• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mchoraji mashuhuri wa Brazil awaletea furaha watoto wa sehemu zilizokubwa na maafa za mkoani Sichuan kwa michoro yake ya karagosi

    (GMT+08:00) 2010-09-30 14:19:33

    Msichana Yang Haoxiao mwenye umri wa miaka 11 ni mwanafunzi wa darasa la tano wa shule ya msingi huko Yaan mkoani Sichuan. Mwanzoni mwa mwezi Septemba, yeye pamoja na watoto wengine 28 kutoka mkoa wa Sichuan na mjini Shanghai, walikusanyika kwa furaha katika Jumba la Brazil kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai, na kujifunza kuchora picha za karagosi kutoka kwa mchoraji mashuhuri wa Brazil Bw. Mauricio de Sousa.

    Tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mwaka 2008 huko Wenchuan liliiharibu vibaya shule aliyosoma msichana Yang Haoxiao. Kampuni ya Vale do Rio Doce (CVRD) ya Brazil ilitoa dola za kimarekani laki 4 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule 3 za msingi zilizoko katika miji ya Ya'an, Guangyuan na Liangshanzhou mkoani Sichuan, ikiwemo shule anayosoma Yang Haoxiao. Siku hiyo wajumbe wa walimu na wanafunzi wa shule hizo tatu walikwenda kutembelea kwa furaha Jumba la Brazil kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai na kushiriki kwenye shughuli za kuchora picha pamoja na Bw. Mauricio.

    Alipozungumzia safari hii ya kuwaleta wanafunzi kutembelea maonesho ya kimataifa ya Shanghai, Mwalimu wa shule ya msingi ya matumaini ya Vale do Rio Doce ya mji wa Guangyuan mkoani Sichuan alisema,

    "Kwanza tunaishukuru sana kampuni ya CVRD kwa kutoa vifaa vingi vya kufundishia kwenye shule yetu, kutujengea upya majengo ya shule, na pia kutupatia mabegi ya shule na nguo. Tunafurahi zaidi na kuishukuru kampuni hii kwa kutuwezesha kuja kutembelea kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai."

    Kwenye Jumba la Brazil, mchoraji mashuhuri wa picha za karagosi wa Brazil Bw. Mauricio anawafundisha watoto wa shule hizo namna ya kuchora katuni, pia anatazama pamoja nao katuni iliyotengenezwa kwa mujibu wa sura ya "Monica", ambayo imebuniwa naye. Baadaye Bw. Mauricio aliwapa watoto vitabu vya katuni na wanasesere, na watoto nao walimpa Bw. Mauricio zawadi maalum—utarizi wa mtindo wa msalaba wa panda wa mkoa wa Sichuan.

    Bw. Mauricio ni mchoraji maarufu wa picha za karagosi nchini Brazil, pia ni mtengenezaji wa filamu za katuni. Anaongoza kikundi chenye wasanii zaidi ya 150, ambacho kinashughulikia mambo mbalimbali ya kiutamadunia yakiwemo uchapishaji, katuni na tovuti. Vitabu vyake zaidi ya bilioni 1 vinauzwa duniani, na vimetafsiriwa kwa lugha zaidi ya 50 ikiwemo lugha ya Kichina. Amebuni zaidi ya sura 200 zinazovutia za wahusika katika katuni, kama vile "Monica", "Pelezinho" na "Ronaldinho".

    Akimzungumzia "Monica", Bw. Mauricio alisema ana matumaini kuwa sura hiyo ya katuni italeta furaha kwa watoto wa China. Alisema,

    "Tumebuni sura ya Monica kwa watoto, kwa kuwa tunataka kuwaeleza watu kuwa furaha haina mpaka, na watu wanaweza kuwa na furaha bila kujali umri wala utamaduni wao. Nadhani watoto wa China watampenda Monica kutoka Brazil. Leo watoto wamekusanyika hapa kujifunza kuchora picha za katuni, nadhani watajifunza mambo mengi zaidi kwenye maonesho ya kimataifa."

     

    Ni mara ya kwanza kwa msichana Yang Haoxiao kwenda mji wa Shanghai, pia ni mara yake ya kwanza kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa. Kwenye shughuli ya kuchora picha pamoja na Bw. Mauricio, Yang Haoxiao alibuni sura ya Haibao palepale, lakini hakuridhika na ubunifu wake. Lakini alimpenda sana Bw. Mauricio, alisema,

    "Mjomba Mauricio ni mpole, na ni rahisi kuwasiliana naye."

    Baada ya kuwa pamoja na watoto hao alasiri nzima, Bw. Mauricio aliona kuwa watoto wa China wanapendeza sana. Kuhusu uchungu ulioletwa na tetemeko la ardhi, Bw. Mauricio aliona kuwa, watoto wanaweza kuondokana na uchungu haraka, na picha za karagosi pia inaweza kuwasaidia kuondoa uchungu huo. Alisema,

    "Watoto wanaweza kuondokana na uchungu haraka, hivi sasa wanataka kuishi kwa furaha. Ili waweze kushinda masikitiko, katuni inaleta furaha kwao, na furaha hiyo itakuwa pamoja nao katika maisha yao yote."

    Bw. Mauricio ana watoto kumi, na sura nyingi za katuni zinazopendeza alizibuni kutokana na sura za watoto wake. Anafuatilia kwa makini maisha ya watoto, na anaona kuwa kuwaelimisha watoto kupitia burudani kunawawezesha watoto hao kujifunza ujuzi wa maisha katika hali yenye furaha, ambapo wanaweza kupata pia tabia nzuri. Bw. Mauricio anatoa mchango mkubwa katika kuwaelimisha watoto kupitia uchoraji wake wa picha za karagosi.

    Alipozungumzia ushirikiano kati ya Brazil na China katika mambo ya katuni, Bw. Mauricio alifurahia sana uhusiano huo na kuona kuwa kuna haja ya kubuni sura ya "Monica kutembelea maonesho ya kimataifa", alisema,

    "Bila shaka teknolojia ya China katika uchoraji wa picha za karagosi imekuwa ya hali ya juu, na Brazil na China kushirikiana kutengeneza filamu za katuni ni hatua inayozinufaisha nchi hizo mbili, tunajadiliana na China kuhusu mambo hayo."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako