• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji

    (GMT+08:00) 2011-01-04 16:06:52

    Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga Tanzania, ametuletea barua akisema nchi na mashirika zaidi ya 240 kutoka sehemu mbalimbali hapa duniani, zilijidhatiti kutumia nafasi adimu ya kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa ya Shanghai, maonesho hayo yalipewa kauli mbiu ya miji bora, maisha bora. Maonesho hayo ya kimataifa yalikuwa na lengo la kutafuta njia ya kupatikana kwa maendeleo ya kudumu katika miji hapa duniani, vilevile kuboresha maisha ya jamii hapa ulimwenguni katika karne hii ya sayansi na teknolojia, inayoendelea kuvumbuliwa kila uchao na wataalmu wa fani pamoja na nynja za kila aina hapa duniani hususan nchini China.

    Kwa mantiki hii maonesho ya kimataifa ya Shanghai yalikuwa ni maonesho ya 41 kufanyika nchini China, na ni mara ya kwanza kufanyika maonesho haya katika nchi hii inayoendelea, ambapo nchi hii ya China ni ya pili kiuchumi duniani baada ya Marekani. Maonesho haya hasa yanahusu uchumi, jamii, sayansi pamoja na teknolojia. Ni dhahiri shahiri kuwa nchi zinazoendelea barani Afrika, zimejidhatiti kutumia nafasi ya maonesho hayo kuweza kuhamasisha miji mbalimbali duniani kufanya juhudi ili ikuwe na iwe bora zaidi, pia ni jambo la faraja kuona kuwa China ilitenga mfuko wenye dola za kimarekani zipatazo milioni mia moja, kwaajili ya kuzisaidia nchi zinazoendelea.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija kwa barua yako, maonesho ya kimataifa hivi sasa yamemalizika, na tunatumai kuwa na wewe pia uliyafurahia, kwani ulibahatika kutembelea maonesho hayo kabla ya kufungwa. Na kwa ujumla maonesho yalifana sana kwani yalivunja rikodi kwa kutembelewa na watu wengi na nchi nyingi kushiriki. Ahsante sana.

    Msikilizaji wetu mwingine ni Philip Ng'an'ga Kiarie wa S.L.P 601 Maragua Kenya anasema kwanza salamu ziwafikie watangazaji na wasimamizi wa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa. Hongereni kwa kazi nzuri mnayofanya ya kutufahamisha, kutuelimisha na kutuburudisha kila siku.

    Pia napenda kuwashukuru wasimamizi na watangazaji kwa kuanzisha huduma ya ujumbe mfupi, ambapo wasikilizaji hutuma ujumbe kwa kupitia simu ya mkononi kwenda CRI huku wakitumia nambari maalumu ambayo ni 2001, ambapo baada kutuma msikilizaji naye hutumiwa ujumbe mfupi wa kuthibitisha kuwa ujumbe wake umefika na kupewa shikurani yaani "thank you for listening to redio China" mimi nashangaa kwani sio wasikilizaji wote wanaoelewa kuongea kingereza kwanini isiwe " ahsante kwa kusikiliza redio China kimataifa"

    Pongezi za dhati ziwafikie watangazaji wanaotuandalia kipindi chetu cha sanduku la barua, ambapo wasikilizaji huchangia mawazo na kupeana fikra kupitia kipindi hiki. Wasikilizaji wengi wanahamu ya kujifunza kichina kupitia kwenye kipindi chetu cha jifunze kichina, lakini ni matumaini yangu kuwa idhaa ya Kiswahili ya redio China kimataifa mtafanya juhudi ya kuwatumia wasikilizaji vitabu vya kuwa nasi jifunze kichina ili wapate urahisi wa kujifunza.

    Nafurahishwa sana na tangazo la kukaribisha kipindi cha kuwa nasi jifunze kichina ambalo ni "hujambo, ni hao, asante, xiexie kuwa nasi jifunze kichina" kama kunawezekana liwepo pia tangazo la kumalizia kipindi hiki, kwa mfano maneno ya kuagana kama vile zai jian kwaheri n.k. ahsante kwa leo.

    Shukurani za dhati msikilizaji wetu Philip Ng'an'ga Kiarie kwa barua yako, kwa kweli kwa suala la ujumbe mfupi kuhusu kujibiwa kingereza inatubidi tufanye hivyo, kwani namba hiyo inatumiwa na watu wa mataifa mbalimbali ambao wanajua Kiswahili na wasiojua Kiswahili, hata hivyo si tatizo kwani tunaamini kuwa watu wengi wajuao na wasiojua Kiswahili wanafahamu neno thank you. Na kuhusu kuwepo kwa tangazo la kufungia kipindi tumesikia ushauri wako tutangalia uwezekano. Ahsante sana.

    Sasa ni barua ya Geofrey Wandera wa Eveready Security Guard S.L.P 57333 Nairobi Kenya, anasema hii ni fursa nyingine ambayo ningependa kuwaarifu kuwa nimeshapokea kifurushi maridadi mlichonitumia, baada ya kupokea kifurushi hicho kutoka posta, nilielekea moja kwa moja hadi nyumbani kwangu nikiwa na furaha nyingi na huku moyoni nikiwa na hamu ya kutaka kujua nini kilichomo ndani ya kifurushi. Mara tu nilipowasili nyumbani nilimuita mke wangu "njoo hapa mezani tukifungue hichi kifurushi maridadi ambacho tumetumiwa na CRI kutoka China"

    Amini usiamini zawadi niliyokuwa nikiisubiri kwa muda mrefu, ndiyo ambayo ilikuwa imetumwa, punde si punde nilianza kulipekua boksi langu, na ndani mlikuwa na vitabu vya kujifunza kichina pamoja na CD. Kulingana na vidokezo vilivyomo ndani ya vitabu sita, kuna mambo kama vile historia ya chai kwa wachina, utamaduni wa wachina, vyakula vya wachina, biashara na mazungumzo ya wachina pamoja na mambo mengine mengi mazuri.

    Ingawa hiyo CD bado sijaisikiliza lakini mara tu nitakapo fanya hivyo bila shaka nitawajuza mengi yaliyomo. Mwisho napenda kusema asante sana kwa azimio lenu la kuimarisha mawasiliano bora na wasikilizaji wenu kote duniani. Zaidi ya yote bado natarajia mambo mengi makubwa kutoka kwenu, siwezi kumaliza barua hii bila ya kuyatakia maonesho ya kimataifa ya Shanghai kila la heri.

    Kwanza tunapenda kushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Geofrey Wandera kwa barua yako, tumefurahi kusikia zawadi ya vijitabu na CD za jifunze Kichina zimekufika, tunatumai kuwa utafanya haraka kujifunza, kwani chelewachelewa yaaumiza matumbo, na kwa kujifunza haraka utaweza kujua mambo mengi ambayo umeyaorodhesha na kikubwa zaidi ni kujua kichina. Ahsante sana.

    Na barua ya mwisho inatoka kwa msikilizaji wetu Nahimana Theophile wa S.L.P 173 Napula Msumbiji, anasema napenda kutoa shukurani za dhati kwa vitu mlivyonitumia, ila naomba mnitumie fulana ili nami nijihisi kuwa ni mjumbe wa redio China kimataifa. Hapa nilipo Msumbiji, siku zilizopita kulikuwa na maandamano ya wananchi kwasababu ya bei ya bidhaa muhimu kupanda ghafla kwa asilimia kubwa, ambapo watu walikuwa hawategemei hilo. Kwa hiyo ningekupasheni habari hii mapema sana iwezekanavyo ila nahisi siruhusiwi kwani hamkunipa jukumu hilo, naomba mnishirikishe kwa kutoa habari mbalimbali nikwa nimeruhusiwa rasmi.

    Shukurani msikilizajhi wetu Nahimana Theophile kwa barua yako, hivi sasa bado hatujawa na mpango wa kutuma fulana, lakini pale tu tutakapoanza kutuma na wewe pia tutakutumia, aidha suala la kutaka kutusaidia kutuma habari kutoka Msumbiji, hivi sasa bado hatujahitaji waandishi, ila tutakapohitaji au kufanya usaili kwaajili ya waandishi wa huko tutakuarifu. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako