• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji

    (GMT+08:00) 2010-11-26 17:34:07

    Msikilizaji wetu Lenusi kingalu wa S.L.P 24 Kihonda Morogoro Tanzania, ametuletea baruapepe akisema kutokana na matangazo ya tarehe 4/10/2010 yaliyohusu msitu wa mianzi, habari hii imenivutia sana, kwani nilikuwa najiona kama nipo kwenye mazingira yenyewe wakati kipindi kilipokuwa kinarushwa, namna kilivyonogeshwa na waandaaji, msitu huo ambao una vinjia vilivyomwagiwa changarawe, msitu wenye upepo mzuri wa kuvutia, ukubwa wa msitu huo ni kilometa 10,000, hakika serikali imejua kuona umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya asili. Nimesikia kuwa machipukizi ya mianzi yanaliwa, je yanaliwaje? Pia maeneo mengi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nchi mbalimbali hususani Tanzania sasa yanaelekea kuwa jangwa kwa ukame unaotishia kuyakumba maeneo mengi ya dunia, hali ikoje katika hifadhi kama hizo huko china? Ni vyema kuangalia kama kuna vyanzo vya maji katika msitu huo na maeneo mengine ya misitu ili kuhakikisha watu hawaweki makazi karibu na maeneo hayo, kwa hofu ya kukata miti na mianzi kwa matumizi ya kibinadamu kisha maeneo hayo kuwa jangwa baadae. Hongera serikali ya china na watu wake.

    Pia nimesikia habari ya mazungumzo kati ya waziri wa china na wa japan kuhusu visiwa vilivyodaiwa kuwa viko upande wa japan, furaha yangu ni pale niliposikia kuwa wamekubaliana. Hali hii inaonesha kukomaa kwa watu wachina. Inavyoonesha hapo baadae China itakuwa msuluhushi wa migogoro na maeneo tata duniani. Na itapewa jukumu kubwa la dhamana ya mataifa duniani.

    Asante.

    Shukurani za dhati msikilizaji wetu Lenusi kingalu kwa baruapepe yako, ni kweli kama ulivyosema kwenye barua yako kuwa China inajitahidi kutunza mazingira, hasa kuhamasisha watu wasikate miti kwani kama tujuavyo miti mbali ya kusaidia kuepukana na jangwa vilevile inachangia kuleta mvua. Na kuhusu machipukizi ya mianzi ni kweli yanaliwa, na kawaida huwa yanapikwa hayo machipukizi kwani yanakuwa malaini sana ni matamu sana siku ukija China utaonja tu chakula hicho.

    Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah Mbarouk wa S.L.P 52483 Umoja wa falme za Kiarabu, Dubai, anasema ndugu wapendwa ningependa kuchukuwa nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Radio China Kimataifa, kwa uzinduzi wa kituo kimpya cha kurusha matangazo yake ya lugha ya Kihispania kupitia masafa ya kati, yaani AM 1470 huko Mjini Tijuana, Mexico mnamo tarehe 1 mwezi November mwaka huu na kupelekea idadi ya vituo vya urushaji wa matangazo ya Radio China Kimataifa katika nchi za nnje kufikia 50.

    Kwa kweli hayo ni mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano yanayoendelea kuchukuliwa na kituo hichi cha matangazo, ili kukidhi mahitaji na shauku ya mamilioni ya wasikilizaji wake kote Ulimwenguni kupitia lugha mbali mbali. Juhudi hizo zisizosita zinatosha kuwa ushahidi wa mafanikio ya Radio China Kiamataifa katika kipindi cha karibu miaka 70 tangu kuanzishwa kwake , ambapo kilele chake kitafikia mwaka ujao wa 2011.

    Ni matumaini yetu makubwa kwamba mapendekezo yetu tuliyochangia tulipokuwa ziarani nchini China hivi karibuni juu ya kuanzishwa kwa kituo cha kurushia matango ya Kiswahili kupitia mfumo wa FM kwa upande wa Tanzania Bara, hatimaye nayo yataweza kufaulu ili wasikilizaji wenu waweze kunufaika na matangazo yenu kwa usikivu ulio bora zaidi. Ahsanteni sana,

    Tunakushukuru sana Bwana Mbarouk Msabah Mbarouk kwa barua yako, na tunapenda kupokea pongezi ulizotupa kwa kuzindua kituo kipya cha AM 1470 huko Mjini Tijuana, Mexico, kwani hilo ni jukumu kuu la CRI kuhakikisha kuwa inasikika kila pembe ya dunia, na kuhusu kuanzisha kituo cha FM huko Tanzania kwa kweli juhudi bado zinaendelea ili na wasikilizaji wetu wa Tanzania nao waweze kufaidika na matangazo yetu tunawaomba wasikilizaji wetu wavute subira.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako