• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji 0803

    (GMT+08:00) 2010-08-03 16:45:16

    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Mchana J Mchana wa S.L.P 1878 Morogoro Tanzania, anasema madhumuni ya kuandika barua hii ni kuiomba CRI iwakutanishe wasikilizaji wa Tanzania na Kenya. CRI ina kituo cha redio ni vizuri kukaandaliwa tamasha la kuwakutanisha wasikilizaji wake ili kufahamiana zaidi na kutufanya tuwe na marafiki na ndugu wa karibu, naomba hilo kwasababu sisis tumekuwa ndugu wa karibu kwa maoni na salamu, kwani jambo hilo litaisaidia CRI kupanuka zaidi na kuwa karibu na wasikilizaji wake.

    La pili ni kuhusu watangazaji wa CRI naombe waige mfano wa Fadhili Mpunji wa kukutana na wasikilizaji na nampongeza sana kwa kukutana nami uso kwa uso hongera kwa hilo.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Mchana J Mchana kwa maoni yako, kuhusu ombi lako la kukutanishwa kwa wasikilizaji wa CRI, kwa hivi sasa itakuwa vigumu kidogo, lakini ombi hilo tayari tumelipokea na labda tutalifanyia kazi baadaye.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Wilson Julius Akhusama wa S.L.P 2191 Kakamega Kenya anasema natoa shukurani kwa mliyonifanyia, mimi ni shabiki sugu wa salamu na maswali ya chemsha bongo, natoa shukurani zangu nyingi kwa CRI, kwa juhudi zenu njema, kutokana na zawadi mlizoniletea ni za hali ya juu, zawadi hizo ni pamoja na cheti cha heshima nawashukuru sana tena Mungu awabariki.

    Nikimalizia nahitaji nambari yangu ya uanachama pamoja na mtihani mwingine.

    Msikilizaji wetu Bi. Mwanahawa Akoth wa S.L.P 34-40602 Ndori Kenya anasema asalam aleikum, nataraji kuwa hamjambo mimi na aila yangu tu wazima kama kigongo, madhumuni hasa ya barua hii ni kutoa shukurani zangu za dhati kwenu kwa zawadi kemkem mlizonitumia hivi karibuni zikiwa ni pamoja na magazeti ya China Daily, ambayo yanaendelea kunielimisha vilivyo, hususan kuhusu yale yaliyotokea nchini China yakiwemo masuala ya uchumi, michezo, siasa na mengineyo mengi yenye manufaa.

    Mbali na hayo nimepokea pia bahasha zilizolipwa, kalenda ya mwaka huu, masuali kuhusu maonesho ya Shanghai ingawaje muda umeyoyoma na pia picha mbili za makabila madogo ya Manchu na Kazak, ama kweli haya yote yananitia moyo na kunipa furaha nyingi, kwani asiyekujua hakuthamini,

    Kwa kumalizia naomba ushirikiano huu uendelee kwa manufaa yetu sisi sote. Ahsanteni.

    Nasi tunawashukuru sana wasikilizaji wetu Wilson Julius Akhusama na Bi. Mwanahawa Akoth kwa barua zenu, zinazoonesha wingi wa furaha mliyonayo kwa kupata zawadi mbalimbali, sisi tunawapongeza pia tunawataka muendelee kushiriki zaidi kwenye mashindano tunayoyaandaa hapa CRI na kusikiliza vipindi vyetu mbalimbali.

    Ni barua yake Bwana Philip Ng'ang'a Kiarie anayetunziwa barua zake na Kiarie Ndumbi wa S.L.P 601 Maragua Kenya, anasema kwanza nawapa mkono wa salamu wafanyakkazi wa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa. Pili sina budi kuipongeza serikali ya China kwa kuzidi kusaidia kupitia misaada isiyo na masharti yoyote.

    Mbali na hayo vitu vyenye ubora na bei nafuu na vyombo mbalimbali ambavyo hutumiwa na watu wenye mapato ya chini vimewasaidia sana katika nyakati hizi, kwa mfano vijana wengi wameanzisha biashara za uchukuzi wa bodaboda huku wakitumia pikipiki zenye chapa maalumu ya China ambapo wanajipatia vyanzo vya mapato, huku shida za ajira miongoni mwa vijana zikipungua. Nashukuru sana.

    Aidha kwa kweli watu wengi siku hizi wanaelewa nchi ya China kuwa ni yenye ujuzi na wana hamu kubwa sana ya kuelewa utamaduni, mila na desturi za watu wa China. Kufuatia kuanzishwa kwa chuo cha confucious hapa nchini Kenya na masomo ya kuwa nasi jifunze kichina kupitia matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa.

    Ni wazi kuwa lugha ya kichina inaendelea na kuenea hapa Kenya na vijana wengi wanaendelea kujifunza lugha hii, na hivi juzi nilifurahi sana kwa kuona tangazo kwenye gazeti moja ambalo ni maarufu hapa nchini, likiwatakia wananchi wa China heri njema ya sikukuu ya mwaka mpya, tangazo hilo lilikuwa limeanzia hivi "nihao China". Ahsante.

    Shukurani za dhati Bwana Philip Ng'ang'a Kiarie kwa maoni yako murua kabisa, kwa kweli kama ulivyosema hivi sasa lugha ya kichina inazidi kuenea na si Kenya pekee bali duniani, kwani watu wengi wamepata mwamko wa kujifunza, hili ni jambo la kujivunia kabisa, ahsante sana.

    Barua ya sasa inatoka kwake Bwana Ramadhani Hamisi wa S.L.P 14-40602 wa Ndori Kenya. Anasema kwa watangazaji wote, habari zenu? Ni matumaini yangu kuwa siha zenu ni njema kama vile yangu na ya familia yangu.

    Nachukua fursa hii adhimu kukushukuruni mno kwa mawasiliano yenu ya mara kwa mara. Nimekuwa nikipokea bahasha zilizolipiwa, vipeperushi vinavyoonesha ukuta mkubwa wa China, na kadi za salamu. Lakini sielewi ni kwa nini mmeamua kubadilisha aina za kadi za salamu na kutumia kadi zenye picha! Kadi kama hizi nimekuwa nikiziweka kwenye album ili kuzihifadhi kutokana na uzuri na kuwa ni picha za makabila madogo madogo nchini China. Hivyo basi huona ugumu kuzitumia kama kadi za salamu. Tafadhali tutumieni kadi za salamu za hapo awali.

    Nikifikia tamati, ningependa kuendelea kutoa pongezi zangu kwa serikali ya China kwa kufanikisha maonesho ya Kimataifa ya Shanghai yanayoendelea hivi sasa. Ahsanteni.

    Nasi tunakushukuru sana Bwana Ramadhani Hamisi kwa barua yako, lakini kuhusu kadi mpya za salamu usiwe na shaka unaweza kutumia, kwani hizo ndio kadi za siku hizi, na sababu ya kutumia kadi hizo ni kutangaza vivutio vya China kwa hiyo huna haja kuwa na wasiwasi unaweza ukahifadhi kwa zile ambazo unazipenda.

    Na barua ya mwisho inatoka kwa Elias Lufungulo Kamena wa S.L.P 201 Geita, Mwanza Tanzania. Kwenye barua yake anatujulisha kuwa amepokea kalenda ya mwaka 2010 na picha ya Meng Gu Zu yaani kabila la wamongolia.

    Anasema nimepokea zawadi hizo nilizotumiwa na CRI bila wasiwasi nashukuru sana. Sasa naomba mambo mawili kwanza nitumiwe magazeti ya Kiswahili kutoka China ili niweze kudumisha urafiki wa raia wa China na Tanzania.

    Na pia naomba rafiki mmoja au wawili kutoka China, hao watanifundisha uzalishaji kwa njia ya kilimo bora kutoka China. Sababu mimi napenda sana kilimo na ninafurahia maendeleo ya kilimo kutoka China.Nashukuru sana,

    Asante sana bwana Elias Lufungulo Kamena kwa barua yako ambayo unaomba kutumiwa magazeti ya Kiswahili ya China, lakini kwa bahati mbaya siku hizi magazeti ya Kiswahili hayachapishwi nchini China, labda kama unataka ya kingereza tunaweza kukutumia, na kuhusu kupatiwa marafiki wa China kwa kweli ni suala gumu kidogo, kutokana na kazi zetu, tungependa kukushauri tu kama sehemu unayoishi unaweza kupata mtandao wa internate basi ni vyema ukatafuta kwa njia hiyo kwani ni rahisi mno kupata marafiki kwa njia hiyo, ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako