• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kupanda mlima Taishan

    (GMT+08:00) 2010-08-02 17:15:59

    Mlima Taishan uko kwenye upande wa mashariki wa milima mitano maarufu ya China. Mlima huu pia unaitwa mlima wa mashariki, na una sifa ya "mlima unaoongoza kati ya milima mitano" na "mlima unaochukua nafasi ya kwanza nchini China". Mlima huu licha ya kuwa na mandhari nzuri ya kimaumbile, una historia na utamaduni wa miaka mingi, ni bustani kubwa ya mlima ya maumbile, na vilevile ni mfano wa historia na utamaduni wa taifa, mlima Taishan uliorodheshwa kuwa urithi wa maumbile na urithi wa utamaduni wa dunia kwa wakati mmoja, hali kama hii haikutokea hapo kabla..

    Ni vizuri kutembelea mlima Taishan kwa kufuata njia ya lango jekundu, ambayo ni njia kuu ya katikati iliyotumiwa na wafalme wa enzi mbalimbali. Njia hii yenye ngazi za mawe inayopindapinda na kuzunguka mlimani, ina miti mingi mikubwa kwenye kanda zake mbili, watu wanaona milima mizuri, maji yanayotiririka kwenye vifereji, mabaki mengi ya kale ya kiutamaduni, hivyo njia hii inapendwa pia na wasomi na watu wa kawaida. Mwongoza watalii Lu Hong alisema

    "Kutembea kutoka kwenye lango jekundu hadi kwenye lango la mbinguni la kusini kuna ngazi 6,293, kwenye njia hii inayopindapinda kuna vivutio mbalimbali vya kimaumbile, hususan mizunguko 18, ambapo njia inazunguka mara 18 na ina hatari kutokana na kuwa na mtelemko mkali wenye mita zaidi ya 400, sehemu hii ina ngazi zaidi ya 1,600 inayoelekea hadi kwenye lango la mbinguni la kusini. Njia hii ilitumiwa na wafalme wa enzi mbalimbali kwenda kutoa sadaka kwa mungu kwenye jukwaa lililojengwa juu ya mlima. Mizunguko 18 ni sehemu inayopima uwezo wa nguvu za mwili na imani ya wapanda mlima."

    Njia ya pili ni kutoka kijiji cha Tianwai hadi lango la katikati la mbinguni, njia hii inapinda kwa mara 9. Kwenye njia hii kuna bwawa lenye kina kirefu la Helong, daraja la Changshou na genge la Shanzi, mandhari za sehemu hizi ni nzuri sana kutokana na kuwa na vivutio vya maji yanayozunguka mlimani.

    Njia inayopita Houshiwu, ambayo ni sehemu yenye vivutio vingi ikiwa ni pamoja na milima na makorongo mazuri, misonobari na mawe ya kupendeza, chemchemi za mlimani, vifereji na maporomoko ya maji. Watalii wanaona mandhari hayo ni kama michoro ya kupendeza, kwa hiyo sehemu hii pia inaitwa "ujia wenye michoro wa kilomita 5", ambayo ni njia inayopendwa kufuatwa na watalii wanaopenda kugundua maajabu na vitu visivyo vya kawaida.

    Sehemu nzuri zaidi iko kwenye kilele cha Dai cha mlima Taishan. Baada ya kupanda kwenye lango la kusini la mbinguni, watu wanaweza kutembea kwenye ngazi za mawe za Tianjie, ambapo wanaweza kujiona kama wanatembea peponi huku wakiburudishwa kwa mandhari nzuri ya kimaumbile. Kwenye sehemu ya Yuhuangding, ambayo ni sehemu yenye mwinuko zaidi kwenye mlima Taishan, asubuhi watu wanaweza kuona jua likichomoza. Katika alfajiri ya kila siku, kuna watalii wengi wanaoangalia upande wa mashariki wakishuhudia jua likichomoza juu ya mawingu meupe.

    Mtalii Li Yongqing kutoka mkoa wa Guangdong alisema, "Mimi ninatoka Guangdong, watu watatu wa familia yangu wote tumekuja kupanda mlima Taishan na kuangalia jua likichomoza. Watu wanasema, mtu akipanda mlima Taishan atakuwa na usalama maishani', mwaka huu nitapata kila la heri kazini na maishani."

    Watalii wakiwa kwenye kilele cha Dai wanaweza kuona "milima mingine yote ni midogo", licha ya hayo wanaweza kuona mandhari nne nzuri za kimaumbile ikiwa ni pamoja na 'jua jekundu likichomoza', 'mawingu ya rangirangi ya machweo', 'bahari ya mawingu' na 'mkanda wa dhahabu wa mto Manjano'. Bi.Zhang alisema, 'Wakati mzuri wa kutembelea mlima Taishan ni kati ya mwezi Aprili na Novemba, kwani hali ya hewa katika kipindi hiki ni nzuri, watalii wanaweza kuona vizuri jua likichomoza asubuhi."

    Ingawa mvua inanyesha sana katika majira ya joto kwenye mlima Taishan, lakini watu wanaotembelea huko wakati huo, mara kwa mara wanaweza kuona mandhari nzuri ya bahari ya mawingu. Kutembelea huko katika majira ya baridi, watu wanapata fursa nyingi zaidi za kuona jua likichomoza asubuhi, na kama theluji ikianguka, mandhari inapendeza zaidi.

    Lakini mbali na mandhari nzuri, watalii wanaotembelea mlima Taishan wanaweza kupata chakula maarufu cha huko cha Doufu, samaki wekundu na Jianbing.

    Kutembelea mlima Taishan ni sawa na kufanya matembezi ya kiutamaduni, hususan kwenye shughuli zinazofanyika kwenye mahekalu kila mwaka baada ya sikukuu ya Spring, watu wanaweza kuona vitu vingi vya sanaa vinavyotengenezwa kwa mikono, chakula chepesi cha huko na maonesho ya michezo ya sanaa.

    Mtalii kutoka mkoa wa Heilongjiang Wang Yong alisema, "Kutalii kwenye mlima Taishan ni sawa na kufanya utalii wa kiutamaduni, licha ya kuangalia mandhari nzuri, ninataka kushuhudia shamrashamra ya gulio na vyakula vyepesi vya hapa. Hekalu la Dai linatilia mkazo kwenye mambo ya kiutamaduni, vilevile linawaandalia watalii shughuli za burudani, ninaona hali hii ni nzuri sana."

    Toka zamani za kale, wachina wanaabudu mlima Taishan, wafalme wa enzi mbalimbali walikwenda huko kutoa sadaka kwa mungu na kujenga mahekalu. Mlima Taishan unachukuliwa kama ni "mlima wa mungu" na "mlima wa utamaduni", na ni maskani ya kiroho ya wachina.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako