• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maisha ya uzeeni ya Wachina

    (GMT+08:00) 2011-01-20 14:26:40

    Wachina wana mtizamo tofauti na watu wa nchi za magharibi kuhusu maisha ya uzeeni. Kwa wazee wengi wa China maana kubwa ya maisha ya uzeeni ni kukaa zaidi pamoja na familia zao.

    Siku moja katika majira ya baridi mjini Beijing, upepo mkali ukiwa unavuma, mzee Sun Xichun mwenye umri wa miaka 80 na mkewe walifanya mazoezi ya asubuhi. Mzee Sun Xichun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika miaka 16 iliyopita baada ya kustaafu, kila siku asubuhi ni lazima atembee kwa miguu kwa umbali wa kilomita 5, jambo ambalo limekuwa ni kawaida kwake. Mzee Sun alisema,

    "Sisi tumepanga vizuri maisha yetu, kila asubuhi tunaamka saa kumi na mbili, na kula chakula cha asubuhi saa moja na nusu, kisha tunasafisha chumba na kwenda nje kutembea. Kila siku ninatembea kwa saa mbili, na kufanya mazoezi katika bustani ya karibu bila kujali hali ya hewa ni ya namna gani."

    Mzee Sun anaishi katika mtaa wa makazi ya Xiaoguan, eneo la Chaoyang mjini Beijing, ana watoto watano, ambao wote wanaishi mjini Beijing. Jambo linalowafurahisha mzee Sun na mkewe ni kwamba, watoto wao wote wanawatunza vizuri wazazi, wanapokuwa na nafasi wanarudi nyumbani kupiga soga nao. Wakati wa sikukuu jamaa karibu 20 wanakusanyika pamoja, mzee Sun alisema,

    "Watoto wote wanatupenda sana, tunaona furaha kweli. Wakati wa sikukuu watoto wote wanarudi nyumbani, na vyumba viwili vinajaa watu. Badala ya kula nyumbani, sote tunakwenda kula mgahawani."

    Katika siku ya kawaida, mzee Sun anapenda kusoma vitabu na magazeti. Majirani wanajua kwamba mzee Sun anajua mambo mengi, hivyo wanapomwona wanapenda kuongea naye kuhusu mambo makubwa ya nchi na mengine mbalimbali, pia vijana wengi wamekuwa marafiki naye bila kujali tofauti ya umri. Mzee Sun alisema,

    "Kila siku nasoma habari za Beijing na za nchi, hivyo najua mambo mengi. Napata ujuzi mwingi, na upeo wangu umepanuka. Vijana na watu wa makamo wanaponiona wanapenda kupiga soga nami."

    Katika miaka ya hivi karibuni, mzee Sun anavutiwa na matibabu ya Kichina, na mara kwa mara hutumia ujuzi aliojifunza kusikia mapigo ya moyo ya mkewe na wazee wengine katika makazi hayo, pia anawaelimisha namna ya kula chakula chenye lishe bora. Mzee Sun Xichun anaona kuwa wazee wanapaswa kutafuta wenyewe maisha yenye furaha.

    China imetekeleza sera ya uzazi wa mpango kwa zaidi ya miaka 30, hivi sasa idadi ya familia yenye mtoto mmoja imezidi milioni 100, na familia nyingi zinajumuisha wazee wanne, mume na mke na mtoto mmoja. Muundo huo unachukuliwa kuwa ni tatizo kubwa kwa utaratibu wa kuwatunza wazee. Tofauti na nchi za magharibi, wazee wengi wa China wanajitahidi kuwasaidia watoto wao kufanya kazi za nyumbani na kutunza na kuelimisha wajukuu. Wazee wa China wamekuwa "nguvu isiyoonekana" ya kusaidia maendeleo ya uchumi na utulivu wa jamii.

    Lakini sio wazee wote nchini China ni kama mzee Sun Xichun, ambaye amebahatika kuwa na watoto wengi ambao wanaishi karibu naye. Wazee wengi wanaishi peke yao. Bibi Zou Tianrong mwenye umri wa miaka 74 ni mmoja wao. Bibi Zou anaishi mkoani Henan, China. Ana watoto watatu wa kiume na mmoja wa kike. Miongoni mwao wawili wamekwenda nchini Marekani baada ya kuhitimu kutoka vyuo vikuu, na wengine wawili wanafanya kazi katika sehemu nyingine nchini China. Watoto hao wana shughuli zao, hivyo hawapati muda wa kurudi nyumbani kwa wazazi. Bibi Zou alisema,

    "Watoto wangu wawili wanakaa nchini Marekani, wanarudi nchini China kila baada ya miaka kadhaa. Safari iliyopita walirudi mwezi Oktoba mwaka jana. Na mtoto ambaye anakaa karibu nami zaidi anakuja kunitembelea kila baada ya miezi miwili."

    Hivyo ingawa bibi Zou ana umri wa zaidi ya miaka 70, lakini hakika yeye ni "nguzo" ya familia. Licha ya kumtunza mume wake, ambaye afya yake ni dhaifu, bibi Zou pia anapaswa kumtunza kwa makini mama yake mwenye umri wa miaka 102. Bibi Zou anasema amezoea maisha ya wazee watatu, alisema,

    "Kila siku napika chakula kwa watu watatu, nafua nguo na kusafisha chumba. Kama hatutaugua, maisha haya hayana matatizo."

    Familia ina umuhimu mkubwa kwa Wachina, watu wachache wanataka kuishi katika nyumba za wazee kwenye jamii wanapozeeka. Hivyo ingawa maisha ya bibi Zou Tianrong si rahisi, lakini bado anataka kuishi nyumbani kwake. Na asilimia 90 ya wazee wa China wanapozeeka, wanachagua kuishi nyumbani kwao.

    Kama walivyo wazazi wengine wa China, bibi Zou Tianrong na mumewe pia wanawakumbuka watoto wao, lakini ili watoto wao waweze kuendeleza shughuli zao vizuri na kuishi maisha mazuri, yeye na mumewe wanafarijiana na kupeana moyo. Bibi Zou alisema,

    "Katika miaka iliyopita nilipowakumbuka watoto wangu nilitaka kulia. Lakini sasa nimeelewa, na maisha yanapaswa kusonga mbele."

    Uchunguzi umeonesha kuwa karibu asilimia 50 ya wazee wa mijini nchini China wanaishi peke yao. Lakini shughuli za kuwatunza wazee kwenye nyumba za wazee zilizoanzishwa na serikali zimeanza muda mfupi tu. Hivi sasa kuna nyumba za wazee elfu 40, lakini haziwezi kukidhi mahitaji ya wazee wa China.

    Hivyo huduma zinazotolewa katika mitaa ya makazi ya kuwatunza wazee zimekuwa ni hatua mpya.

    Mwaka 2008 mtaa wa makazi ya Baoxiaoxincun anayoyaishi bibi Zou Tianrong yaliunda "kikundi cha utoaji huduma kwa wazee", ambacho kinatoa huduma kwa wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 70, ambao watoto wao hawaishi pamoja nao. Bibi Zou Tianrong alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, huduma na misaada inayotolewa na mtaani inamsaidia sana. Bibi Zou alisema,

    "Tukipata matatizo tunaomba misaada kutoka kwao, kwa mfano kusaidia kumbeba mama yangu kwenda ghorofa ya juu na chini. Wakati wa sikukuu, watu wa kujitolea wa mtaani wanatutembelea na kutuletea vitu mbalimbali. Mwaka jana walitununulia blanketi na vyombo vya umeme, wanatufuatilia na kutusaidia sana."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako