• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua za Wasikilizaji

    (GMT+08:00) 2011-05-31 16:05:01
    Msikilizaji wetu Lucas Josephat Mangu wa S.L.P 610, Kinampundu Singida Tanzania, anasema ndugu zetu wapendwa wa CRI, watangazaji na wafanyakazi wote, sisi wasikilizaji washirika wa CRI kutoka kijiji cha Kinampundu tunatoa pongezi kwa kazi nzuri mnayofanya, hivyo hongereni sana.

    Wasikilizaji kwa pamoja tunatoa masikitiko yetu makubwa kwa kutozipokea zawadi zetu mlizotutumia kwa njia ya posta, baada ya sherehe ya kutoa tuzo kwa washindi wa chemsha bongo iliyofanyika kwenye ukumbi wa ubalozi wa China nchini Tanzania. Sisi tunauhakika zilifika katika posta ya Singida maana walituletea kadi za kuchukulia mizigo EMS zilizotolewa tarehe 14 Disemba mwaka 2010, kadi hizo zilichukua muda mrefu hadi tulipozipokea tarehe 13 Februari mwaka 2011, tulipofika posta kuchukua mizigo walidai kuwa mizigo yetu imesharudishwa ilikotoka bila ya kupewa maelekezo yoyote.

    Hapo tulikuwa na mashaka kwamba huenda zawadi zetu zimechukuliwa na wafanyakazi wa hapo Posta. Hivyo kwa barua hii tunawaomba ndugu zetu mtujulishe ukweli kuhusu zawadi hizo kama zimerejeshwa au la. Na tunaomba mtupatie utaratibu wowote ule ili tuweze kuzipata zawadi zetu, ni matumaini yetu kuwa tutakuwa pamoja na tunawatakia kila la kheri katika kazi.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Lucas Josephat Mangu kwa barua yako, kwanza tunapenda kukupa pole wewe na wote waliokosa zawadi zao hapo Kinampundu, pia tunapenda kuwaambia kuwa msiwe na wasiwasi kwani tutajitahidi kukutumieni zawadi nyingine, hayo ni makosa ambayo yanatokea mara kwa mara kwenye posta, lakini si kitu tutajaribu kusawazisha kosa lililojitokeza. Ahsante sana.

    Msikilizaji wetu mwengine ni Ras Manko Ngogo anuani yake ya baruapepe ni rasmanko2003@yahoo.com naye anasema ndugu wa CRI, nimefurahia sana kuwasikiliza jinsi mnavyoandaa na kutuletea kipindi cha Utamaduni. Tathimini yenu ya maana ya methali zinazolenga maana moja kwa kichina na kiswahili, kunanifanya nivute fikra za kuwaomba mruhusu wasikilizaji kutuma methali kwa lugha zao mama. Niko tayari kufanya hivyo kwani kabila langu linazo nyingi mno. Mwisho, mpango wenu wa kutoa tangazo la kipindi na mada itakayotangazwa, siku moja au mbili kabla ni mzuri sana, kwani unatayarisha fikra za msikilizaji na hamu ya kusikiliza. Ahsante.

    Shukurani za dhati msikilizaji wetu Ras Manko Ngogo kwa barua yako, kwa kweli tumefurahi kuona unafuatilia kipindi chetu cha utamaduni, lakini tunasikitika kukueleza kuwa methali tunazotumia kwenye kipindi ni za Kiswahili kwasababu watu wengi wa Afrika Mashariki wanakifahamu, tukitumia methali za lugha za makabila itakuwa vigumu kwa wengine kuelewa. Ahsante sana.

    Sasa ni barua ya Al- Ustadh Salim Muchila Said wa S.L.P 167-20227 Kenya anasema kwanza kabisa nawasalimu watangazaji wote wa redio China kimataifa, nikitumai kwamba mu bukheri wa afya. Naomba kuwa shabiki wa salamu katika redio china kimataifa kwani mimi napenda kusikiliza matangazo yenu, kwa hiyo ikiwa ni mara yangu ya kwanza kutuma barua naomba mnitumie kadi za salamu ili niendelee kuwa shabiki sugu, nawatakia kazi njema.

    Msikilizaji wetu Lulyeho K. Madale wa S.L.P 46254 Dar es salaam, anasema nawapongeza sana CRI kwa matangazo mazuri. nawaaahidi kuwa nanyi mwaka huu wa 2011, nitaendelea kuwasikiliza na kuwapata vizuri. mwisho nawatakia kazi njema.

    Na mwisho ni Barua kutoka kwa Bwana wanjala Ainea Mswahili wa S.L.P 292 Kimilili Kenya naye anasema narudisha shukurani nyingi kwa watangazaji wa redio China Kimataifa kwa zawadi mliyonitumia, pia kadi za salamu ambazo nilizikosa kwa muda, sasa nimepata ningependa nitumiwe picha ya mji wa Beijing ili nijionee mwenyewe. Ahsante sana.

    Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu Salim Muchila Said, Lulyeho K. Madale na wanjala Ainea Mswahili kwa barua zenu, kwanza tungependa kumjibu Salim Muchila kuwa tayari tumekupokea shabiki wetu mpya na kukuweka kwenye orodha ya mashabiki wetu, pia tutakutumia kadi za salamu pamoja na zawadi nyingine nyingi tunazotoa kwa wasikilizaji wetu wote. Tunaomba muendelee kusikiliza vipindi vyetu na kutoa maoni. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako