• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji

    (GMT+08:00) 2010-11-02 16:32:19

    Msikilizaji wetu Franz Manko Ngogo mwenye anuani ya barua pepe rasmanko2003@yahoo.com anasema, ndg. Wa CRI, shukrani zangu ziwafikie hapo Beijing. Nachukua wasaa huu kuwapongezeni kwa hatua yenu ya maendeleo mliyoonesha. Kweli, "kimya kingi kina mshindo mkuu" zawadi za televisheni kwa washindi wa kwanza, cherehani kwa washindi wa pili na kifuta jasho cha redio kwa washindi wa tatu ni kitu cha kujivunia. Kukutana na wasikilizaji wengine wenye tabia na mawazo ya aina moja ya kusikiliza CRI, ambao walikusanyika katika ubalozi wa China nikiwemo mimi pamoja na wasikilizaji wanachama 10 wa KEMOGEMBA Club ambao walichoma nauli zao kutoka Tarime hadi Dar bila kujali watapata nini. Hakika ni jambo la kujivunia kuwa na mambo ya kutia moyo kama haya. Mola awatie nguvu.

    Sasa ni barua ya msikilizaji wetu Mchana John Mchana wa Morogoro Tanzania naye pia ametutumia barua pepe yenye anuani mchanajo@yahoo.com akisema leo napenda kuwashukuru wale wote walio shughulikia mipango yote ya sherehe iliyo fanikiwa huko Dar es salamu kwa kiasi kikubwa. Pia shukrani ziwafikie watangazaji na wakurugenzi wote wa radio shiriki na washindi wa chemsha bongo. Nina furaha tele hapanilipo kwani furaha yangu kubwa ni kukutanishwa na wasikilizaji wa mikoa mbali mbali, kwani tulikuwa tunashiriki kwenye vipindi mbali mbali ila kwa sura tulikuwa hatujuani lakini kwa kuwa redio China mara nyingi inafanya mambo ambayo ni ya msingi imetukutanisha kupitia chemsha bongo. Kwa hilo hakuna kama radio china. kama hiyo haitoshi wamenikutanisha na jamaa yangu na mtangazaji wa KBC jakobo Magoha kwa sasa ni mtangazaji wa radio china kimataifa.

    Pia maelezo ya mkurugezi wa radio china kimataifa wakati akihojiwa na TBC yalinifurahisha sana. kwa kifupi Tanzania naomba ikubali uanzishwaji wa uashirikiano wa vipindi vya CRI na TBC. waache hofu ombi kwa wasikilizaji baada ya kupata zawadi tusibweteke tufungue ukurasa mpya, tuwe na kasi ya aina yake tuipe ushirikiano CRI kwa moyo wetu wote na nguvu zetu zote, waswahili walinena akupendae naye mpende.

    Shukrani za dhati wasikilizaji wetu Franz Manko Ngogo na Mchana John Mchana kwa barua zenu, kwa kweli nasi pia tumefurahi, kwani licha ya wawakilishi wetu waliokuja Tanzania kwenye sherehe za kutoa tuzo kuonana na wasikilizaji wetu mbalimbali, hata na sisi pia tumeweza kuonana na wasikilizaji wetu ambao wamepata tuzo ya nafasi maalumu na kuja kutembelea China. Tumeweza kubadilishana nao maoni na kuwafahamu zaidi. Sisi tunawaomba muongeze bidii zaidi ya kushiriki kwenye chemsha bongo zetu kwani ni njia pekee ya kuweza kuonana uso kwa kwa uso pale inapofika wakati wa sherehe ya kutoa tuzo au kwa wale wanaokuja China. Ahsante sana.

    Ni barua yake Bwana Philip Ng'ang'a Kiarie wa S.L.P 601 Maragua Kenya, anasema kwanza salamu zangu ziwaendee watangazaji na wasimamizi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa. Pili nachukua fursa hii kuutakia mji wa Shanghai kila la kheri katika maonesho yake ya kimataifa, shukrani za dhati ziwafikie watangazaji na wasimamizi wa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa kwa kutuandalia shindano la chemsha bongo kuhusu "tukutane Shanghai" nilifurahi kwa kufahamu jinsi maonesho ya awamu ya 41 yanavyofanyika huko Shanghai China.

    Hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa maonesho ya kimataifa kufanyika kwenye nchi inayoendelea tangu maonesho ya kwanza yafanyike miaka 159 iliyopita. Kwa hakika watu waliotembelea huko Shanghai wamejionea majumba mbalimbali ya maonesho yenye sifa na mitindo tafauti inayovutia macho. Mbali na hayo nchi zilizoshiriki zimepata fursa nzuri ya kufanya biashara na kujifunza mambo mbalimbali.

    Nakubaliana kabisa na kauli mbiu ya maonesho hayo ambayo ni "miji bora, maisha bora" ili kutafsiri vizuri kauli mbiu hiyo limejengwa jumba la tafsiri ya kauli mbiu ili kujadili uhusiano kati miji na binaadamu na maisha na uhusiano kati ya dunia na maisha ya mbele, la kutia moyo ni kwamba maonesho hayo pia ni sehemu inayoonesha uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, aidha kwenye maonesho hayo yameoneshwa matunda mapya ya sayansi na teknolojia na hali ya kutotoa hewa inayochafua mazingira, ambapo matumizi ya nishati na maji ndani ya majengo yote kwenye eneo la maonesho yanadhibitiwa, na nishati ya jua na zana na vifaa endelevu vinatumiwa kwenye majengo hayo. Namalizia barua yangu nikiwa na matumaini ya kuendelea kusikiliza na kuiandikia barua Idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa.

    Tunakushukuru sana Bwana Philip Ng'ang'a Kiarie kwa barua yako kuhusu maonesho ya kimataifa, tarehe 31 Olktoba maonesho yamemalizika lakini maonesho ya kimataifa ya Shanghai yamepata mafanikio makubwa kabisa hasa kwa kupokea watalii wengi zaidi kuliko ilivyotarajiwa waliotembelea kwenye maonesho hayo, pia uvumbuzi wa aina mbalimbali umeoneshwa kwenye maonesho hayo, kwa kweli ni maonesho ya kupigiwa mfano. Ahsante sana.

    Barua ya mwisho inatoka kwa msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa S.L.P 161 Bariadi Shinyanga Tanzania, anasema salamu nyingi sana kutoka kwangu hapa Tanzania mzipokee, napenda kuwaeleza kwamba nilivutiwa sana na matangazo yenu ya tarehe 13 Aprili mwaka huu, baada ya taarifa ya habari kukamilika, tuliletewa maelezo baada ya habari yaliyosomwa na mtangazaji Han Mei na Shie Yi, ambapo walizungumzia mkutano uliohusu silaha za nyuklia, mkutano huo muhimu ulifanyika mjini Washington D.C tarehe 13 Aprili mwaka huu ulihudhuriwa na rais Hu Jintao wa China na rais Barack Obama wa Marekani na viongozi wengine kutoka nchi 47 duniani pia wamehudhuria.

    Ni jambo la faraja na matumaini makubwa kwamba viongozi hao mashuhuri wameshaiona hatari ya kuenea silaha za nyuklia ndio maana wakaona umuhimu wa kuwa na ajenda ya suala hilo na kujadili kwa kina. Ni ukweli wa mambo kuwa suala la nyuklia ni suala nyeti sana kuhusu mustakabali wa suala la usalama duniani. Lazima tutambue kwamba binadamu wote ni sawa hivyo ni lazima pia kuthamini, kuheshimi na kulinda maisha ya viumbe na binaadamu na viumbe vingine dhidi ya mashambulizi ya makombora ya nyuklia na silaha nyingine za maangamizi. Ni ukweli ulio wazi kuwa dunia inaendelea na binadamu wanavumbua teknolojia na sayansi mpya kila mara, jambo jema sana, lakini tunapaswa kufikiri mara mbili na kujiuliza ulazima wa kurundika silaha za nyuklia kila sehemu bila kujiuliza mantiki yake.

    Upunguzaji na udhibiti wa silaha za nyuklia ni hoja na ajenda ya msingi sana inayopaswa kuzingatiwa na watu wote wapendao amani, usalama na maendeleo katika dunia nzima. Hivyo basi amani ya dunia ilindwe wakati wowote mahali popote na kwa gharama yoyote bila kusita. Mipango na vitendo vyovyote vyenye nia ya kigaidi lazima vizuiwe kwa nguvu zote, sambamba na hilo silaha za nyuklia zisiangukie mikononi mwa watu hatari wasio na huruma hata kwa watu wasio na makosa wakiwemo wanawake wema na watoto.

    Binadamu wote wenye dini, makabila na mataifa tofauti bila kujali rangi na itikadi zetu na hisia zetu, utashi na vitendo vyetu vijikite zaidi katika kutenda mema, kuwapenda binadamu wenzetu, kuwahurumia na kuwasaidia badala ya kufikiria kufanya hujuma, ukatili unaoambatana na ugaidi. Kila mmoja atimize wajibu wake kwa uadilifu na kutenda mema ipasavyo katika maisha yetu yote.

    Mimi napenda sana amani, umoja na mshikamano siyo tu kwa nchi yangu Tanzania au kwa China lakini kwa mataifa yote duniani, huo ni mtizamo na msimamo wangu wa jana, leo na siku zote. Napenda dunia yetu iwe huru dhidi ya tishio la silaha za nyuklia. Kwasababu hii tunawashukuru na kuwapongeza sana viongozi hao mashuhuri rais Hu Jintao na Barack Obama na viongozi wengine kutoka nchi 47 duniani. Tunawashukuru sana na tunaomba jitihada hizo ziendelee mbele. Ahsanteni sana

    Nasi tunakushukuru sana msikilizaji wetu Kilulu Kulwa kwa barua yako kuhusu mkutano wa silaha za nyuklia, sisi tunaungana nawe na tukiwa kama chombo cha habari hatutasita kuhamasisha watu mbalimbali waachane na matumizi mabaya ya nyuklia kwani nyuklia ikitumika vizuri ina manufaa makubwa sana. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako