• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji 0810

    (GMT+08:00) 2010-08-10 17:07:02

    Msikilizaji wetu Mchana J Mchana wa S.L.P 1878 Morogoro Tanzania, anasema salamu kwa watangazaji na waandaaji wa vipindi wa redio china Kimataifa. Napenda kuwapongeza viongozi wa China kwa maandalizi ya maonesho ya Shanghai, na nakiri kuwa umoja wa viongozi na wananchi wa China ni wa kuigwa, kwani hadi leo hii hakuna taarifa mbaya zilizoripotiwa, kila idara imekamilika , Mungu awape nini, mshikamano wenu muuendeleze hivyohivyo hadi mwisho wa maonesho ili maadui wenu wabaki midomo wazi, maonesho ya mwaka huu hoyee.

    Aidha anasema napenda kuwapa pole watu wa Qinghai, kwa kuondokewa na watu wengi kwa wakati mmoja na kuharibiwa kwa miundo mbinu, ambayo inaweletea maisha magumu wale walionusurika na matetemeko na mafuriko ya mara kwa mara. Pia magonjwa nayo yanapata mwanya wa kupiga kambi kwenye matatizo kama hayo yanapojitokeza.

    Mkoa wa Qinghai, umepata pigo hivyo nawapa pole kwa yote yaliyotokea, Mungu azilaze mahali pema peponi roho za wale wote waliopoteza maisha. Pia Mungu awape unafuu majeruhi wote ili wapate nguvu za kuijenga Qinghai mpya na kujiletea maisha bora. Hongera rais wa China Hu Jintao kwa kuijenga upya Qinghai .

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Mchana J Mchana kwa barua yako, na tunapokea pole kwa niaba ya waathirika wote wa tetemeko la ardhi la Qinghai. Hivi sasa watu wengi wamepangwa au kuhamishiwa sehemu zilizo salama huku ujenzi wa miundo mbinu pamoja na nyumba kwa wale wote waliopoteza makazi, unaendelea, kwani serikali ya China inajitahidi sana ili kuhakikisha wananchi wake wote wanakuwa na maisha bora. Ahsante sana.

    Sasa ni barua ya Bi Zuhura Khavere wa S.L.P 34-40602 Ndori Kenya, anasema asalaam aleikum, ni matumaini yangu kuwa nyote hamjambo na mnachapa kazi barabara. Nachukua nafasi hii ya pekee kuandika barua hii ili kukujuzeni kuwa nimekuwa nikipokea bahasha zilizolipwa, picha ya ukuta mkuu wa China na kadi za salamu zenye picha zinazoonesha makabila madogomadogo ya China. Picha kama hizi aghlabu huwekwa kwenye album na sio kutumiwa kama kadi za salamu. Hivyo basi naomba kutumiwa kadi za salamu za hapo awali.

    Hata hivyo natoa pongezi na shukurani zangu za dhati, kwa redio hii kwa mawasiliano ya mara kwa mara nasi wasikilizaji, muendelee na moyo huohuo.

    Msikilizaji wetu Norman Khaoya wa S.L.P 4365-30200 Kitale Kenya, anasema ninafuraha nyingi kwa kupata fursa hii ya kuwasiliana nanyi kama wahusika wa CRI. Hongera sana kwa ari na juhudi ya kuwahimiza wasikilizaji wenu, nimekuwa na furaha sana tangu siku ya kwanza nilipojiunga nanyi kwani nimejua mengi kutoka kwenu. Sina mengi ya kusema ila ni kuwapa pongezi tu, ahsanteni.

    Shukrani za dhati wasikilizaji wetu Zuhura Khavere na Norman Khaoya kwa barua zenu. Tumefurahi kusikia kuwa zawadi tulizotuma zimekufikeni, hivyo tunawaomba tu muendelee kusikiliza matangazo yetu, na kuweza kutoa maoni yenu. Ahsanteni sana.

    Sasa tuko kwa Bwana Okongo Okeya wa S.L.P 381 Iganga Uganda, anasema waheshimiwa wapendwa, watu wa China na taifa rafiki na wakarimu mno kwa watu wote ulimwenguni, asanteni sana Mwenyezi Mungu mwenye uwezo wa kila jambo awabariki neema daima.

    Wapendwa wafanyakazi wa CRI na wasikilizaji wote popote pale walipo ulimwenguni napenda kuwapa heko na hongera sana kwa kujenga na kudumisha urafiki wetu zaidi, nauombea urafiki huu udumu milele amin.

    Pia napenda kuwajulisha kuwa katika siku za nyuma hali yangu ilikuwa si nzuri, kwani nilifanyiwa upasuaji kutokana na uvimbe niliokuwa nao tumboni, ingawa hivi sasa naandika barua hii nikiwa bado nasumbuliwa lakini nimepata nafuu sio kama mwanzo, na namuomba mungu anijaalie nipone haraka. Ahsanteni sana CRI na wasikilizaji wote kwa kunisikiliza na naomba dua na sala zenu ili nipone haraka zaidi.

    Kwanza tunakupa pole sana msikilizaji wetu Okongo Okeya kwa upasuaji uliofanyiwa, sisi tunakuombea kwa mola akupe uzima wa haraka, ili uweze kuendelea vyema na pilika zako kama kawaida. Na vilevile tunawaomba wasikilizaji wetu wamuombee rafiki yetu huyu ili apone haraka, ahsante sana.

    Msikilizaji wetu Kenedy Eliakimu Akhusama wa S.L.P 2191 Kakamega Kenya, anasema naomba kwenu niwe shabiki wa vipindi vya CRI kwasababu ya vipindi vyenu ambavyo ninavisikia kila siku, kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa. Vipindi vyenu hasa ni habari, mazungumzo baada ya habari, salamu zenu, chemsha bongo na vinginevyo kupitia KBC shirika la utangazaji la Kenya. Sina mengi ila namuomba Mungu awabariki watangazaji wa CRI na wafanyakazi wote.

    Shukrani za dhati msikilizaji wetu Kenedy Eliakimu Akhusama. Sisi tunasema usiwe na shaka kwani mtu yoyote anaweza kuwa shabiki wetu, hivyo endelea kusikiliza vipindi vyetu pamoja na kushiriki kwenye chemsha bongo.

    Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga Tanzania anasema natumai kuwa hamjambo sana wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa. Mimi ni mzima wa afya njema naendelea na majukumu yangu ya ujenzi wa taifa langu la Tanzania kama kawaida, sambamba na kufuatilia kila siku matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa.

    Awali ya hayo yote napenda kuwapa pole sana wananchi wa Haiti na Chile huko barani Amerika kwa kukumbwa na matetemeko ya ardhi yaliyotokea kwa nyakati tafauti na kusababisha vifo vya watu wengi zaidi na wengine kupoteza makazi pamoja na mali zao. Hivyo basi sina budi kuwaomba wananchi pamoja na viongozi wa nchi hizo wawe na subira, na kwa msiba huo tupo pamoja nao.

    Pia natumia wasaa huu kuzipongeza nchi zilizojitolea kuzisaidia nchi hizo, ambazo ni China iliyotoa misaada mbalimbali kama vile wataalamu wa fani ya uokozi n.k

    Aidha kwa upande mwingine nachukua wasaa huu kumpongeza rais wa kampuni ya kutengeneza magari ya kijapani, magari hayo aina ya Toyota, Bwana Hakiyo Toyoda kwa kujielezea kuhusu tatizo la kampuni yake ya magari ya Toyota na kutaka magari yenye hitilafu yarejeshwe viwandani. Aidha kampuni hii iliuza magari yapatayo milioni 8 katika nchi na sehemu mbalimbali duniani, ambapo mengi ya magari hayo yalinunuliwa huko Marekani na China ilinunua magari yapatayo laki 4, na mengine yaliyobaki yakanunuliwa na sehemu nyingine hapa duniani.

    Mwisho nawatakia marafiki zangu wote wa Redio China Kimataifa kila la kheri na mafanikio mema kazini, pamoja na kuijenga vyema CRI.

    Ahsante sana Bwana Stephen Magoye Kumalija kwa barua yako kuhusu kumpongeza rais wa kampuni ya kutengeneza magari ya kijapani Bwana Hakiyo Toyoda, kweli hicho ni kitendo cha uungwana sana, na tunatoa wito kwa viongozi wote kwamba yanapotokea makosa basi wawe wepesi kukiri na kufanya juhudi ya kuyarekebisha. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako