• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za wasikilizaji

    (GMT+08:00) 2011-01-04 16:09:23

    Msikilizaji wetu Mchana J Mchana wa Morogoro Tanzania, ametuletea barua pepe yenye anuani mchanajo@yahoo.com akisema washindi mlio kwenda China nawapongeza sana, nadhani kwa sasa tumejumuika pamoja kuliletea taifa letu maendeleo, kwani hamkwenda kutalii tu, bali kuna mengi mliyo jifunza mlipokuwa China sasa basi zile chembe chembe mlizoambukizwa, mtuambukize na sisi ili tujisikie kama tuliosafiri na tukarudia njiani, pia tuweze kuyafanyia kazi kwa pamoja. tuwe kama wachina kazi kwenda mbele. Pia nawapa pongezi Fadhili na mama Chen kwa kazi zenu za kila siku. Mwanzoni nilikuwa nasikia sauti tu ya mama Chen lakini siku ya sherehe iliyofanyika Dar, nilimuona kupitia kipindi maalum kilicho rushwa kutoka China nilifurahi sana.

    Msikilizaji mwingine ni wa Godfrey Wandera wa Eveready Security Guard S.L.P 5733 Nairobi Kenya, naye anasema ziara ya wasikilizaji wenzangu watano kutoka Tanzania, ambao walitunukiwa nafasi maalumu kuitembelea China kwa siku 10, ambapo safari hiyo ilipata mafanikio bora. Ingawa siku ya kwanza ya ziara yao sikuipata vizuri lakini siku ya pili hadi ya 10 nilifanikiwa kuzinasa. Siku ya pili wenzangu hawa walitembelea jumba ama jengo la CRI ambapo waliona picha za watangazaji pamoja na wale wote waliowahi kufika ama kulitembelea jengo hilo.

    Siku ya tatu walitembelea uwanja wa Tianamen square pamoja na kasri la kifalme, siku ya nne walitembelea moja ya maajabu saba duniani ukuta mkuu uliopo Beijing ambao pia ni fahari ya China au moyo wa China, na kwa kutimiza msemo wa kichina usemao kama umefika Beijing na kutopanda ukuta mkuu wewe sio shujaa, wenzangu hawa waliupanda, hivyo wao sasa ni mashujaa halisi hongereni wenzangu. Siku ya tano walizuru mjini Shanghai na kulitembelea jumba la maonesho ya kimataifa yaliyokuwa yakiendelea, na sehemu waliyotembelea kwenye maonesho hayo ni kitengo maalumu cha wanahabari, siku ya sita bado walikuwa Shanghai ambapo walitembelea mnara wa lulu ama mnara wa Shanghai pamoja na kutembea kwenye njia ya vioo, siku hiyo mvua ilinyesha sana, lakini haikutatiza safari yao walisafiri kwa kupanda gari moshi kutoka Shanghai hadi Beijing.

    Siku ya saba walitembelea mtaa mmoja uliopo mjini Beijing ambapo waliingia ndani ya vichochoro na kukutana na wapiga ngoma ambao waliwatumbuiza. Ilipotimia siku ya nane walitembelea kasri la majira ya joto ama summer palace, pamoja na maktaba ya taifa ya China, iliyo na nyaraka za zamani pamoja na vitabu vilivyohifadhiwa kwa muda mrefu. Siku ya tisa walitembelea uwanja wa kiota ambao ni uwanja mkubwa zaidi nchini China, upatikanao mjini Beijing, ikikumbukwa kuwa uwanja huu wa kiota ndio uliotumika mwaka 2008 kwa ufunguzi na ufungaji wa sherehe za michezo ya Olimpiki.

    Na katika siku ya mwisho yaani siku ya kumi ambayo waliondoka walitembelea soko moja mjini Beijing, ambapo walipata kutumia lugha ya kibiashara, na ujanja wa wauzaji na wanunuzi, kwa kweli ulikuwa mchezo wa paka na panya kwani sokoni ama biashara ina lugha nyingi za ujanja. Mwisho natowa wasia wangu kwa hawa wenzangu watanzania watano, daima dawama kumbukeni hili siku zote kuwa kumbukumbu ni hazina kuu katika historia yoyote ile.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa S.L.P 504 Lindi Tanzania, anasema siku ya Jumatano tarehe 23 Septemba katika ofisi ya ubalozi wa China nchini Tanzania ilikuwa ni siku maalumu ya kukutana wasikilizaji wa idhaa ya kiswahili ya CRI. Sherehe ya kukabidhiwa zawadi wasikilizaji walioshinda chemsha bongo maalumu ya kuadhimisha miaka 45 ya uhusiano wa kinbalozi kati Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya watu wa Tanzania, kwenye sherehe hiyo tulioneshwa studio ya matangazo sehemu mbalimbali za watangazaji au wafanyakazi kwa kupitia DVD, matangazo hayo yaliendeshwa kwa umakini na mtangazaji na katika sehemu ya barua zilioneshwa barua zangu, ama kwa kweli CRI inaweka kumbukumbu za wasikilizaji wake. Naipongeza CRI pamoja na wafanyakazi wote nawatakia mafanikio mema katika kazi zenu, sitosahau kwa siku nyingi. Mwisho nasema ahsante kwa kupokea kifurushi cha vitabu vya jifunze kichina.

    Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu Mchana J Mchana, Geofrey Wandera na Gulam Haji Karim kwa barua zenu, ziara ya wasikilizaji wetu walioshinda nafasi maalumu imemalizikia, hata sisi pia imetuachia kumbukumbu nyingi sana, kwani wasikilizaji hao waliweza kuwawakilisha vyema wasikilizaji wote ambao hawajafika China, kwa kujionea mambo mengi mbalimbali, na uchangamfu wao pamoja na udadisi wao umewafanya watambue mambo mengi sana. Tunawashukuru sana kwa hilo, na tunawaomba wasikilizaji wetu wengine wote wasikate tamaa, kwani ipo siku nao watabahatika kuja kutembelea China kama hao wenzao waliotanmgulia, ahsanteni sana.

    Naye Hilali Nassor Kindy wa S.L.P 22 Oman anasema natoa shukurani kubwa kwa vitabu vya kujifunza lugha ya kichina, post card, na karatasi nzuri, nitafurahi kama mtanikumbuka kila mara ahsanteni.

    Sasa ni barua ya Naomi Cherotich Chesebe wa S.L.P 139-50201 Chaptais Kenya, anasema mimi nina umri wa miaka 11 na niko katika darasa la sita nchini Kenya. Mimi hupendelea sana kusikiliza redio China Kimataifa, hasa kusikiliza mafunzo ya lugha ya kichina na ningependa kujifunza lugha ya kichina na tamaduni za kichiana, hivyo nawaomba vitabu vya kichina, huku Kenya sisi tunawapata kwa njia muafaka kabisa, hasa maeneo ya Magharibi mwa Kenya.

    Kwanza tunapenda kukushukuru bwana Hilali Nassor Kindy kwa barua yako fupi tu, nasi tumefarijika kwa kusikia kuwa zawadi tulizotuma umepokea, sasa ni wakati wako wa kujifunza kichina bila ya kuingia darasani, na kwa upande wa msikilizaji wetu Naomi Cherotich Chesebe pia tunakushukuru kwa kuwa msikilizaji wetu ambaye ni mdogo sana, usijali tutakutumia vitabu vya kichina ili uweze kujifunza,ahsante sana.

    Na barua ya mwisho inatoka kwa msikilizaji wetu Lukas J Mangu wa S.L.P 610 Singida Tanzania, anasema nafurahi kutuma salamu zangu kwa watangazaji na wafanyakazi wote wa CRI, ni matumaini yangu kuwa nyote hamjambo na mnaendelea vyema na shughuli za kazi. Pia nasikitika kwa wale wote waliokumbwa na mafuriko, wengine kupoteza maisha na wengine kupoteza makazi, hivyo tupo pamoja katika majonzi.

    Katika miaka iliyopita mlikuwa mkitutumia nakala za majina ya washidi wa chemsha bongo kutoka nafasi maalumu hadi nafasi ya tatu, sasa hivi hamtoi imekuwaje? Pamoja na kadi za salamu pia hatupati. Kuhusu mawasiliano na redio China kimataifa kupitia KBC ya Kenya siku hizi hatuyapati, sasa je mnatufikiriaje sisi wapenzi wa CRI tuliopo hapa Tanzania, mjue kuwa hilo linatusikitisha, hivyo mngefanya uwezekano wowote ili nasi tupate mawasiliano. Mwisho naomba mtuwezeshe ili nasi tupate CD za mafunzo ya lugha ya kichina, nafurahi kuwasalimia wasikilizaji na wapenzi wote wa CRI pamoja na wananchi wote wa China nawatakia kila la heri katika maisha yao yote.

    Shukurani za dhati msikilizaji wetu Lukas J Mangu kwa barua yako ya masikitiko, lakini ni muda mrefu sasa umepita bila ya mawasiliano yoyote, hata hivyo kuhusu suala la kukosa matangazo ya CRI yanayorushwa na KBC, sasa juhudi zinafanyika ili muweze kusikia matangazo hayo kupitia TBC ya Tanzania hivyo vuta subira tu. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako