• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mji mdogo wa kale Pingle

    (GMT+08:00) 2010-06-28 14:47:18

    Tokea zama za kale kulikuwa na msemo mmoja nchini China unaosifu Chengdu, mji mkuu wa mkoa wa Sichuan kuwa ni sehemu ya "peponi", Chengdu ina hali nzuri ya hewa na mavuno mazuri ya kilimo, wakazi wa huko wanapenda hali ya starehe na utulivu katika maisha yao. Watalii wengi wanavutiwa kwenda Chengdu kushuhudia maisha ya starehe na utulivu ya wakazi wa huko, hususan kwenye baadhi ya tarafa na vijiji vya kale vilivyoko kwenye sehemu inayouzunguka mji wa Chengdu.

    Mji mdogo wa kale Pingle uko umbali wa kilomita 93 kusini magharibi mwa mji wa Chengdu, ambayo imethibitishwa kuwa mji mdogo maarufu wa kihistoria na kiutamaduni, mji wenye mazingira mazuri na ni moja ya "miji kumi ya wilaya ya kuvutia zaidi" nchini China. Maji ni kitu cha kuvutia zaidi katika mji mdogo wa kale Pingle, ambayo yanaonekana kati ya majengo ya kale, mtu akitembea kwa miguu kwenye maeneo ya majengo hayo anasikia raha sana. Mwongoza watalii Zhu Dan alisema, "Hivi sasa mtaa wetu huu unaitwa 'mtaa wenye mandhari ya maji', mfereji huu una urefu wa mita zaidi ya 500, juu ya mfereji huu yamejengwa madaraja zaidi ya 10 wanayopita watu, na kila daraja ni tofauti na lingine. Kwenye mtaa huu kuna vitu vingi vyenye umaalumu wa mji huo mdogo, kwa mfano, nyama ya kondoo ya Wanwan, tambi zenye maziwa, nyama ya kuku ya Benben, mgando wa maharage au doufu unaotiwa hamira, keki za ufuta, ambazo ni umaalumu wa mji mdogo wa Pingle."

    Hali ya kale ni moja ya umaalumu wa mji mdogo wa kale Pingle. Katika kipindi cha enzi ya Han ya Magharibi, mwaka 150 KK, yaani miaka zaidi ya 2,000 iliyopita, ilikuwepo mji mdogo wa kale Pingle, vitu 9 vya kale vya mtaa, hekalu, daraja, miti, kingo za mto, karakana, barabara, mambo ya jadi na nyimbo, vinaonesha utamaduni mkubwa wa kale wa Pingle. Mji mdogo wa kale Pingle iko kwenye kando ya mto Baimo, mto huo wenye maji mengi unachukuliwa na wenyeji wa huko kuwa ni mto mama. Mti mmoja wa Banyan, ambao ulianza kuota kwenye daraja kiasi cha miaka 1,500 iliyopita, ni kama kitu kinacholinda mji huo. Mwongoza watalii Zhu Dan alisema "Mti tunaouona sasa ulianza kuota kabla ya miaka 1,500 iliyopita, hadi sasa bado unaendelea kustawi, kwa hiyo wenyeji wa hapa wanasema mti huu una roho. Hapa kuna mila moja, yaani watoto wachanga wanaozaliwa hupelekwa huko na kuwafanya kama watoto wa mti huo wa kale, ili ulinde usalama wa maisha yao. Kila ikifika tarehe 1 na 15 kwa kalenda ya kilimo ya China, wafanyabiashara wa huko vilevile wanakuja kutambika kwenye mti huu na kuomba uwabariki katika shughuli za biashara."

    Katika mji mdogo wa kale Pingle, licha ya watu kuweza kuona mandhari ya asili na majengo ya kale, pia wanaweza kuona utamaduni wa jadi. Hata sasa bado watu wanaweza kuona karakana ya wahunzi iliyojengwa miaka zaidi ya 100 iliyopita na kuendeshwa na vizazi vitatu vya watu wa familia hiyo, studio ya picha iliyoanzishwa katika kipindi cha Jamhuri ya China, chakula chepesi kitamu cha jadi, ambacho kilikuwepo zaidi ya miaka 100 iliyopita, n.k. Sehemu hii si sehemu ya utalii peke yake, wenyeji wengi wameishi huko kwa karne kadhaa, hadi hivi sasa bado wanadumisha mtindo wa maisha ya jadi.

    Kwenye mtaa wa kale, kuna duka moja linalouza kiungo cha Douchi, watu hata wakiwa mbali wanaweza kusikia harufu ya viungo hivyo vya vitoweo vya mkoa wa Sichuan. Bango moja lililoandikwa maneno yasemayo "Duka la zamani kabisa la Pingle" lililotundikwa kwenye mlango wa duka, bango hilo linaonesha tofauti kati yake na maduka mengine. Mwenye duka Bibi Chen alisema, "Maneno hayo ni sifa nilipewa na serikali, inadhihirisha kuwa mimi ninafanya vizuri shughuli hizo toka utotoni mwangu. Duka hilo ni la zamani sana. Wateja wengi wanakuja kununua viungo dukani, wateja wanaweza kuonja ladha yake kabla ya kununua".

    (Mteja: Ninaweza kuonja kwanza?)

    "Sawa kabisa, kiungo hiki kina ladha ya Huajiao, kinaweza kutumika katika kitoweo cha pilipili, mgando wa viazi na nyama ya sungura; kiungo hiki kilitengenezwa pamoja na sosi tamu, watu wasiopenda pilipili wanaweza kukitumia wakati wanapokula Mandou, aina ya mkate uliuotengenezwa kwa mvuke….."

    Watalii wengi wanaotembelea mji mdogo wa kale Pingle, wanapenda kukaa kwa siku nyingi kidogo, kwa sababu wanataka kupunguza kasi ya ratiba ili kujiunga na maisha ya starehe na mapumziko ya huko. Mwongoza watalii Zhu Dan alisema,

    "baada ya watalii kufika hapa, wanaweza kuungana haraka na maisha ya mji wetu, na kushuhudia hali na mtindo wa maisha ya jadi kabisa. Mandhari ya mji wetu ni nzuri sana, hapa kuna milima na mito, wakazi wa mji huu wanaishi maisha ya starehe na mapumziko, wakimaliza shughuli zao, wanapenda kutengeneza chai, wanakunywa chai na kuongea na marafiki zao, mtindo huo wa maisha unapendwa sana na wakazi wa hapa."

    Katika mji mdogo wa kale Pingle hakuna aina nyingi za burudani, sababu ya watalii kutembelea hapa ni unafuu wa huduma, wanataka kupumzika kwenye kando ya mto Baimo, kunywa chai, kucheza karata na kupata hewa safi ya huko, wanaona raha mustarehe. Mandhari ya usiku ya tarafa hii ni nzuri sana, wenyeji wanaoishi katika nyumba za zamani zilizoko kwenye kando za mto, huwasha taa za jadi zenye rangi mbalimbali, zikiwa pamoja na maji ya mto zinatengeneza mandhari nzuri ya kupendeza. Wakati huu, licha ya watu kuweza kuburudika kutokana na mandhari nzuri ya usiku, wanaweza pia kuonja mishikaki na kwenda kuweka taa za mishumaa kwenye maji ya mto na kuomba mambo mema. Chini ya mwanga wa taa, wanastarehe pamoja na marafiki au watu wa familia zao.

    Watu wanaotembelea mji mdogo wa kale Pingle katika nyakati mbalimbali wanaweza kuona shughuli mbalimbali za sherehe, mwongoza watalii Zhu Dan alisema, "Mji mdogo wa kale Pingle umeanzisha tamasha la taa katika sikukuu ya Qingming, na gulio la hekalu tarehe 11 Machi kwa kalenda ya kilimo ya China, katika siku hizo kunakuwa na shamrashamra nyingi. Licha ya hayo katika kila tarehe 6 Juni kwa kalenda ya kilimo ya China, kuna sherehe kubwa, kwani siku hiyo ni siku ya kuzaliwa kwa Buddha wa mlima Jinhua. Sherehe hizo ni kuweka taa za mishumaa kwenye maji ya mto pamoja na taa za Conming, ambazo zinaweza kupanda na kufika angani. Katika majira ya joto, tunafanya sherehe ya kuimba nyimbo za mapenzi mtoni, wakazi wa hapa pamoja na watalii wanaweza kujiandikisha na kushiriki."

    Mji mdogo wa kale Pingle una eneo la kilomita za mraba 80, mbali na sehemu ya kati ya tarafa, watalii wakiwa na muda wa kutosha, wanaweza kutembelea vivutio vingine vya karibu. Umbali wa kilomita 1 kutoka kwenye mji huo mdogo, kuna njia ya hariri ya sehemu ya kusini, ambayo ni njia ya usafirishaji iliyotumika katika enzi ya Qin na Han, wanaweza pia kupumzika kwa kupika na kula chakula kwenye korongo la Jinji au kutembelea hekalu la mlima wa Jinhua.

    Sehemu hizo ni karibu na mji wa Chengdu, usafiri ni mzuri pia, tena mahoteli yaliyoanzishwa na wakulima wa huko ni za bei nafuu, hivyo kupumzika kwenye mji mdogo wa kale Pingle mwishoni mwa wiki kumekuwa chaguo la kwanza kwa wakazi wa Chengdu. Mkazi wa Chengdu, Bw Hu alisema, tokea majira ya Spring ya mwaka huu yaanze, karibu kila mwisho wa wiki yeye na watu wa familia yake wanafika huko. Alisema "Ninafika hapa kila wiki, kwani hapa ni karibu sana na Chengdu, nina kazi nyingi kila siku, hivyo ninapenda kupumzika mwishoni mwa wiki, kucheza karata, kunywa chai na kujiburudisha."

    Watu wanasema, kila mtu ana kumbukumbu tofauti kuhusu mji mdogo wa kale Pingle. Tunakukaribisha kutembelea na kupumzika katika mji mdogo huo wa kale.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako