• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mchezo wa redio wa kabila dogo "sigh of snow mountain" waelimisha watu jinsi ya kujikinga na ukimwi

    (GMT+08:00) 2011-07-17 18:52:22

    (sauti kutoka kwenye mchezo wa redio)

    Huu sio mchezo wa kawaida tu, bali ni mchezo unaoelimisha jinsi gani ya kujikinga na ukimwi kwa lugha ya kabila dogo la Wanaxi. ..

    Mchezo huo unaitwa "sigh of snow mountain", uliandikwa na mwandishi wa michezo wa kabila la Wanaxi, na kuigizwa na waimbaji na wacheza dansi maarufu wa kabila hilo.

    Mtayarishaji Liu Xiaojun anasema mchezo huo unahusu maisha halisi.

    "Mchezo huo wa redio unasimulia hadithi za familia mbili. Jamaa wa familia moja aliambukizwa virusi vya ukimwi kutokana na kuongezwa damu yenye virusi vya ukimwi baada ya ajali ya barabarani. Jamaa wa familia nyingine aliambukizwa kutokana na kufanya mapenzi bila kinga na kahaba. Hadithi hizo mbili zinahusu maisha ya watu."

    He Xuexian, Mnaxi mwenye umri wa miaka 70 anasema amejifunza mengi kupitia mchezo huo wa redio.

    "Naona ni vizuri kuusikia kwa lugha yangu mwenyewe. Hadithi inatufunza tuwe na matumaini na tujikinge na virusi vya ukimwi, ili tuishi maisha mazuri na ya furaha.

    Mchezo huo wa redio ni sehemu ya mpango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni, Elimu na Sayansi UNESCO kuhusu kuwawezesha watu wa makabila madogo madogo waongeze ufahamu.

    Mpango huo ulianzishwa miaka minane iliyopita, ambapo watafiti walitambua kuwa watu wa makabila mengi madogo madogo walishindwa kuongea, kusoma wala kuandika kichina sanifu.

    UNESCO iliamua kutumia vipindi vya redio, michezo ya kuchekesha, tamthilia na filamu kuelimisha namna ya kujikinga na ukimwi.

    Mpango huo umetayarisha michezo ya redio kwa lugha za makabila sita tofauti, ambayo yametangazwa kwenye mkoa wa Yunnan na mkoa unaojiendesha wa kabila la Zhuang wa Guangxi nchini China.

    Daktari Heather Peters kutoka UNESCO anajivunia sana mradi huo.

    "Kutokana na mradi huo, msaada wetu unaweza kuwafikia watu ambao hawajawahi kuupata awali. Michezo mingi ya redio iliyoandaliwa na serikali kuhusu jinsi gani ya kujikinga na ukimwi haikuandikwa kwa lugha ya makabila madogo madogo. Kama ingekuwa, ingetafsiriwa kutokana na maelezo yaliyokuwepo kwa lugha ya taifa. Na vilevile tunapata fursa ya kueneza utamaduni wao na lugha."

    UNESCO imeshirikiana na vituo vya redio vya huko kwa ajili ya kurusha hewani michezo hiyo ya mafunzo redioni, na wanavijiji hupewa nakala za michezo hiyo kwenye CD.

    Daktari Peters anasema matokeo yanatia moyo.

    "Katika sehemu wanayoishi watu wa kabila la Wawa, mabadiliko yameshuhudiwa. Kwa mfano, ufahamu wa kutumia kondomu kwa ajili ya kujikinga na virusi vya ukimwi umeongezeka hadi asilimia 72 kutoka asilimia 31. Awali asilimia 70 ya wanavijiji waliamini kuwa watu waliambukizwa virusi vya ukimwi kwa kuumwa na mbu, lakini baada ya kuusikia mchezo huo, idadi hiyo ilishuka hadi asilimia 25. Mabadiliko hayo ni dhahiri. Mchezo wa redio umewafanya wanavijiji kuanza kuwajali watu walioambukizwa virusi vya ukimwi kwenye jamii hiyo."

    Mradi huo umeungwa mkono na serikali za mitaa na taasisi za utafiti.

    Naibu mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Jamii cha Yunan Bw. Yang Fuquan anahimiza serikali kuongeza juhudi zake katika vita dhidi ya ukimwi.

    "Labda serikali inaweza kuwanunulia watu wa huko DVD, VCD na maandishi ya tamthilia. Serikali ina njia mbalimbali za kuwahamasisha watu hao kupata elimu, kama vile kutuma maofisa kuandaa maelezo ya elimu hiyo. Serikali pia inaweza kushirikiana na mashirika ya kimataifa ikiwemo UNESCO kufanya kazi halisi zaidi. Matokeo yatakuwa mazuri zaidi"

    China imetangaza mpango wa kuzuia na kudhibiti maambukizo ya virusi vya ukimwi katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Mpango huo unazingatia kueneza habari zaidi katika vijiji na sehemu wanayoishi watu wa makabila madogo madogo. Kama ilivyofanya UNESCO, mpango huo pia unalenga kutumia vyombo vya habari ikiwemo redio, televisheni na filamu ili kuwaelimisha watu wa China jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa ukimwi.

    Filamu yasimulia maisha ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi "Together"

    Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia ugonjwa wa ukimwi UNAIDS linakadiria watu elfu 740 nchini China wanaishi na virusi vya ukimwi. Mwendeshaji filamu wa China, Zhao Liang anaeleza kwa karibu maisha yao kwenye filamu ya tukio "Together" yaani pamoja.

    Filamu hiyo inasimulia kwa undani jinsi filamu "maisha ni muujiza" ilivyotengezwa na mwendesha filamu wa China, Gu Changwei. Filamu hiyo itakayoonyeshwa hivi karibuni pia ni taswira kamili ya maisha ya watu walioambukizwa virusi vya ukimwi nchini China.

    Filamu ya "Tuko Pamoja" hivi majuzi ilionyeshwa kwenye maonyesho ya filamu ya kifahari mjini Berlin nchini Ujerumani.

    (sauti kutoka kwenye filamu)

    Hiyo ni sehemu ya filamu ya Zhao Liang "Tuko Pamoja". Jamaa aliyeambukizwa virusi vya ukimwi anaelezea jinsi anavyoogopa kutoka nje ya nyumba yake kutokana na hofu ya kusemwa wanakijiji.

    Zhao Liang anasema mwanamume huyo hapaswi kuishi hivyo.

    "Iwapo watu wasiokuwa na virusi vya ukimwi wataelewa maisha ya walio na virusi hivyo basi hawatawaogopa. Wazo la filamu hiyo lilitokea pale mwendesha filamu Gu Changwei alipomtaka Zhao kuwa mhusika mkuu kwenye filamu "maisha ni muujiza"

    Baadhi ya watu wanaoshiriki kwenye filamu hiyo wanaishi na virusi vya ukimwi.

    Mtoto aliambukizwa na mama.

    Mwanamke mmoja aliambukizwa kutokana na kuongezwa damu yenye virusi.

    Zhao pia anakutana na watu wengine wenye virusi kutoka sehemu mbalimbali nchini China. Anakutana nao kwenye mtandao wa kuwasiliana moja kwa moja. Baada ya hapo anaonyesha mawasiliano hayo kwenye filamu hiyo.

    Zhao anaeleza kuwa kwenye mawasiliano hayo anapata kuijua dunia nyingine ngeni ambayo hakuwa anaifahamu. Huenda marafiki zako au watu mnaofanya kazi nao wanaishi na virusi hivyo bila wewe kujua. Wanaishi na siri. Ni kupitia kwa mtandao tu ambako wanaiweka hali yao wazi, kuwa wanasaidiana kutatua matatizo yao.

    Dan Edward anasema mawasiliano ya moja kwa moja ya mtandao ndio yaliyogusa hisia za wengi kwenye filamu hii. Yeye ni mhariri kwenye tovuti ya jarida la Beijinger na pia anatunga filamu huru kwenye blog yake, Screening China.

    "Unapozungumzia masuala kama ukimwi nchini China, ni rahisi kuchukuliwa kama dhana tu kwa kuwa hayana umuhimu kwa maisha yao ya kila siku. Kwa hiyo kusikia matukio ya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini China imekuwa ni kama kuwafichulia wachina. Edward anasisitiza kuwa "Pamoja" imeweka wazi haja ya elimu. Wahusika kwenye filamu hiyo huandaa wakati wa kupokea ushauri kutoka kwa wataalam wa ukimwi. Ni wazi kuwa wengi wao hawana ufahamu wa kutosha kuhusu ugonjwa huo, kwa kuwa wanauliza maswali kama, wajua, tunaweza kupata ukimwi kwa kuwagusa watu wenye virusi na mambo kama hayo."

    China haiko peke yake.

    Marta Jagustyna ni meneja wa mpango wa Shirika la Pact linalofanya kazi barani Asia kuimarisha maisha ya watu wenye virusi vya ukimwi.

    "kwa sababu matukio ya unyanyapaa pia yanatokea kwenye nchi nyingine, lakini yanajitokeza katika njia tofauti. Ni vigumu kupima viwango vya unyanyapaa na kusema matukio hayo ni mengi katika nchi fulani kuliko nyingine."

    Jagusztyn anasema kuushinda unyanyapaa si kwa njia ya elimu pekee. Ni lazima sheria zitungwe zitakazowalinda watu wenye virusi vya ukimwi….na kuwaona tena watu hao wakifurahia utamaduni unaofuatwa na wengi kama vile tamthilia."

    "Tunachohitaji kufanya katika kupambana na unyanyapaa ni kuweka mifano mema ya kuigwa. Itakuwa vyema kuwaona watu wenye virusi vya ukimwi wakijitokeza na kujitangaza, na kusema mimi naishi na virusi vya ukimwi na nakufahamisha, na sijali na naendelea kuishi maisha ya kawaida. Kuna haja kwa watu kujitokeza kimasomaso na kuzungumza lakini ni wazi kuwa sitamlazimisha mtu kufanya hivyo kwani najua kwa mtu wa kwanza kufanya hivyo, matokeo yatakuwa hatari zaidi."

    Huenda maonyesho ya filamu ya Berlin yataiweka filamu ya "Tuko Pamoja" kufuatiliwa zaidi duniani…… Lakini Zhao anasisitiza kuwa anawalenga zaidi watu wa China.

    "Kwa sababu hili ni suala linalohusu China, bila shaka natarajia kuwa wachina wataitazama filamu hii……hiyo ina maana kuwa juhudi zetu za mwaka mmoja hazitakuwa bure."

    Hivi sasa, filamu "Tuko Pamoja" imeonyeshwa tu kwenye kumbi ndogo ndogo za maonyesho. Lakini itatolewa tena na kuonyeshwa sambamba na filamu "maisha ni muujiza" kati ya Machi na Mei mwaka huu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako