• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Zhu Weishang: kupanda matufaha ni kupanda furaha

    (GMT+08:00) 2011-07-11 20:12:48

    Ni saa nne asubuhi. Jua limechomoza na kuleta hali ya uvuguvugu kwenye matufaha makubwa, mekundu na ya kutamanisha. Zhu amekuwepo shambani hapo kwa muda wa saa mbili. Anamiliki shamba hilo na matufaha hayo ni hazina yake. ..

    "huwa nafanya kazi hapa kwa saa kumi kila siku, nakagua kama kuna matatizo yanayoikumba miti ya matufaha na kurutubisha ardhi. Sidhani kama huu ni muda mrefu, napenda kufanya kazi kwenye shamba langu. Napenda matufaha yangu, na nayachukulia kama ni watoto wangu."

    Zhu Weishang amekulia Yan'an, mji unaojulikana kama ni "ardhi takatifu ya mapinduzi ya Wachina". Kihistoria, mji wa Yan'an ulikuwa masikini sana, na tokea miaka ya 80, wakulima wengi walianza kupanda miti ya matufaha ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umasikini.

    Zhu Weisheng alianza kupanda matufaha miaka 21 iliyopita, na hali ya hewa mjini Yan'an inafaa kwa kilimo cha matufaha. Sasa Zhu amekuwa na shamba lake la matufaha na anapata Yuan milioni 60, sawa na dola za kimarekani milioni 8.5 kila mwaka. Yeye na mkewe wanatunza shamba hilo. Katika majira ya kuchipua na baridi, shamba hili halihitaji kutunzwa sana, lakini katika muda wa pilikapilika, huwa wanafanya kazi kuanzia alfajiri hadi jioni. Mara nyingi, wanakosa muda wa kula hivyo wanakula tambi za haraka au mikate ya kichina kama chakula cha mchana.

    Zhu haamini kuwa kufanya kazi kwa muda mrefu kunamchosha, hivyo anatumia siku chache kupumzika. Ameweka moyo wake wote katika matufaha yake. Akiangalia matufaha hayo mazuri chini ya mwanga wa jua la kupendeza wakati wa mchana, Zhu anatabasamu na kusema kupanda miti ya matufaha kumempa furaha nyingi.

    "kadri ninavyofanya kazi kwa bidii, ndivyo matufaha yanakuwa mazuri zaidi na nitakavyochuma pesa nyingi zaidi. Hivyo kwanini nisifanye kazi kwa bidii? Sasa nina nyumba yangu yenye ghorofa mbili na vyumba kumi, na ujenzi wake ulinigharimu kiasi cha Yuan elfu 40. Nina magari mawili, nayatumia kusafirisha matufaha yangu. Nina watoto wawili, ambao wanasoma mjini Xi'an, kaskazini magharibi mwa China. Kila siku wanatumia yuan 60 kila mmoja kulipia nyumba waliyopanga. Pesa zote hizo zinatokana na shamba la matufaha. Bila matufaha, sina kitu chochote. Kila ninapoangalia shamba langu, naangalia furaha yangu."

    Baada ya kusema hayo, Zhu anaendelea na kazi yake. Sasa yuko katika pilikapilika za kufunga matufaha yaliyoiva kwenye maboksi yaliyoandikwa "Weishang" kila upande. Katika majira ya kuchipua, huwa anashughulika na upandaji wa mbegu. Wakati wa majira ya joto, anafanya kazi kwa makini na kutunza miti hiyo ya matufaha kuepukana na maafa ya kimaumbile na magonjwa. Majira ya mpukutiko, mavuno yanapatikana. Zhu anasema kuvuna matufaha kunahitaji uangalifu.

    "tunapaswa kukata kila tufaha katika sehemu maalumu. Kama ukichagua sehemu isiyo sahihi, tufaha halitakuwa na ladha nzuri. Kwa wastani, kila tufaha linaweza kudumisha ladha yake nzuri kwa muda wa nusu mwaka. Vilevile unapaswa kuwa mwangalifu kuhusu mazingira ya kuchuma matufaha, ama sivyo huenda utayaangusha matufaha mengine yaliyoiva sana, na ni hasara."

    Zhu amejitahidi kuzalisha matufaha yenye ladha nzuri zaidi katika miaka 10 iliyopita. Ametembelea na kujifunza kwenye mashamba ya ikolojia nchini Japan, ambapo alifurahishwa kuona mbolea za ogani huko. Zhu anasema ili kuzalisha tufaha zuri, kufanya kazi kwa bidii pekee hakutoshi. Anapaswa kutilia maanani teknolojia mpya na njia za kisasa za upandaji. Hivi karibuni alimwajiri mkulima mmoja kutoka mkoa wa Shan'xi mwenye uzoefu mkubwa katika kupanda tufaha kuwa mshauri wake. Mshauri huyo atatembelea shamba lake mara moja kila mwezi na kufanya kazi pamoja naye. Zhu anasema msemo unaomwongoza katika upandaji ni "kitu wengine wasichokuwa nacho, ninacho; walichonacho wengine, nina kizuri zaidi." Kutokana na utunzaji na uvumilivu wakati wa kupanda miti ya matufaha, kila mwaka anapata mavuno makubwa zaidi kuliko ya mwaka uliopita.

    Unafika mchana jua linawaka kwenye anga la bluu. Marafiki kadhaa wa Zhu wanamtembelea na kusherehekea mavuno yake, miongozi mwao yuko mama mkwe wake. Mzee huyo anamshukuru Zhu kwa maisha mazuri anayompatia. Anapendezwa na utayari pamoja na moyo wa kujifunza alionao Zhu.

    "Anafanya kazi kwa bidii sana. Mchana anashinda shambani, na usiku anasoma majarida na vitabu. Mara nyingi namwambia hana haja ya kufanya kazi kwa bidii namna hiyo lakini hanisikii."

    Zhu haoni majivuno kutokana na sifa hizo. Anaendelea kufunga matufaha hayo kwenye maboksi. Anatarajia kuwa iko siku matufaha yake yatajulikana kote duniani.

    Jua limetua na baridi kidogo inakuja. Baada ya kumaliza kazi ya siku nzima, Zhu anavaa koti lake, anwashukuru wasaidizi wake na kuelekea nyumbani akiambatana na mama yake. Huenda sentensi moja inaweza kuelezea maisha ya Bw huyo mwenye ari kubwa, "kupanda miti ya matufaha ni kupanda furaha". Tunamtakia kila la heri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako