• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji 0921

    (GMT+08:00) 2010-09-21 17:52:23

    Msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie wa S.L.P 601 Maragua Kenya anasema kwanza salamu zangu ziwafikie watangazaji na wasimamizi wote wa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa. Naomba kuchukua fursa hii ili kuwapa pongezi kwa juhudi zenu za kutupeperushia kipindi chetu cha kuwa nasi jifunze Kichina, huku nikiendelea kufahamu na kupata uzoefu wa kutamka maneno kadhaa ya Kichina, kuna baadhi ya herufi ya kusaidia kutamka maneno ya Kichina ambazo hunitatiza sana kuzitamka kama vile qi, xi, zha, le, na an.

    Kwa mfano wakati nilipoanza kujifunza Kichina kupitia kwenye kipindi chetu cha kuwa nasi jifunze Kichina maneno qing nilisikia yakitamkwa ching na neno xiexie ambalo maana yake ni ahsante nilisikia kama shieshie. Ombi langu ni kuwa kama kuna uwezekeno mnitumie jarida la kuwa nasi jifunze Kichina, ili nipate urahisi wa kujifunza Kichina. Vilevile kama kuna uwezekano mtuandalie shindano la chemsha bongo linalohusiana na kipindi chetu cha kuwa nasi jifunze Kichina ili wasikilizaji wapate fursa nzuri ya kufuatilia kipindi hiki kwa makini, vilevile naomba kuwasilisha shairi ambalo linaelezea kuhusu kujifunza Kichina.

    KUWA NASI JIFUNZE KICHINA

    Kuanzia maneno ya kusalimiana, hadi maneno ya kuagana

    Vijana kwa wazee, sote twajikakamua

    Twapinda na kupindua ndimi, huku tukipata uzoefu

    Lipi la kisasa, kuliko kujifunza kichina.

    Tujifahamishe vizuri, na lugha ya kichina

    Aghalabu vipindi teletele, kujifunza kupitia kwenye redio

    Lugha ya Kichina, tunaimani na kufurahia

    Lipi la kisasa, kuliko kujifunza kichina.

    Kutojua Kichina, ni kosa kubwa nanena

    Sentesi mia tisa za Kichina, twatarajia kunufaika

    Usikilizaji wetu ni faida, kichina twajivunia

    Lipi la kisasa, kuliko kujifunza kichina.

    Ahsante huku nikizidi kufuatilia matangazo na vipindi vya idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa, nashangaa kwani kipindi cha mbinu 39 za kivita za China hatupati siku hizi, kwani kiliondolewa kwenye orodha ya vipindi. Mbali na hayo nilipata fursa nzuri ya kujifunza baadhi ya mbinu 39 za kivita za China kama vile-:

    Kupiga kijembe, kupiga majani na kumshtua nyoka, mtego wa mrembo, kufanya mti uchanue maua na kuondoa ngazi baada ya kupanda kwenye chumba kilichopo ghorofani. Namalizia hapa kwa leo, Ahsanteni.

    Tunakushukuru sana Bwana Philip Ng'ang'a Kiarie kwa barua yako hasa shairi ulilotutumia ambalo ni zuri na linavutia sana, kwakweli sisi tunafurahishwa mno na juhudi unazochukua za kujifunza kichina, hivyo kuhusu suala la kutumiwa kitabu cha kuwa nasi jifunze Kichina usiwe na wasiwasi, tutakutumia kwani tumeshachapisha kitabu na ndani yake kuna cd ambapo utapata kujua pia namna ya kutamka maneno vizuri, ahsante sana.

    Msikilizaji wetu Ally Omar Seif wa Mlindo Pandani S.L.P 114, Wete Pemba Tanzania, anasema salamu nyingi sana, na natumai kuwa muwazima wa afya kabisa mkiendelea na kazi zenu za ujenzi wa taifa. Katika kipindi cha mwaka 2009, vipindi mbalimbali vya redio China Kimataifa vilitangazwa, katika mwaka huo nilifurahia ziara ya rais wa China Bwana Hu Jintao aliyoifanya hapa Tanzania. Katika ziara yake hiyo nilifurahishwa na hotuba yake ambayo alizungumza kwa lugha ya Kichina alipokuwa akiufungua uwanja wa taifa wa Dar es salaama, alisema kuwa ataendelea kuzisaidia nchi za bara la Afrika mpaka ziondokane na umasikini.

    Vilevile kwa kuisikiliza redio China au CRI kilichonivutia zaidi ni mkutano uliofanyika Sham el Sheikh, Misri tarehe 8 Novemba mwaka 2009, ambapo waziri mkuu wa China alisema kuwa nchi za Afrika ni lazima azisamehe madeni yake yanayodaiwa na nchi yake, kwakweli viongozi wa China ni viongozi wenye imani na ndugu zao wa Afrika, jambo ambalo mataifa ya magharibi hawalitaki, ahsanteni sana viongozi wa China kwa misaada yenu hiyo.

    Kwa kuimarisha vipindi natoa mapendekezo kuwa pawepo na kipindi cha yaliyopita ni dhahabu, licha ya kuomba kipindi hicho nimewaandalia mchezo wa kuigiza, mimi na CRI na mchezo huu nimeshaurikodi katika kaseti nikitumai mtaupenda, mwisho naomba kadi za salamu, kitabu cha kuwa nasi jifunze Kichina, na nawatakia kila la kheri watangazaji wote wa CRI.

    Kwanza kabisa tunapenda kukushukuru msikilizaji wetu Ally Omar Seif kwa maoni yako, kwa kweli China ni nchi ambayo inajitahidi sana kuzisaidia nchi mbalimbali za Afrika tokea kuanzishwa kwa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika na kabla ya hapo. China mpaka sasa imetekeleza ahadi nyingi tu ilizotoa kwa Afrika na ushirikiano huu umepiga hatua kubwa kabisa, hususan China imeanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali katika bara la Afrika. Miradi hii ni ya kunufaisha pande zote mbili, mfano mzuri tu ni hivi karibuni ulipoibuka msukosuko wa fedha, China bila ya kujali chochote ilizisaidia nchi za Afrika na kuendelea na utekelezaji wake wa hatua nane zilizotolewa katika mkutano wa baraza la ushirikiano, kuhusu kipindi cha yaliyopita ni dhahabu, kwanza tunajadiliana na uongozi baadae tutakupa jibu kama tutaweza kuanzisha au la.

    Na sasa ni barua ya Bwana Stephen Magoye Kumalija wa Kahama Shinyanga Tanzania anasema ni dhahiri shahiri kuwa hamjambo wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa, mimi ni mzima wa afya njema na ninaendelea kila siku kufuatilia matangazo yote ya redio China kimataifa.

    Awali ya hayo naomba kutumia wasaa huu kuwauliza wananchi wa Tanzania kuwa jee tunaelekea wapi? Ambapo hivi karibuni kimefanywa kitendo cha kinyama kwa kuwauwa kikatili watoto, kinamama na wanafunzi wa shule wapatao 17 huko katika kijiji cha Mahale ambapo waliuwawa na watu wasiojulikana, tena wote ni wa familia moja. Vilevile mwanzoni mwa mwaka katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza watu wapatao 12 waliuawa na majambazi kwa kumiminiwa risasi ambapo watu hao walikuwa ni wavuvi na wengine ni wachuuzi wa samaki.

    Hivyo basi naomba uongozi wote wa jeshi la polisi pamoja na serikali na wananchi wote wa Tanzania, wafanye kazi ili watu wanaofanya vitendo hivyo viovu na vya kikatili wasakwe na kukamatwa ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua kali mno, kwani viongozi wetu wa serikali ya Tanzania msipofanya hivyo, hapo baadae vitendo hivyo vya kinyama vitazidi na kuhatarisha maisha ya jamii hapa nchini Tanzania. Mwisho nawatakia wafanyakazi wote wa redio China kimataifa kazi njema na yenye mafanikio mema katika mwaka huu wa 2010.

    Ahsante sana Bwana Stephen Magoye Kumalija kwa barua yako, kwanza tunapenda kutoa pole kwa familia zote zilizokumbwa na mkasa huo. Kwakweli inasikitisha sana kuona vitendo viovu kama hivyo vinashamiri katika jamii hasa ya Tanzania, jambo muhimu ni kushirikiana kati ya vyombo vya dola na wananchi na kuhakikisha unyama huo unaondolewa kabisa kwenye jamii ili wananchi waweze kuishi kwa amani na utulivu. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako