika na nchi wanachama wake zitaweza kupata njia mpya, ili miji ya nchi za Afrika itimize lengo la amani na usalama kwa kupitia maisha bora."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako