• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • "Kituo cha kuhudumia wazee" mjini Yantai

    (GMT+08:00) 2010-11-04 15:50:23

    "Nashiriki katika shughuli mbalimbali kama vile kucheza dansi, kucheza ngoma ya Yangge, kuimba, na kuiga wanamitindo. Hivi sasa ninacheza ngoma ya vijiti nyumbani."

    Huyo ni bibi Zhang Yuhua mwenye umri wa zaidi ya miaka 80, na anaishi katika kituo cha kuhudumia wazee mjini Yantai. Kituo hicho kiko katika wilaya ya Laishan, inazungukwa na milima katika pande tatu, na upande mmoja unatazamana na bahari.

    Mkurugenzi wa kituo hicho Bw. Yu Yongjun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, wana mpango kamili ambao utawawezesha kuwatunza wazee hao kwa kuwapa huduma za matibabu, burudani pamoja na mapumziko, ikiwa ni aina mpya na ya kisasa katika utoaji wa huduma kwa jamii. Bw. Yu alisema,

    "Mwaka 2000 tulipata kitambulisho cha viwango vya kimataifa ya ISO 9001. Tuna mpango kamili wa kazi, na tunawataka wafanyakazi wetu watoe huduma mbalimbali zikiwemo matibabu, matunzo, huduma za kiroho, na burudani. Na wanatakiwa kutoa huduma hizo kwa moyo wa dhati, na kuwachukulia wazee hao kama wazazi wao."

    Bw. Yu Yongjun alisema kituo cha kuwahudumia wazee mjini Yantai kilianzishwa mwaka 2007, na hadi sasa idadi ya wazee wanaoishi katika kituo hicho imezidi 440. Bw. Yu alifahamisha kuwa, katika kituo hicho kuna wazee kutoka Yantai na sehemu mbalimbali nchini China. Wazee hao wanaona kuwa hali ya hewa, mazingira na hali ya kuishi mjini Yantai ni nzuri, hivyo nao wanakwenda Yantai kupumzika wakati wa majira ya joto, na kurudi maskani yao wakati wa majira ya baridi.

    Katika kituo cha kuwahudumia wazee mjini Yantai, mwandishi wetu wa habari aliwakuta bibi Liu Jin na mumewe, ambao wanatoka Beijing. Alipoulizwa sababu ya kuchagua kuishi Yantai kwa muda uliobaki wa maisha yao, bibi Liu alisema,

    "Marafiki zetu wawili walitujulisha kituo hiki, kwa kuwa walikaa hapa mwaka jana wakati wa majira ya baridi. Walisema mazingira na huduma zinazotolewa hapa ni nzuri, na chakula cha hapa kinafaa kwa wazee, kwa sababu kinatiwa chumvi na mafuta kidogo. Sisi tunakaribia kutimiza umri wa miaka 80, na tunatafuta mahali ambapo afya zetu zitaangaliwa vizuri, hivyo tulipoambiwa kituo hicho tuliamua kuja hapa."

    Ingawa mwanzoni bibi Liu na mumewe walikuja kutokana na kusikia sifa ya mahali hapo, lakini baada ya kuishi, bibi Liu alisema kituo hicho kweli ni kizuri, na uzuri wake sio tu katika mandhari ya sehemu kilipo, bali wafanyakazi katika kituo hicho wanatoa huduma nzuri, hivyo yeye na mumewe wameipenda sana sehemu hiyo. Bibi Liu alisema,

    "Kwanza mazingira ya hapa ni mazuri, kwani kituo hiki kiko katikati, kimezungukwa na milima kwa pande tatu. Pili huduma zinazotolewa na wafanyakazi wa hapa ni nzuri. Tunaona kama tuko nyumbani, tunajisikia ukunjufu sana wakati wa chakula wasichana hawa wanapotuita babu na bibi. Vilevile vyumba viko katika mpangilio mzuri na ni visafi. Tunaona furaha kukaa hapa, hapa kweli ni pazuri."

    Mume wa bibi Liu Jin babu Hua Jun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika kituo cha kuwahudumia wazee mjini Yantai, anapata huduma nzuri sana. Alisema wazee wanaokaa hapo hawana haja ya kufikiria kuhusu kufua, kupika, wala hawatakiwi kufikiria kuhusu maji, umeme na gesi, wanachotakiwa kufanya kila siku ni kuwa wachangamfu na kuishi vizuri wakiwa na afya.

    Babu Hua alisema, hapo ni mahali pa furaha kwa wazee, kwani hawaoni upweke, bali wanaishi kwa furaha. Babu Hua alisema,

    "Suala kubwa linalowasumbua wazee ni upweke, wanataka kuzungumza na watu wengine. Wanataka watoto wao wawatembelee mara kwa mara, lakini watoto wao wana shughuli nyingi, hivyo kwa kuishi hapa suala hili limetatuliwa. Hapa wafanyakazi wamepangilia vizuri maisha ya wazee. Usiku tunaweza kuzungumza pamoja, au kutembea, hatuoni upweke."

    Bibi Liu alisema, baada ya kukaa hapo kwa muda mfupi na kuchunguza maisha ya kwenye kituo hicho, wameamua kukaa hapo kwa muda fulani kila mwaka, na baada ya kuzeeka kidogo, wataishi hapo muda wote uliobaki wa maisha yao.

    Bibi Liu alisema maneno hayatoshi kueleza upendo wake kwa kituo hicho, hivyo alitunga shairi kueleza hisia yake. Alisema:

    "Nimekaa katikati ambapo pande tatu zinazungukwa na milima, maua yanachanua na ujia unanukia, ndege wanaimba na samaki wanacheza majini, wazee wanaishi hapa pamoja kwa furaha."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako