• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maisha mazuri ya walioacha mazoea ya kutumia dawa za kulevya kwenye "makazi ya Yulu"

    (GMT+08:00) 2010-10-14 15:49:28

    Katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahani na kabila la Wayi wa Honghe ulioko kusini magharibi mwa China, kuna mji mdogo unaoitwa Kaiyuan, na "Makazi ya Yulu" ni moja kati ya makazi 19 mjini humo. Tofauti na makazi mengine, watu karibu 600 waliowahi kutumia dawa za kulevya wanaishi katika makazi ya Yulu kwa hiari baada ya kuacha kutumia dawa hizo. Katika makazi hayo misaada mbalimbali hutolewa, misaada hiyo ni pamoja na kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya kuacha kabisa mazoea hayo, kuwapatia matibabu pamoja na ajira, ili watu hao waweze kuishi vizuri zaidi baada ya kurudi kwenye jamii.

    Bw. Xu Yunhui ana umri wa miaka 33, anaishi katika "makazi ya Yulu" kwa hiari baada kukamatwa kwa mara ya 8 kwa kosa la kutumia mihadarati na kulazimishwa kuacha. Anasema kuwa sasa anathamini sana mapumziko baada ya kazi,

    "Katika eneo hilo la makazi, tunaweza kuwa na shughuli nyingi za kufanya, na maingiliano ya watu pia ni mengi, licha ya hayo kuna baadhi ya majengo ya burudani. Baada ya kazi tunaweza kutazama televisheni, au kucheza mahjong na michezo mingine na wenzetu."

    Mkoa unaojiendesha wa Honghe ni maskani ya Bw. Xu Yunhui. Kutokana na hali yake ya kijiografia, mkoa huo uliathiriwa vibaya kwa kushamiri kwa mihadarati duniani katika miaka ya 80 ya karne iliyopita. Wakati huo Bw. Xu Yunhui alikuwa na umri mdogo, na hakujua mengi kuhusu dawa za kulevya alipoanza kuzitumia. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa alianza kutumia dawa za kulevya mwaka 1993, na alilazimishwa kuacha dawa hizo mara 8 bila mafanikio. Kadiri siku zilivyozidi kupita, ndivyo alivyozidi kukata tamaa ya maisha. Baada ya kuhamia kwenye "makazi ya Yulu", ndipo akahisi tena uzuri wa maisha.

    "Makazi ya Yulu" licha ya kuwa na nyumba zenye kodi ndogo, bwalo lenye uwezo wa kujaa watu zaidi ya 100, na kliniki inayotoa huduma za matibabu kwa saa 24, pia yana maktaba, sehemu ya kunyoa nywele na maduka. Vilevile makazi hayo yanatoa mafunzo ya ufundi na nafasi za ajira kwa wakazi wa hapo. Wakazi wa hapo wanaweza kuchagua kujifunza ufundi fulani kutokana na hali zao halisi. Kwa mfano watu ambao hawana ufundi wa sanaa za mikono wanaweza kuchagua kushiriki kwenye miradi ya kilimo na ufugaji, na watu ambao ni hodari wa maonesho ya usanii wameunda kikundi cha wasanii cha Yulu, na wanafanya maonesho kwa ajili ya kuielimisha jamii juu ya madhara ya kutumia mihadarati. Hivi sasa kila mkazi katika makazi hayo ameajiriwa, na mshahara wa chini zaidi kwa mwezi umefikia Yuan 600, na wale wenye mapato madogo pia wanaweza kuomba ruzuku ya kuhakikisha maisha ya kimsingi.

    "Makazi ya Yulu" yana lengo la kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya kuacha kabisa mazoea hayo, na kuwawezesha kurejea katika familia zao na kuishi katika upendo na watu wa familia. Jamaa wa wakazi wa hapa wanaweza kuja kuwatembelea wakati wowote. Hivi karibuni binti wa Bw. Xu Yunhui mwenye umri wa miaka minane alikwenda kumtembelea, na kusema "baba, usitumie tena mihadarati." Maneno hayo ya binti yake yalimgusia sana. Baada ya kupewa mafunzo, hivi sasa Bw. Xu Yunhui amezoea kazi ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi, na ameamua kutoishi kama zamani. Alisema,

    "Nimehamia kwenye makazi hayo kwa miezi 7, safari zilizopita nilishindwa kabisa kuacha kutumia mihadarati baada ya kulazimishwa. Lakini hivi sasa naamini kuwa maisha yangu ya siku za baadaye yatakuwa mazuri."

    Baada ya muda wa kuishi kwa hiari kwenye "makazi ya Yulu" kutimia, Bw. Xu Yunhui anataka kwenda kufanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi mkoani Guangdong. Anasema anataka kuwasaidia jamaa zake kuwa na maisha mazuri kwa kutegemea mikono yake.

    Tofauti na Bw. Xu Yunhui, Bw. Zhuang Yisheng ameishi kwenye makazi hayo kwa zaidi ya mwaka mmoja, na anapenda kuendelea kuishi hapo. Baada ya kuona mabadiliko makubwa ya Bw. Zhuang Yisheng, dada yake mkubwa Zhuang Ning alilia na kusema,

    "Baada ya kuanza kutumia dawa za kulevya, kaka yangu mdogo alianza wizi, na aliiba vitu vyote vya thamani vilivyokuwa nyumbani. Lakini baada ya kuishi kwenye makazi ya Yulu, amebadilika kabisa. Kila mara tunapomtembelea, tunaona amenenepa na amekuwa mkarimu, na kazi yake katika makazi hayo pia ni nzuri."

    Mkuu wa idara ya kulinda usalama wa umma ya mji wa Kaiyuan Bw. Zhao Yunfeng ndiye aliyetoa wazo la kujenga "makazi ya Yulu". Anasema watumiaji wa dawa za kulevya sio tu ni watu wanaokiuka sheria, bali pia wamekuwa watu wanaodhuriwa na wagonjwa, kwa kuzingatia hilo, makazi ya Yulu yamejengwa kwa ajili ya kutoa jukwaa kwa watu hao ambao hawataki au hawana uwezo wa kurudi kwenye jamii baada ya kulazimishwa kuacha mihadarati.

    Toka "makazi ya Yulu" yaanzishwe mwaka 2006, idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya wanaoacha matumizi ya dawa hizo, na kurudi kwenye jamii imefikia zaidi ya 1,300. Watu hao wamekuwa na ufundi, ambao unawawezesha kupata ajira mwafaka na kuhakikisha wanaweza kuishi maisha ya kawaida baada ya kurudi kwenye jamii.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako