• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji 0706

    (GMT+08:00) 2010-07-07 15:36:38

    Msikilizaji wetu Magdalena Pendo wa S.L.P 119 Asumbi Kenya anasema mimi ni msichana mwenye asili ya Kenya mwenye miaka 21 hivi, majuzi nilidokezwa na mjomba wangu ambaye ni shabiki wenu Ayubu Mutanda, kuhusu kipindi chenu na nikasikiliza na kukifurahia sana. Ningependa kushiriki na pia kujiunga nanyi kwasababu uraibu wangu ni kusikiliza habari, kuandika barua, kujifunza na kujihusisha na watu wenye hekima na maarifa kama nyinyi. Asante kwa ukarimu na mafunzo yenu mazuri, Maulana awabariki.

    Shukrani nyingi msikilizaji wetu Magdalena Pendo kwa barua yako fupi ya kuomba kujiunga nasi, kwa kweli sisi kwa upande wetu hatuna matatizo hata kidogo na tunakukaribisha kwa mikono miwili uwe msikilizaji wetu, pia unaweza kushiriki kwenye chemsha bongo zetu pamoja na kutuma barua na kadi za salamu. Ahsante sana.

    Msikilizaji wetu Daniel Msobi Mponeja wa S.L.P 18 Mwanza Tanzania, ametuletea barua akisema ndugu wa CRI naomba kuwajulisha kuwa nimepokea zawadi yenu mliyonitumia ya chemsha bongo kuhusu maadhimisho ya miaka 60 tangu China ianzishwe. Zawadi hiyo nimeipokea tarehe 17, Februari mwaka huu, ambayo ni fulana ya rangi ya maziwa yenye nembo ya CRI pamoja na cheti, na ninawapongeza sana kwa kunichagua kuwa mshindi wa tatu, nami sina budi kusema mara nyingine Mungu anijaze akili ili niweze kuwa mshindi maalumu au wa kwanza.

    Pia mimi napenda sana kujifunza lugha ya kichina, hivyo naomba mnitumie kitabu cha jifunze kichina ili niweze kuelewa haraka, aidha naomba mnitumie kalenda ya ukutani bila ya kusahau picha ya rais Hu Jintao wa China. Nitafurahi sana kama ombi langu mtalipokea kwa mikono miwili. Mwisho nawatakia kila la Kheri katika utendaji wenu wa kazi, ni matumaini yangu kuwa mtajituma zaidi, ahsante.

    Shukrani nyingi sana msikilizaji wetu Daniel Msobi Mponeja, kwa kweli hata sisi pia tunakupongeza kwa ushindi huo ulioupata, ila tunakuomba tu uzidishe bidii zaidi ili upate nafasi maalumu katika shindano jingine la chemsha bongo.

    Msikilizaji mwingine ni Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga Tanzania anasema natumai wafanyakazi wote wa redio China Kimataifa mko wazima kabisa na mnaendelea na shughuli zenu za kila siku, na mimi naendelea vyema na majukumu yangu ya kazi katika kuijenga nchi yangu ya Tanzania, vilevile naendelea kuitegea sikio vyema idhaa ya Kiswahili ya CRI pamoja na kuwasiliana nayo kwa njia ya barua.

    Baada ya hayo mwaka huu wa 2010 ni mwaka wa nchi ya Afrika Kusini hapa barani Afrika, ambapo nchi hii ya Afrika Kusini mwaka huu ni mwenyeji wa michuano ya kombe la dunia, ambapo michuano hii inafanyika katika miji mbalimbali kama Johannesburg na Durban tarehe 11/6 na kumalizika Julai 11/2010. katika mji wa Durban huko Afrika Kusini kuna uwanja wa mpira ambao ni wa pili kwa ukubwa barani Afrika unaojulikana kwa jina la Moses Mabida na unachukua watu elfu 60 wote wakiwa wameketi.

    Hivyo basi sina budi kuwatakia wanamichezo mbalimbali wa Jamhuri ya watu wa China watakao shiriki michezo ya kombe la dunia huko Afrika kusini, mola awasaidie ili wafanye vizuri katika michezo hiyo na kujinyakulia medali nyingi za aina mbalimbali kama vile fedha, dhahabu pamoja na shaba, vilevile pamoja na kulichukua kombe hilo la dunia kule Afrika Kusini na kulipeleka China. Nawafagilia sana wanamichezo wote wa China na ninawatakia bahati njema mungu awasaidie sana katika mashindano hayo ya kombe la dunia.

    Vilevile napenda kuchukua fursa hii ili kuwapongeza na kuwashukuru sana wafanyakazi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa kwa kunitumia majarida saba ya China Daily, bahasha zilizokwisha lipiwa gharama za stempu pamoja na kadi za salamu, vyote hivyo nimevipokea salama, asante sana. Mwisho ninawatakia wafanyakazi na wasikilizaji wote wa redio China Kimataifa kila la kheri pamoja na mafanikio mema katika mwaka huu wa 2010.

    Ahsante sana msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija kwa barua yako, kwa kweli kombe la dunia hivi sasa linaendelea kuchanja mbuga, na linaelekea ukingoni tena, ambapo tarehe 11 mwezi huu tutamjua bingwa wa soka wa dunia, lakini pia tunapenda kukueleza kuwa kwa bahati mbaya China haikufanikiwa kuingia kwenye michuano hii, ila tuiombee dua ifanikiwe katika michuano ya mwaka 2014 itakayofanyika huko Brazil.

    Msikilizaji wetu mwingine ni Bwana Abdi Saidi Iyubu wa S.L.P 316 Kondoa Tanzania. Yeye ana maoni yanayosema kwamba, Kushirikiana na Russia kutoa hoja ya kuwepo kwa makao ya Umoja wa Mataifa katika sehemu mbili na kuitetea hoja hiyo.

    Anasema hivyo kwa sababu siasa zinazotawala dunia hii ni za mifumo miwili yaani mfumo wa siasa ya kijamaa (Communist) na mfumo wa kibepari (Capitalist). Hivyo New York ibakie kwa mataifa ya Kibepari na Kifalme, na kwa mataifa ya serikali za kijamaa (Communist) iwe aidha Moscow Russia au Beijing China. Kwa sababu 75% ya mataifa ya dunia hii ni ya serikali za kijamaa (Communist) lakini serikali za mataifa hayo zinashindwa kujipanga kiutawala unaolingana na maazimio ya mifumo ya malengo ya siasa zao. Kutokana na kukosekana kwa makao makuu yanayoweza kujishughulisha kikamilifu katika uendeshaji wa serikali zao za mfumo wa kijamaa (communist) kama ilivyo kwa mataifa ya kibepari (NATO). Kwa sababu mataifa yote yanayowapata viongozi wao kwa kutegemea uchaguzi wa wananchi wa taifa lolote lile ni mataifa ya mfumo wa kijamaa. Sio kama ilivyo kwa mataifa ya kibepari na kifalme, wagombea hupatikana kwa kura za uchaguzi wa maseneta, malodi, na wajumbe wa koo za kifalme na watu wengine walio wengi ndani ya mataifa hayo ni watimiza mradi tu hata wasipochaguliwa tayari viongozi wao wameshachaguliwa na watu wa madaraja niliyoyataja hapo juu.

    Pili, mataifa haya ya kijamaa malengo yao ya kutaka kuendesha serikali zao kwa mfumo wa serikali za kijamaa (communist) yanashindikana kutokana na kuyumbishwa na elimu hii ya kada hizi tano za utawala za uchumi, biashara, uongozi, utawala na sheria. Kwa sababu wahitimu wa kada hizi wanapohitimu shahada zao ni moja kwa moja wanakuwa wameingia katika mfumo wa kibepari, hili ni moja ya tatizo linalozikumba nchi au mataifa ya mfumo wa kijamaa kwa sababu ya kukosekana na kuwemo kwa ubunifu wa utunzi wa vitabu vya mfumo wa uchumi na utawala wa kijamaa (communist). Kwa hiyo, hali hii ndiyo inayosababisha mataifa yetu kubakia gizani na kuona sera za mifumo ya kibepari ni nzuri kwa sababu hakuna ubunifu mbadala wa mfumo wa kijamaa ambao ni mzuri na unarahisisha maisha ya watu hapa duniani. Mwisho nasema asanteni sana na nawatakia kila la heri kwa mwaka wa 2010.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Abdi Saidi Iyubu kwa maoni yako mazuri kabisa kuhusu China kushirikiana na Russia kutoa hoja ya kuwepo kwa makao ya Umoja wa Mataifa katika sehemu mbili na kuitetea hoja hiyo. Kwa kweli tunanafurahishwa na sana na maoni yako na tunakuomba tu uendelee kutuandikia zaidi. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako