• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kuonja chai maarufu katika jumba la makumbusho la chai

    (GMT+08:00) 2010-12-23 18:50:12

    Katika shamba moja la michai, kando ya ziwa Xihu, mjini Hangzhou mkoani Zhejiang, China, ukienda mbele kwa upande wa magharibi kwa kufuata ziwa Xihu, unaweza kuona shamba moja la michai, kati yake kuna jengo moja nadhifu lenye kuta nyeupe na mapaa ya rangi nyekundu, jengo hili ni jumba la makumbusho la chai nchini China. Mkuu wa jumba hio Bw Wang Jianrong alisema,

    "Jumba letu la makumbusho ya chai lilijengwa mwaka 1991, hadi sasa imepita zaidi ya miaka 20. Vitu muhimu vinavyooneshwa hapa ni kuhusu historia ya chai, utamaduni wa chai, chai na afya ya watu na chai maarufu za China. Licha ya hayo, tunafanya baadhi ya maonesho ya muda kila mwaka. Maonesho ya muda yanayofanyika hivi sasa ni kuhusu mchanga wa rangi ya zambarau, kwenye sehemu kadhaa karibu na mji wa Hangzhou, umegunduliwa mchanga wa rangi ya zambarau, ambao ni mali-ghafi nzuri sana ya kutengeneza buli za chai. Kila mwaka tunafanya maonesho ya muda zaidi ya kumi. Hivi sasa idadi ya watu wanaotembelea jumba letu la makumbusho ni kiasi cha laki 5 kwa mwaka, ambao kiasi cha elfu 6 hadi elfu 7 ni watalii kutoka nchi za nje. Kwa sababu chai ni kitu maarufu cha jadi ya China, na ni moja ya alama za utamaduni wa China, kwa hiyo inapendwa sana na watalii kutoka nchi za nje.

    Baada ya kuingia kwenye jumba la makumbusho ya chai, watalii huvutiwa na njia wanayopita. Njia hii imetandikwa vipande vya mawe, ambavyo baadhi yake vina maneno 100 ya Kichina ya chai, yaliyofuatishwa kutoka kwenye maneno yaliyochongwa kwenye vipande vya mawe ya kumbukumbu, na hati na michoro ya watu mashuhuri. Maneno hayo ya kisanaa yanapendeza sana na kuvutia.

    Baada ya kupita katika njia hiyo yenye maua, watu wanaingia kwenye ukumbi wa mwanzo wa maonesho, ambapo watu wanavutiwa na sauti ya mtiririko wa maji. Kumbe ni maji yanayoanguka chini taratibu kutoka kwenye kimo cha mita 10 hivi, neno moja kubwa la "chai" lililo chini kwenye maji linaonekana safi sana na la kuvutia. Chini ya maji hayo kuna vyungu vya maua. Wazo la usanifu huu la kuunganisha kitu kinachotembea, yaani maji yanayotiririka na vitu vilivyotulia kama vyungu vya maua, linaonesha historia ndefu ya utamaduni wa chai wa China, uhusiano kati ya chai na maji, na uhusiano kati ya mazingira ya maumbile na binadamu.

    Maonesho ya utamaduni ya jumba la makumbusho ya chai ni ya kuvutia, ambayo ni kitu muhimu zaidi kwenye jumba hilo la makumbusho. Mkuu wa jumba la makumbusho Bw Wang Jianrong alisema, maonesho yanagawanyika katika sehemu 6 za historia ya Chai ambazo zinaonesha kwa kirefu kuhusu mvutio wa utamaduni wa chai. Alisema:

    "Jumba letu la makumbusho linaonesha historia ya chai, yaani zamani tulikunywa chai kwa namna gani, na chai iligunduliwa namna gani. Kwa sababu China ni sehemu ya chimbuko la chai, na chai iligunduliwa mapema zaidi nchini China, michai iliyoko katika sehemu nyingi za duniani, ilichukuliwa moja kwa moja kutoka China, au kupitia sehemu nyingine, kwa hiyo tunasema, chai ni mchango muhimu uliotolewa na China kwa dunia. Michai maarufu yenye majina yaliyopo nchini China kwa hivi sasa ni zaidi ya aina 1,200, michai maarufu muhimu inayooneshwa kwenye jumba letu la makumbusho ni aina zaidi ya 200. Hivi sasa mnaweza kuonja chai za aina 23 au 30 hivi kwenye jumba letu la makumbusho."

    Kitu kinachovutia watu zaidi ni desturi ya kunywa chai kwenye sehemu mbalimbali za China. Kwa mfano, chai ya samli ya kabila la Watibet, ambapo watazamaji wanaweza kuitengeneza wao wenyewe; chai ya kuokwa ya kabila la Watai, mkoani Yunnan; mgahawa wa chai wa Qixing ulioko kwenye kando ya mto; bendera ya tangazo la biashara inayopeperuka kwenye upepo iliyoko mbele ya duka la chai la mfanyabiashara wa mkoa wa Anhui, vitu hivyo kama vinawarudisha watu mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Kwenye kando ya duka hilo la chai, inaonesha ufundi wa kutengeneza chai ya Gongfu ya Fujian, msichana mmoja anatengeneza chai, miondoko yake ya madaha pamoja na harufu nzuri ya chai vinavutia watu kuangalia. Kiongozi wa kikundi cha utengenezaji wa chai cha jumba la makumbusho, Xu Zemei alisema,

    "Hiki ni kikundi cha utengenezaji wa chai. Wao wanafuata kanuni za utengenezaji wa chai, nilichukua majani ya chai kwa kijiko, kwani majani ya chai kavu ni rahisi kuvunjika. Hiki ni kibanio, kinatumika kushika kikombe wakati kukisafisha, kwa kawaida kinatengenezwa kwa mbao ngumu ikiwemo mpingo."

    Tulipumzika kidogo na kuonja chai maarufu zilizohifadhiwa kwenye jumba la makumbusho ya chai, Bi Xu Zemei alituchagulia aina ya chai ya Dahongpao, huku akisafisha kikombe na kumimina maji ya chai kwa uhodari sana, alituambia kuwa kuna kanuni moja inayofuatwa wakati wa kutengeneza chai, yaani majani ya chai yaliyokomaa zaidi yanahitaji maji moto zaidi: Alisema:

    "Majani ya chai ya Dahongpao ni ya aina ya chai ya Wulong, majani ya chai ni manene na yamekomaa zaidi ikilinganishwa na chai ya rangi ya kijani. Inahitaji kutumia maji ya moto zaidi. Kabla ya kunywa chai, kwanza unatakiwa kuangalia rangi ya maji ya chai, halafu unanusa harufu yake, na mwisho ni kuonja ladha yake."

    Baada ya kunywa chai, tuliendelea na safari hadi kwenye ukumbi wa chai maarufu. Kwenye ukumbi huo yanaoneshwa majani ya chai zaidi ya aina 300 ya makundi 6, watalii wakitumia spika za masikioni wanaweza kusikiliza maelezo ya aina ya chai wanayochagua.

    Kwenye jumba la makumbusho ya chai, kuna sehemu moja iliyopandwa michai maarufu. Hii ni bustani ya michai inayoonesha aina zaidi ya 100 za michai. Wataliii wanaofika huko katika wakati wa kuchuma majani ya chai, wanaweza kuona majani ya chai yakitengenezwa kwenye karakana inayoitwa Peixiangyi, mchakato muhimu wa usindikaji wa majani ya chai unaoneshwa kwa watalii.

    Mbali na hayo, jumba la makumbusho ya chai linatoa mafunzo kuhusu utengenezaji wa chai, watazamaji wanaweza kuchagua mafunzo ya nusu siku au ya muda mrefu zaidi kwa kufuata mambo wanayopenda. Mafunzo hayo yanapendwa sana na watu. Mkuu wa jumba la makumbusho Bw Wang Jianrong alisema, "Zamani watu walioshiriki mafunzo ni watu wanaofanya kazi za chai, lakini hivi sasa watu wa aina mbalimbali wakiwemo waalimu, na wanafunzi wa vyuo vikuu, hayo ni mabadiliko makubwa."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako