• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Jumba la maonesho la pamoja la Afrika lawa jukwaa la kuonesha sura za nchi mbalimbali za Afrika

    (GMT+08:00) 2010-07-22 16:24:09
    Hivi karibuni idadi ya watalii wanaotembelea Jumba la pamoja la Afrika kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai imezidi milioni 7.5, na inakaridiwa kuwa hadi mwishoni mwa mwezi Julai, idadi hiyo itazidi milioni 10.

    Tarehe 1 Novemba mwaka 2007 Libya ilithibitisha kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai, baada ya hapo, nchi 48 za Afrika zenye uhusiano wa kibalozi na China, zote zilikuwa zimethibitisha kushiriki kwenye eneo la maonesho hayo. Jumba la pamoja la Afrika lililoko sehemu C kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai lina majumba ya maonesho ya nchi 43 za Afrika na jumba la maonesho la Umoja wa Afrika. Huko watu wanaweza kuona vitu mbalimbali vya Afrika vikiwemo nguo, chakula, nyimbo na ngoma, hivyo wanaweza kujionea wenyewe tamaduni mbalimbali za bara la Afrika.

    Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni muziki uliopigwa na bendi ya "Alves Brader's" ya Cape Verde. Bendi hiyo iliundwa na ndugu watatu, na inajulikana sana nchini Cape Verde. Mwimbaji mkuu wa bendi hiyo Bw. To Alves alisema,

    "Nashukuru sana maonesho ya kimataifa ya Shanghai kwani yametupa fursa hii ya kuweza kuwasiliana na watu na kuona tamaduni mbalimbali, nayatakia maonesho ya kimataifa ya Shanghai mafanikio!"

    Ili nchi mbalimbali za Afrika ziweze kuonesha vizuri mila na desturi zao, China imetoa msaada mkubwa kwa nchi hizo katika ujenzi na mpango wa majumba yao. Waziri wa biashara na viwanda wa Ghana bibi Hanna Tetteh kwenye sherehe ya kuadhimisha siku ya jumba la maonesho la Ghana alisema,

    "Kwa niaba ya rais wa Ghana na wananchi wa Ghana, ningependa kuishukuru serikali ya China na watu wake kwa kuandaa maonesho ya kimataifa, na ningependa kuishukuru serikali ya China kwa kuiunga mkono na kutoa msaada kwa Ghana, ambao umeiwezesha kushiriki kwenye maonesho haya bila vikwazo."

    Mwakilishi mkuu wa Jumba la maonesho la Cape Verde Bw. Joao Vieira pia aliishukuru sana China kwa msaada inayotoa kwa nchi zinazoendelea. Alisema,

    "Kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai, China imetoa misaada mingi kwa nchi zinazoendelea. Bila misaada hiyo, tusingeweza kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa."

    Jumba la pamoja la Afrika linawavutia watalii wengi. Mfanyabiashara kutoka Msumbiji Bw. Zeca Logomale alisema, hapa watalii wa China wanaweza kuona wenyewe sanaa za mikono za Afrika. Pia alisema kazi nzuri ya maandalizi ya maonesho ya kimataifa ya Shanghai ilimfanya ajione kama amerudi barani Afrika. Alisema,

    "Sasa inakaribia miaka miwili tangu niondoke barani Afrika, lakini nilipokuja hapa, nilijiona kama nimerudi katika maskani yangu, barani Afrika. Hili kweli ni jambo zuri sana. Na jumba hili la maonesho pia linapendeza sana."

    Bila shaka mafanikio yanayopatikana kwenye maonesho ya Jumba la pamoja la Afrika hayatengani na juhudi za nchi mbalimbali za Afrika zinazoshiriki kwenye maonesho ya kimataifa. Ofisa mkuu wa idara ya usimamizi ya Jumba la maonesho la pamoja la Afrika Bw. Chen Jintian aliona kuwa, nchi mbalimbali za Afrika zimefanya maandalizi mazuri, hivyo jumba la pamoja la Afrika limekuwa moja ya majumba yanayowavutia watalii wengi zaidi. Bw. Chen alisema,

    "Nchi za Afrika zinaona fahari sana kwa kuwa na jukwaa kubwa la kuonesha mambo yao mbalimbali kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai. Aidha tunashirikiana nao kwa karibu, hivyo watu wanalisifu sana jumba hili."

    Bw. Chen alifahamisha kuwa, Jumba la pamoja la Afrika linaweza kupokea watu elfu 50 kwa siku, lakini hivi sasa kila siku idadi ya watalii wanaotembelea jumba hilo imezidi elfu 50, na idadi hiyo iliwahi kufikia laki 1.8. Bw. Chen alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Julai, idadi ya watalii wanaotembelea Jumba la maonesho la pamoja la Afrika itazidi milioni 10, na anaamini kuwa idadi hiyo itaendelea kuongezeka. Bw. Chen alisema baada ya kufungwa kwa maonesho ya kimataifa ya Shanghai, watu hawatasahau Jumba la pamoja la Afrika, na wala hawatasahau vitu mbalimbali vinavyooneshwa na Afrika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako