Rais wa Nigeria Bw. Goodluck Jonathan aliapishwa Jumapili mjini Abuja, na muda wake wa urais ni miaka minne. Wachambuzi wanaona kuwa changamoto kubwa inayomkabili rais Jonathan ni kuleta upatanishi nchini humo na kusukuma mbele maendeleo ya uchumi,.
Kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika katikati ya mwezi Aprili mwaka huu, rais Jonathan alimshinda kiongozi wa serikali ya zamani ya kijeshi Bw. Muhamadu Buhari ambaye ni Mwislamu kutoka kaskazini, na kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Nigeria. Lakini Waislamu wa upande wa kaskazini wanaona kuwa rais Jonathan ameharibu kanuni kuhusu Wakristo wa upande wa kusini na Waislamu wa upande wa kaskazini ya kushika madaraka kwa zamu, ambayo si kanuni rasmi lakini inakubalika kwa wanasiasa wa nchi hiyo. Rais wa zamani Olusegun Obasanjo ambaye ni Mkristo wa upande wa kusini alishika madaraka kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2007. Baadaye Bw. Umaru Yar'Adua ambaye ni Mwislamu wa upande wa kaskazini alichaguliwa kuwa rais, na alifariki dunia mwezi Mei mwaka 2010 baada ya kuwa madarakani kwa miaka mitatu. Bw. Jonathan ambaye wakati huo alikuwa makamu wa rais alikaimu wadhifa wa urais, na mwaka huu alishinda kwenye uchaguzi. Lakini Waislamu wa upande wa kaskazini wanaona kuwa rais wa awamu hii anatakiwa kuwa Mwislamu. Ili kuonesha kutoridhika kwao, baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, vurugu kubwa ilitokea kaskazini mwa Nigeria, na kusababisha vifo vya watu elfu kadhaa. Namna ya kufanya upatanishi kuwaunganisha Waislamu wa upande wa kaskazini, na kuzuia hali ya kuyumbayumba nchini humo ni changamoto ya kwanza inayomkabili rais Jonathan baada ya kushika madaraka.
Njia ya kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Nigeria na kuboresha maisha ya wananchi ni changamoto nyingine kubwa. Nigeria iliwahi kuwa nchi yenye uwezo mkubwa katika mambo ya kilimo, na ilikuwa ya kwanza kwa uzalishaji wa pamba na karanga duniani. Baadaye viwanda vya mafuta viliendelezwa vizuri, na serikali ilipata faida kubwa kutokana na uuzaji wa mafuta nje, lakini ilianza kupuuza kilimo, na tatizo kubwa la ufisadi likaanza. Hivi sasa zaidi ya asilimia 60 ya watu hawana ajira. Kutokana na kupungua kwa thamani ya dola ya kimarekani, mwaka huu bei ya vitu imeendelea kupanda nchini humo. Katika mwezi mmoja uliopita, bei ya dizeli ilipanda kwa asilimia 50, licha ya hayo, utoaji wa dizeli unakatishwa mara kwa mara, hili ni jambo la ajabu kwa nchi hiyo inayozalisha mafuta. Rais Jonathan anatakiwa kuwa na uwezo mkubwa katika kurekebisha muundo wa uchumi na kuinua kihalisi kiwango cha maisha ya wananchi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |